Home Habari za michezo MKUDE:- ROHO YANGU ILIKUWA YANGA TU….

MKUDE:- ROHO YANGU ILIKUWA YANGA TU….

Mkude atua Yanga

Kiungo wa klabu ya Yanga SC, Jonas Mkudde ametoa kauli yake ya kwanza mara baada ya kujiunga na miamba ya soka nchini Yanga Sc.

Ikumbukwe kuwa, Mkude ameitumikia Simba kwa takribani miaka 13 tangu alipojiunga nayo akiwa mdogo mpaka hivi karibuni ambapo klabu hiyo ilitangaza kuachana naye.

“Ninapolazimika kufanya maamuzi magumu, huwa naisikiliza roho iliyondani yangu inachotaka.Roho hiyo ilikuwa ni Yanga tu,” amesema Mkude.

ALIVYOTUA YANGA

Miaka 13 ya Jonas Mkude ndani ya Simba ilikuwa ni ya mafanikio, changamoto, furaha na panda shuka za hapa na pale.

Mkude ni zao la Simba B na ndiye mchezaji wa mwisho tutoka ndani ya timu hiyo baada ya wachezaji wenzake waliopandishwa mwaka mmoja kusambaratika na kwenda kujaribu maisha mengine nje ya Simba.

Nyota hao wengine, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Edward Christopher, Abdallah Seseme na wengine, lakini kiungo huyo hakujumuishwa moja kwa moja kama wenzake.

Mkude ameanza kucheza kwenye timu ya vijana ywa Simba 2010, kabla ya 2011 kupandishwa timu ya wakubwa na kuwa msimu wa kwanza kwake katika Ligi Kuu Bara.

Tangu alipoingia Simba, Mkude, ambaye ni maarufu kwa jina la utani la ‘Nungunungu’, hakuwahi kutoka, licha ya misukosuko kadhaa aliyokumbana nayo wakati mwingine kutokana na mambo ya utovu wa nidhamu.

Katika miaka hiyo 13, Mkude, kuna wakati alikuwa nahodha wa kikosi hicho kabla ya kuvuliwa kitambaa akiwa kambi ya maandalizi ya msimu nchini Afrika Kusini.

Kiungo huyu mkabaji ametwaa mataji ya kujivunia ambayo kuna baadhi ya wachezaji waliodumu kwa muda mrefu kwenye vikosi vyao hawajawahi kutwaa.

Mchezaji huyu wa kimataifa wa Tanzania amebeba kila kitu ukiondoa taji la mashindano ya kimataifa (CAF) kwa ngazi ya klabu, lakini kwa hapa ndani kakomba kila kitu kuanzia Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC), Ngao ya Jamii, Kombe la Mapinduzi na mengineyo yaliyoibuliwa na kufa.

Rekodi zinaonyesha kuwa msimu wa kwanza wa kuichezea Simba, Mkude alibeba taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, tena kwa kishindo, kwani alikuwepo kwenye kikosi kilichoinyoa Yanga mabao 5-0.

Kwa waliosahau, Mkude aliingia kipindi cha pili kumpokea kaka yake, Mwinyi Kazimoto, wakati vijana wa Jangwani wakipigwa kama ngoma na Wekundu wa Msimbazi waliokuwa chini ya mwenyekiti, Ismail Aden Rage.

Kisha akatwaa mengine manne mfululizo kuanzia msimu wa 2017/18, 2018/19, 2019/20 na 2020/21, pia amebeba Ngao ya Jamii mara nne, kuanzia 2012, 2018, 2019 na 2020, kabla ya Yanga kutibua misimu miwili mfululizo iliyopita.

Mkude pia alibeba ASFC mataji matatu ya msimu wa 2016/17, 2019/20 na 2020/21, kabla ya mataji hayo kuhamia Jangwani alkikosajiliwa, wakati kwa Kombe la Mapinduzi, mwamba kabeba mara tatu kati ya mataji manne iliyotwaa Simba.

Mkude katwaa nao 2011, 2015 na 2022, taji alilolikosa ni lile la 2008, kwani wakati huo alikuwa yupo Mwanza na huenda hakufikiria kama angekuja kuichezea Simba kwa mafanikio hayo.

Msimu ujao, Mkude atakuwa anavaa jezi ya njano na kijani akiitumikia timu ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Lakini katika kikosi cha Yanga, Mkude anakutana na upinzani mzito katika eneo la kiungo, ambalo limekuwa silaha kubwa kwa miamba hiyo misimu miwili mfululizo.

SOMA NA HII  NYOTA MTIBWA SUGAR AJIFUNGA POLISI TANZANIA