Home Habari za michezo KWELI MAISHA YANAENDA KASI SANA MKUDE AINGIA KATIKA ORODHA HII

KWELI MAISHA YANAENDA KASI SANA MKUDE AINGIA KATIKA ORODHA HII

Mkude atambulishwa yanga

MAISHA yanaenda kasi sana. Ebu fikiria kabla ya Juni 9 Ligi Kuu Bara ya msimu uliopita kufikia tamati, Jonas Mkude alikuwa staa wa Simba. Ndiye aliyekuwa mchezaji mwandamizi katika kikosi hicho akikichezea tangu mwaka 2011.

Mkude alikuwa kati ya wachezaji wa awali kupewa ‘Thank You’ na Simba kuhitimisha miaka 13 ndani ya klabu hiyo. Mashabiki na wapenzi wa Msimbazi hawakuamini. Lakini ndivyo imeshakuwa na wengi walitarajia Agosti 6 katika Tamasha la Simba Day angeagwa rasmi.
Hata hivyo mambo ni tofauti. Kwa sasa ikiwa ni mwezi na wiki moja tu tangu Ligi Kuu ilipoisha, Mkude ni mali ya Yanga. Ndio, Nungu Nungu ni mchezaji mpya wa Yanga akipewa mkataba wa mwaka mmoja.

Usajili wa kutua Jangwani haukuaminika na wengi. Asilimia kubwa walichukulia kwa namna alivyoitumikia Simba kwa muda mrefu, isingekuwa rahisi kuhama mtaa na kutua Jangwani.
Lakini imeshakuwa Mkude atakiwasha nchini akiwa na uzi wa rangi ya kijani na njano tofauti na ule aliouzoea tangu akiitumikia timu ya U20 ya Simba inayotumia rangi nyekundu na nyeupe.
Kama hujui sasa ni kwamba kiungo huyo mkabaji anakuwa mchezaji wa 14 kwa miaka ya hivi karibuni kuhama mtaa kutoka Msimbazi kwenda Jangwani na wale wa kutoka Yanga kutua Simba.

Blogu letu linakuletea mastaa hao waliokipiga kotekote, huku Mkude akiingia kwenye orodha hiyo safari hii ambako anakutana na wachezaji aliokuwa akionyeshana nao kazi alipokuwa Msimbazi, yaani Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Yannick Bangala waliopo Yanga tangu msimu uliopita.

MRISHO NGASSA
Alijiunga na Yanga mwaka 2006 akitokea Kagera Sugar na kuichezea hadi mwaka 2010 alipoondoa na kujiunga na Azam FC.
Alicheza Azam kwa misimu miwili na katika msimu wa kwanza tu wa 2010-2011 alinyakua tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara kwa kukwamisha jumla ya mabao 18, kisha ndipo akajiunga na Simba kwa mkopo 2012 katika sakata lililopata umaarufu kipindi hicho kutokana na kuibusu nembo na jezi ya Yanga akiwa Matajiri wa Chamazi walioamua kumpeleka Simba ili kukatili ndoto zake za kurudi tena Jangwani kuliamsha.
Wakati anaondoka Azam, mwamba huyo alitwaa tuzo ya Mfungaji Bora msimu wa 2013

Simba alikaa mwaka mmoja tu akarudi zake Yanga hadi 2015 alipoondoka kwenda kujiunga na Free Star State ya Afrika Kusini kisha Fanja FC ya Oman, Mbeya City na Ndanda baadae akarudi tena Yanga sasa yupo mitaani akikuza vipaji vya vijana.

IBRAHIM AJIBU
Ni zao la Simba alijiunga kwenye akademi ya timu hiyo mwaka 2009 kabla ya kupandishwa kwenye timu ya wakubwa mwaka 2013. Hakuna na maisha mazuri sana ndani ya Simba hadi alipoamua kutafuta changamoto nyingine nje ya timu hiyo.
Agosti 2017 alijiunga na Yanga chini ya kocha Mwinyi Zahera ambaye alijenga Imani kubwa kwa mchezaji huyo na kufanikiwa kumpa kitambaa cha unahodha akiwa ndani ya timu hiyo Licha ya kutokuambulia taji lolote aliteka hisia za mashabiki wa timu hiyo kutokana na kuwango chake.
Ajibu aliibuka mkali wa kupiga pasi za mwisho kwenye Ligi Kuu akiwa amefanya hivyo mara 16 huku pia akifunga mabao sita na mchango wake uliifanya hadi Yanga kumpa kitambaa cha unahodha.

BERNARD MORRISON
Licha ya uwezo wake mkubwa uwanjani ameshindwa kutumia vyema nafasi ya pili aliyopewa na Yanga baada ya kutimka ndani ya timu hiyo akijiunga na watani zao Simba.
Morrison alianza kuitukia Yanga msimu wake wa kwanza alijiunga 2020 akitokea Motema Pombe aliitumikia kwa msimu mmoja na baadae akatimkia Simba kwa mkataba wa miwili na baadae kurudi tena Yanga hadi msimu uliomalizika ambapo amemaliza mkataba katika misimu yote aliyocheza Tanzania kafanikiwa kuvuna mkwanja mrefu lakini hakuwa na mafanikio makubwa kutokana na kutokucheza mara kwa mara.

HARUNA MOSHI ‘BOBAN’
Boban alijiunga na Simba mwaka 2004 akitokea Moro United na alichezea timu hiyo hadi 2009 alipotimka na kujiunga na klabu ya Gefle IF ya Sweden ambayo hakudumu nayo sana kwani, alikaa msimu mmoja tu na kurejea Tanzania kisha kujiunga tena na Simba mwaka 2011.
Kiungo huyo fundi uwanjani alicheza ndani ya kikosi hicho kwa msimu miwili mpaka 2013 alipoamua kuondoka na kurejea katika timu yake ya zamani ya Friends Rangers, kisha Coastal Union na Mbeya City.
2019 alijiunga na Yanga dirisha dogo la usajili na kufanikiwa kuichezea msimu mmoja tu ambao haukuwa na mafanikio kwake kutokana na timu hiyo kukosa taji.

KELVIN YONDANI
Beki huyo kitasa ambaye kwa sasa anakipiga Geita Gold alianza kucheza Simba kabla ajatua Yanga aliyoichezea kwa mafanikio makubwa na muda mrefu.
Yondani alijiunga na Simba mwaka 2008 na kucheza hadi 2012 akiwa na timu hiyo alitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Tanzania Bara na baadae akatimkia Yanga.
Yondani ndani ya Yanga alifanikiwa kutengeneza safu bora ya ulinzi kwa kipindi chote na kuifanya klabu kushinda medali zaidi ya 6 katika mashindano mbali mbali , Ligi Kuu bara,klabu bingwa Afrika Mashariki na kati, kombe la ngao ya hisaini na kuiwezesha Yanga kucheza hatua ya makundi chini ya kocha Hans Van Pluijm.

HARUNA NIYONZIMA
Alianza kuwatumikia wanajangwani baada ya kutua nchini mwaka 2011 ameichezea timu hiyo kwa mafanikio makubwa kabla ya kufanya uamuzi wa kusaka changamoto nyingine nje ya Yanga.
Agosti 2017 alijiunga na Simba timu ambayo hakuonyesha uwezo mkubwa kama alivyofanya akiwa Yanga na baada ya misimu miwili ya kumtumikia Mnyanga, kiungo mshambuliaji huyo alirejesha majeshi Jangwani na kucheza kabla ya kuagwa rasmi misimu mitatu iliyopita na kwenda kwao Rwanda kukipiga AS Kigali na kwa sasa yupo Arabuni, huku akiwa na cheti chake cha ukocha kabatini akisubiri kuanza kufundisha.

AMISSI TAMBWE
Tambwe alitua nchini na kusajiliwa na Simba mwaka 2013 akitokea Vital’O ya Burundi na kuitumikia timu hiyo kwa miezi 18 baada ya kutimuliwa katika dirisha dogo la 2014-2015.
Ndani ya miezi yake 18 kwenye klabu ya Simba, Tambwe aliweza kufunga mabao 20 katika mechi za Ligi Kuu. Straika huyo alifunga mabao 19 msimu wa 2013/14 na kuibuka mfungaji bora kabla ya msimu uliofuata kufunga bao moja pekee katika mechi saba za mwanzo wa msimu jambo lililosababisha kuachwa na Simba ambayo kwa wakati huo ilimsajili Danny Sserunkuma kutoka Gor Mahia ya Kenya.
Pia akiwa Simba, Tambwe hakufanikiwa kushinda taji lolote la Ligi Kuu, licha ya kumaliza kama mfungaji bora katika msimu wa 2013/14.
Katika nusu msimu tangu atue Yanga, Tambwe alifunga mabao 13 na kumfanya amalize Ligi akiwa na mabao 14, likiwamo moja la Simba na kushika nafasi ya pili ya Wafungaji Bora nyuma ya Simon Msuva aliyetwaa kiatu.
Msimu uliofuata alifunga 21 na kutwaa kiatu cha ufungaji akiipa Yanga taji na hadi anaondoka mara baada ya msimu wa 2018-2019, mwamba huyo alikuwa ameifungia Yanga jumla ya mabao 54 katika Ligi Kuu Bara akibeba nao ubingwa wa ligi mara tatu, Ngao ya Jamii mbili na taji la ASFC moja.

DEO MUNISHI ‘DIDA’
Kipa huyu naye ameingia katika rekodi ya kucheza mchezo huo akiwa katika klabu hizo mbili tofauti.
Dida alijiunga na Simba mwaka 2009 na kuichezea timu hiyo hadi mwaka 2011 alipoondoka na kujiunga na Azam.
Alidumu Azam kwa misimu miwili na baadae kujiunga na Yanga ambapo aliidakia timu hiyo mpaka mwaka 2017.
Mechi ya mwisho ya watani wa Jadi ilikuwa Februari 26, 2017 aliposhindwa kuizuia Yanga kulala kwa mabao 2-1 dhidi ya Simba.

JUMA KASEJA
Amedaka Simba na Yanga awamu mbili alisajiliwa na Simba mwaka 2003 akitokea Moro United. Alikaa Simba mpaka 2008 alipojiunga Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja. Licha ya Yanga kutaka kumuongezea mkataba baada ya ule wa awali kumalizika, Kaseja alirudi Simba iliyomsajili kwa mkataba wa miaka minne. Baada ya kumaliza mkataba wake na Simba, Kaseja alisajiliwa tena na Yanga mwaka 2013 kwa dau la Sh40milioni lakini maisha yake Jangwani hayakuwa mazuri hadi timu hiyo ilipoamua kuachana naye mapema mwaka huu.
Robo fainali Afrika
Hakuna kipa wala timu ya Tanzania iliyofuzu wala kucheza michuano yoyote ya klabu za Afrika tangu mwaka 2003. Kaseja ndiye wa mwisho kucheza mwaka 2003 akiwa na Simba ambayo ilitinga hatua ya robo ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuiondosha Zamalek ya Misri waliokuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo kwa mikwaju ya penalti.
Kwa kuingia hatua hiyo, Kaseja aliandika rekodi ya kuwa kipa mdogo zaidi kutoka hapa nchini kucheza hatua hiyo. Kipindi hiko alikua na umri wa miaka 18 kwa mujibu wa makadabrasha yake ya usajili yaliyoko Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mataji saba na Simba, Yanga
Unaweza kusema ni kipa pekee wa kizazi cha sasa ambaye amefanikiwa kuipa mafanikio makubwa klabu ya Simba pengine kuliko kipa yeyote yule. Mbali na Simba, Kaseja pia aliipa Yanga mafanikio baada ya kutwaa taji la ligi na timu hiyo mwaka 2008/09.
Hadi anaachwa Simba, Kaseja ameiwezesha timu hiyo kutwaa mataji saba, matano ya Ligi Kuu Tanzania Bara katika misimu ya 2003, 2004, 2007 (Ligi Ndogo), 2010 na 2012 na mawili ya Tusker, mwaka 2003 na 2005 kwa mashindano yaliyofanyika Tanzania kisha Kenya.

GADIEL MICHAEL
Alianza kuwatumikia Azam FC msimu wa 2014-17 ubora aliouonyesha ndani ya timu hiyo uliwavuta Yanga ambao walimwaga noti ili kunasa saini yake na kufanikiwa wakimsajili msimu wa 2017-2019.
Akiwa Yanga akifanya vizuri na kuwa dhanushi Simba ambao walimsajili kwa mkataba wa miaka miwili lakini hakuweza kuendeleza ubora wake kutokana na kukutana na ubora wa beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye amemuweka benchi kwa misimu minne.

HASSAN RAMADHAN ‘KESSY’
Usajili wake ulikuwa wa mgogoro mkubwa kati ya wahasimu hao wa jadi Simba na Yanga baada ya wanajangwani kumvalisha jezi mchezaji huyo akiwa bado anamkataba na Simba hadi kufikia hatua ya kulipishana faini.
Kessy ambaye ni zao la Mtibwa Sugar ambayo aliitumikia kuanzia 2011-2014 alianza kuichezea Simba kwa misimu misimu miwili 2014-2016 na kutua Yanga Msimu wa 2016-2018 baadae alitimkia Nkane ya Zambia

ALLY MUSTAFA ‘BARTHEZ’
Amedumu Yanga zaidi ya mika 7 tangu atoke Simba na kuamua kujiunga na Wanajangwani, mlinda mlango huyo ameiwezesha klabu kushinda mataji mbali mbali ya ndani na nje ya nchi kwa kipindi chote alichodumu Yanga.
Kopi huyo sasa amestaafu soka na kuamua kusomea ukocha wa kuwanoa magolikipa ameandika rekodi ya kumfundisha mshindani wake Dida akiwa Mbeya City sasa hana timu baada ya kukalia kuti kavu City kabla haijashuka daraja.

EMMANUEL OKWI
Alianza kuitumikia Simba kabla ya Kihamia Yanga alijiunga na Wekundu wa Msimbazi mwaka 2010 alipoichezea hadi 2013.
Mwaka 2013 akarejea nchini na kujiunga na Yanga alikocheza msimu mmoja hadi 2014,
Mwaka 2015 Okwi akarejea Simba na na ndani ya mwaka huo huo akajiunga na Senderjyske ya Sweden aliyocheza hadi 2017 ambapo alirejea Uganda na kujiunga na SC villa kisha mwaka huo huo akasajiliwa na Simba.

BENO KAKOLANYA
Alianza kuitumikia Yanga kabla hajatua Simba ambapo usajili wake ulifanikiwa baada ya kushinda kesi ya kuvunja mkataba kutokana na waajiri wale kushindwa kumlipa mishahara.
Kwa misimu miwili aliyokaa Yanga, Kakolanya alidaka mechi 24 tu, kabla ya kujiondoa mwenyewe akiituhumu klabu kukiuka vipengele vya mkataba ambao mwishowe ulivunjwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Na baadae kujiunga na Simba ambayo ameitumikia kwa misimu minne akitwaa mataji matatu ya ligi kuu bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) huku akiwa miongoni mwa wachezaji waliofika hatua ya robo fainali mara tatu.

SOMA NA HII  KWA KANUNI HII YA CAF YANGA ILIKUWA LAZIMA WAFUZU JUZI....