Home Habari za michezo ACHANA NA YANGA, SIMBA SASA WAPENYA KIMATAIFA KAMA MASKHARA

ACHANA NA YANGA, SIMBA SASA WAPENYA KIMATAIFA KAMA MASKHARA

KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua kwa mazoezi kujiandaa na msimu mpya ikiwa jijini Ankara, Uturuki ikiwa inajiandaa kupokea mastaa wengine akiwamo Luis Miquissone na Clatous Chama, huku wakilainishiwa mapema kwenye Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuanza Agosti 15.

Simba ni wawakilishi pekee wa michuano mipya ya African Football League itakayoanza Oktoba, ikiwa ni miezi miwili tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara na ile ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika ambayo timu hiyo itaishiriki sawia na Yanga, Azam na Singida Fountain Gate.

Kutokana na kubanwa na ratiba ya michuano hiyo, Bodi ya Ligi (TPLB), imetanga kuilegezea Simba kwenye ratiba ya mechi za ligi kuu msimu ujao, pia ikiweka msimamo kufungia viwanja ambavyo havitakuwa na ubora wa kutumika.

Hivi karibuni CAF ilitoa taarifa kwa wanachama wao kuona namna gani timu shiriki michuano hiyo mipyazinapewa ratiba rafiki katika ligi zao za nchi husika jambo ambalo TPLB imesema itazifanyia kazi kwa kuweka ratiba rafiki kwa Simba na ligi kwa ujumla ili kusiwe na viporo vingi.

Katika mahojiano maalumu na Ofisa Habari wa TPLB, Karim Boimanda, alisema mechi ambazo Simba haitacheza wakati wa michuano hiyo hazitazidi tatu huku timu zingine zikiendelea kucheza kama kawaida.

“Simba watabeba mechi hizo kama viporo na baada ya mashindano hayo tutaangalia namna gani ya kuvicheza bila kuwaumiza wao na kutoathiri ratiba ya Ligi Kuu. Ni hivyo hivyo itakavyokuwa hata kwenye mechi zingine za CAF za Simba, Yanga, Azam na Singida zitakuwa zinapangiwa tarehe nyingine,” alisema Boimanda na kuongeza;

“Ratiba wakati wa mechi za CAF kwa wawakilishi wetu haitakuwa na tofauti na msimu uliopita, kwani tumezingatia kalenda ya CAF na FIFA, ratiba kamili itatolewa muda si mrefu baada ya hii ya awali.”
Kuhusu ubora wa viwanja kwa kuzingatia matakwa ya Club License, Boimanda alisema; “Kamati ya Leseni iliyo chini ya TFF ilianza kukagua viwanja hivyo, ila hatutasita kufungia viwanja ambavyo havitakuwa na ubora hata kama vimekaguliwa.

“Tunasema hivi kwasababu wamiliki wa uwanja mara wanapokaguliwa basi wanavitelekeza viwanja hivyo haviwagiliwi maji hivyo vinarudi kuwa vibovu, ikumbukwe kuwa utunzaji wa viwanja ni wa muda wote hata kama ligi imemalizika.”
TPLB tayari ilitangaza tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu Agosti 15, Championship inatarajia kuanza Septemba 2 wakati First League itaanza Oktoba 21 mwaka huu

SOMA NA HII  KOCHA TP MAZEMBE, WYDAD WATAJWA KUTUA SIMBA....SIKU YA KUTANGAZWA HII HAPA...