Home Habari za michezo MAJERAHA YAMPONZA BOCCO, SIMBA WACHUKUA MAAMUZI MAGUMU

MAJERAHA YAMPONZA BOCCO, SIMBA WACHUKUA MAAMUZI MAGUMU

Habari za Simba SC

Dar es Salaam. Majeraha ya mara kwa mara ya nahodha John Bocco, ni sababu kubwa iliyoishawishi Simba kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Shaban Chilunda uhamisho uliokamilika juzi.

Chilunda aliyewahi kuitumikia timu ya taifa ‘Taifa Stars’ na pia klabu ya CD Tennerife ya Hispania, alijiunga na Simba juzi na siku yoyote kuanzia leo ataungana na kambi ya maandalizi iliyopo nchini Uturuki.

Kutokana na kuondoka kwa Habibu Kyombo, mmoja wa viongozi ndani ya Simba ameliambia gazeti hili kuwa walihitaji kusajili mshambuliaji wa kati mzawa mwenye uzoefu wa mashindano ya ndani na kimataifa anayeweza kuvaa viatu vya Bocco pindi anapokosekana, ambapo chaguo likawa Chilunda.

“Chilunda ni mchezaji mzoefu na ukiangalia katika washambuliaji tulionao ukiondoa Bocco (John), washambuliaji wengine wa kati hawana uzoefu mkubwa. Mfano Mohamed Mussa hajatimiza hata msimu mmoja baada ya kumsajili kutoka Zanzibar na Willy Onana ndio kwanza amesajiliwa hivyo alihitajika mzawa ambaye anaweza kuwa msaada pindi wengine wanapokosekana,” kilisema chanzo ndani ya klabu hiyo.

Uamuzi wa kumnasa Chilunda umekolezwa zaidi na gharama ndogo ambayo Simba imetumia kumsajili ambapo Simba haijatumia fedha nyingi kwa vile alikuwa huru kwani hakuongeza mkataba Azam baada ya kumalizika msimu uliopita.

Baada ya kumtema Kyombo, Simba ilibaki na washambuliji wawili wa kati wazawa ambao ni Bocco na Musa huku ikiwa na wengine watatu wa kigeni kina Willy Onana, Moses Phiri na Jean Baleke.

Hata hivyo, ukiondoa Baleke, Onana hutumika pia nafasi ya winga kama ilivyo kwa Phiri aliyekosa mechi nyingi msimu uliopita kutokana na majeraha na ameonekana kutomshawishi vya kutosha kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kikosi cha kwanza. Chilunda alijiunga na Azam 2016 akitokea kikosi cha timu hiyo cha vijana wenye umri chini ya miaka 20 ambapo aliitumikia kwa miaka miwili kisha akauzwa Tennerife aliyoitumikia kwa mwaka mmoja kisha akatolewa mkopo kwenda CD Izarra.

Alidumu Izarra miezi sita kisha akarejea Tennerife ambayo 2019 ilimrudisha kwa mkopo Azam ambako baadaye alijiunga moja kwa moja hadi Novemba 2020 alipouzwa kwenda Maghreb Tetouan ya Morocco aliyoichezea miezi sita baada ya hapo akavunja mkataba wa kuitumikia.

Januari 2022, alijiunga tena na Azam aliyoichezea hadi Januari, mwaka huu ambapo walifikia makubaliano ya kutoongezewa mkataba mpya na hivyo kumfanya abaki kuwa mchezaji huru. Mbali na Chilunda, Simba pia inaripotiwa imemnyakua beki wa Geita Gold, Hussein Kazi na hivyo kufanya idadi ya wanaocheza nafasi ya beki wa kati kufikia wanne wengine wakiwa ni Enock Inonga, Che Fondoh Malone na Kennedy Wilson.

Gazeti hili linafahamu kuwa mara baada ya kukamilisha usajili huo, wachezaji hao wanaweza kuondoka leo au kesho kwenda Uturuki iliko kambi ya timu hiyo kujiandaa na msimu mpya wa ligi.

Hadi sasa Simba imeshafanya usajili wa wachezaji saba ambao ni Malone, Onana, Aubin Kramo, David Kameta, Kazi, Chilunda, Fabrice Ngoma.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA KESHO ...MASTAA HAWA WANNE WA SIMBA KUIKOSA AZAM FC...