Home Habari za michezo GAMONDI ATAMBA KUHUSU UBINGWA WA MSIMU HUU YANGA

GAMONDI ATAMBA KUHUSU UBINGWA WA MSIMU HUU YANGA

Habari za Yanga

Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Angel Miguel Gamondi amesema ana matumaini makubwa na kikosi chake kuelekea msimu mpya 2023/24, ambao utaanza rasmi Agosti 15.

Kocha huyo aliyechukuwa nafasi ya Nabi aliyetimkia Far Rabat ya nchini Morocco, amemema hana shinikizo lolote kuelekea msimu ujao na anaimani atafanya vizuri akiwa na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michezo mingine ambayo kikosi chake kitashiriki.

Gamondi amesema katika muda mfupi ambao amekaa na kikosi hicho, ameona wachezaji wanaojituma na kujitambua kitu ambacho kinampa matumaini ya kufanya vizuri katika kila mashindano watakayoshiriki.

“Nimezoea kufanya kazi katika shinikizo hasa soka la Afrika, mashabiki wanahitaji matokeo muda wote, kwa hiyo ni lazima ukiwa kocha ujue kuishi katika nyakati zote, ukiwa umeshinda au umepoteza,” amesema Gamondi.

Kocha huyo amesema pia anaheshimu kila kilichofanywa na watangulizi wake na anatamani kufanya zaidi ya walipoishia, ndio maana ameanza mapema kukisuka kikosi hicho.

Naye Afisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema Yanga itaendelea kutetemesha Afrika kwa kusajili wachezaji wakubwa.

“Kwa sasa Young Africans imeshakuwa klabu kubwa Afrika na hata usajili tunaoufanya sasa ni wa wachezaji wakubwa, huyu (Zouazoua) ni MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, tumemsajili ili kuongeza nguvu katika kikosi chetu, kama nilivyokuwa nikisema siku zote sisi bado tuna kikosi bora ambacho hakijabadilika, tunachofanya ni kuongeza wachezaji wenye viwango vya juu na kuwafanya wachezaji waliopo wasibweteke,” amesema Kamwe.

Amesema lengo wa klabu hiyo ni kufika mbali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, pamoja na kutetea mataji ya hapa nchini wanayoyashikilia.

“Hatuna masihara hata kidogo, kama kuna watu walidhani baada ya kupata mafanikio misimu miwili tutabweteka, si kweli, msimu ujao tunataka tufike kwenye ngazi za juu katika Ligi ya Mabingwa Afrika kama tulivyofanya kwenye Kombe la Shirikisho,” Kamwe ametamba.

Afisa huyo amewasisitiza Wanachama na Mashabiki wa Young Africans kufurika katika Tamasha la Siku ya Mwananchi litakalofanyika kesho Jumamosi (Julai 22) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo watacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Kaizer Chief’s kutoka Afrika Kusini.

SOMA NA HII  YANGA YASEPA NA POINTI TATU MBELE YA RUVU SHOOTING