Home Habari za michezo JAMBO LA YANGA KUWEKA KAMBI DUBAI LABUMA….SASA KUWEKA KAMBI HAPA

JAMBO LA YANGA KUWEKA KAMBI DUBAI LABUMA….SASA KUWEKA KAMBI HAPA

Klabu ya Yanga imeamua kuendelea kukomaa kufanya maandalizi ya msimu ujao hapa hapa nchini badala ya kwenda nje ya nchi kama ilivyo kwa timu zingine.

Simba imetangaza kwenda kuweka kambi nchini Uturuki huku Azam na Singida Fountain Gate zikiwa zinaenda wanaenda Tunisia.

Sababu kubwa ya Yanga kutokwenda nje ni muda mchache wa maandalizi ya msimu ujao lakini pia ni ishu ya timu ya Taifa Tanzania ambayo inajiandaa kucheza Fainali za Mataifa Afrika kwa upande wa wachezaji wanaocheza mashindano ya ndani (CHAN) na ratiba yake itatangazwa muda wowote mwezi huu.

Katika mashindano hayo Yanga ina wachezaji watano wanaoitwa timu ya Taifa Tanzania ambao ni Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Salum Abubakari ‘Sure Boy’, Metacha Mnata na Mudathir Yahya.

Hivyo benchi la ufundi la Yanga linaloongozwa na Miguel Angel Gamondi limeona ni bora timu hiyo isalie hapa hapa nchini kujiandaa na msimu ujao ili kocha huyo apate wasaa mzuri wa kuangalia wachezaji wake.

Chanzo kutoka ndani ya Yanga kimesema kuwa uongozi wa timu hiyo umeshawishika kuibakisha timu Tanzania ili ipate maandalizi kwa wakatii.

“Mfano tunaingia kambini tarehe 10 mwezi huu halafu twende nje, hapo hapo itaitwa timu ya Taifa kwa ajili ya CHAN ambayo inaweza kuitwa tarehe 23 maana tunacheza tarehe 28;

“Kivyovyote kwetu tunajua wachezaji ambao wanakuwa wanaitwa sasa wale wakiondoka na wapo kama watano unaona kabisa timu itabaki na wachezaji wachache kwahiyo tumeona ni bora tubaki hapa,”kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilifunguka zaidi na kusema ;”Baada ya kuamua kubaki hapa sasa tupo kwenye majadiliano kuangalia wapi ni sehemu sahihi kati ya Arusha na pale Avic Town.

Inafahamika kwamba kocha Gamondi anatarajia kuingia nchini Julai 7 (Ijumaa) kwa ajili ya kuanza kazi na kambi ya timu hiyo ikianza Julai 10.

Yanga msimu uliopita pia haikwenda nje ya nchi na ilichukua ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la Azam na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Wadau wa soka nchini kwa nyakati tofauti wameunga mkono maamuzi ya Yanga kuamua kusalia hapa nchini kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.

Mchezaji wa zamani Simba na Yanga, Zamoyoni Mogela alisema upande wake anaona Yanga ipo sahihi kwani kama kutakuwa na ishu ya timu ya Taifa ni wazi wanaweza kubaki na wachezaji nusu kwenye kambi yao.

“Ukienda nje halafu ukabaki na wachezaji nusu haipendezi, benchi lao ni jipya hivyo kocha anahitaji kukaa na wachezaji wake kwa muda;

“Haijalishi kwamba wameondokewa na wachezaji wachache lakini benchi kukaa na wachezaji ni muhimu.”

Upande wa mshambuliaji wa zamani Yanga, Hery Morris alisema hana mashaka na maamuzi ya Yanga kwani hata hapa nyumbani kuna sehemu nyingi za kuweka kambi na kuandaa timu.

“Kikubwa labda kule nje ya nchi wanaokwenda wanaweza kupata mechi nyingi za kirafiki, upande wa Yanga na wao kama watabaki hapa inabidi watafute mechi mbili hadi tatu,”alisema Morris.

SOMA NA HII  KATIKA HEKAHEKA ZA KUIMARISHA VIKOSI, MUSONDA AFUNGUKA MAZITO YANGA