Home Habari za michezo KOCHA WA YANGA AWATAKA WENGINE WATATU HAWA HAPA

KOCHA WA YANGA AWATAKA WENGINE WATATU HAWA HAPA

Kocha Mpya wa Yanga

IMEELEZWA kuwa, Kocha Mkuu wa Yanga, Muargentina, Miguel Gamondi, ameomba kuendelea kuliboresha benchi la ufundi kwa kuleta makocha wengine watatu wapya.

Hiyo ikiwa ni saa chache tangu Yanga wamtangaze Mousa Ndao raia wa Senegal kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo, aliyekuja kuchukua nafasi ya Mrundi, Cedric Kaze, ambaye mkataba wake umemalizika.

Msenegali huyo tayari yupo nchini kwa ajili ya kuanza kazi pamoja na Gamondi aliyemrithi Mtunisia, Nasreddine Nabi ambaye naye mkataba wake ulimalizika.

Kwa mujibu wa mmoja wa mabosi wa Yanga, ujio wa Ndao ni pendekezo la Kocha Gamondi, aliyehitaji kufanya naye kazi.

Bosi huyo alisema, Gamondi amempendekeza kocha huyo kutokana na kuwahi kufanya naye kazi pamoja katika kikosi cha Wydad Casablanca ya nchini Morocco msimu wa 2020/2021.

Aliongeza kuwa, Gamondi ameahidi kuendelea kuliboresha benchi lake kwa kuleta kocha wa makipa, kocha wa viungo na mtathimini mechi ambao muda wowote nao watatambulishwa Yanga.

“Kutambulishwa kwa Ndao sio mwisho, kwani muda wowote Yanga watatambulisha makocha wengine wapya watakaonza kazi msimu ujao, kwani Gamondi ameutaka uongozi wamboreshee benchi lake la ufundi.

“Hivyo tayari majina amekabidhi kwa uongozi, kilichobaki ni kumalizana na makocha hao watatu kabla ya kuwatangaza kama ilivyokuwa na Ndao ambaye aliwahi kuwa kocha msaidizi katika kikosi cha Wydad Casablanca wakati Gamondi akiwa kocha mkuu,” alisema bosi huyo.

Wakati huohuo, uongozi wa Yanga umebainisha kwamba, Julai 22, mwaka huu, ndiyo litafanyika tamasha lao la Wiki ya Mwananchi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar ambapo siku hiyo watatambulisha kikosi kizima cha timu hiyo kwa msimu wa 2023/24.

SOMA NA HII  YANGA WATAMBA KUIPAPATUA VILIVYO COASTAL UNION LEO...MASHABIKI WAPANGA KWENDA NA ROYAL TOUR..