KIPA wa zamani na kocha wa makipa, Ivo Mapunda amesema kipa mpya wa Simba, Jefferson Luis Szerban anatakiwa kuthibitisha ubora wake kwani ameingia kwenye timu ambayo ina kipa namba moja wa timu ya Taifa, Aishi Manula.
Simba imemsajili kipa huyo raia wa Brazil kwa mkataba wa miaka miwili, kipindi hiki ndiye atakuwa akisimama langoni kwani Manula anauguza majeraha yake na atakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu.
Akizungumza na Mwandishi, Ivo ambaye aliwahi kuzidakia Yanga, Simba, Azam FC na Taifa Stars alisema anaamini Manula atakapopona atarudi kwenye ubora wake na ndiye kipa namba moja wa Simba.
“Wote wana changamoto, ni ngumu sana kupambana na kipa namba moja wa timu ya Taifa, inawezekana ni kipa mzuri ila anapaswa kufanya kazi kubwa kuhakikisha anawapa Simba kile walichokitarajia na kinachozidi ubora wa Manula.
“Sio kila mchezaji wa kigeni anayesajiliwa anakuwa na uwezo wa kucheza, Luis ametoka kwenye nchi ambayo soka limezaliwa huko, tunapenda kuona tofauti yake kwa kiwango kikubwa,” alisema Ivo.
Ivo alisitiza anamfahamu Manula hata kama ana mapungufu ambayo hayamfanyi kutokuwa namba moja ndani ya Simba upande wa makipa.
“Kuuguza majeraha kuna mwisho na ninavyomfahamu Manula hawezi kukubali kupoteza namba kwa sababu tu ametoka kwenye majeraha, ni kipa mpambanaji, namba yake iko wazi kabisa pale Simba. Urefu wa Mbrazili huyo anaweza akawa mzuri mipira ya juu pengine hata ya chini, hii haizuii ila atuonyeshe ubora wake wa kumzidi mzawa.”
Simba imemsajili kipa huyo kutoka Resende FC ya Brazil na msimu uliopita ameichezea Itabirito FC-MG kwa mkopo na yupo kambini Uturuki.
Kwa usajili huo Simba inakuwa na makipa wanne Manula, Ally Salim, Ahmed Feruzi βTeruβ pamoja na Jefferson.