Home Habari za michezo MGANDA ALIYESAINI YANGA AKUTANA NA MTIHANI MZITO

MGANDA ALIYESAINI YANGA AKUTANA NA MTIHANI MZITO

Habari za Yanga leo

UJIO wa beki mpya wa Yanga, Gift Fred aliyesaini mkataba wa miaka mitatu Jangwani ni wazi utakuwa mtego mpya kwa mabeki wa kati kwenye kikosi hicho.

Lakini wakati likiwaweka mtegoni mabeki wa sasa wa Yanga, Gift atatakiwa kufanya kazi ya ziada kupata nafasi mbele ya nyota walio katika kiwango bora, nahodha Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Bacca.

Hilo liko wazi kwani licha ya kwamba Yanga ipo imara kwenye safu ya ulinzi ikiwa ni timu ya pili kuruhusu mabao machache (18) katika Ligi Kuu msimu uliopita, Simba iliruhusu (17) katika msimu uliopita.

Gift anasajiliwa Yanga akiwa nahodha wa zamani SC Villa (Uganda), ambayo alicheza msimu uliopita, lakini pia alikuwa kwenye kikosi cha Uganda ‘Cranes’ kilichocheza mechi ya kufuzu Mataifa Afrika (AFCON) kwenye mchezo dhidi ya Algeria, mwezi uliopita, nchini Cameroon.

Wakati Gift akiingia kwenye kikosi hicho, Yanga ina ukuta wa mabeki imara kama Job, Mwamnyeto, Bacca, Yannick Bangala (anamudu kucheza kiungo), wakati Mamadou Doumbia akiwa mlangoni kuondoka.

Kati ya wachezaji ambao wamejihakikishia namba ya kuanza eneo la ulinzi ni Job (muda mwingine hucheza beki wa kulia), Mwamnyeto na Bacca, huku Bangala akitumika eneo la kiungo.

Hadi sasa, hakuna ambaye tayari ana uhakika wa namba, kwani Yanga ina kocha mpya, Miguel Gamondi na anaanza nao kwenye maandalizi ya msimu mpya, hivyo ataangalia ni yupi ambaye atakuwa bora kuanza.

Gift ni beki ambaye ni mtulivu, lakini anatumia nguvu kwenye kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani, huku akiwa na sifa ua jasiri muda wote.

Wadau wa soka nchini kwa nyakati tofauti wametoa maoni yao juu ya mchezaji huyo, wakisema anaweza kuchukua nafasi ya mtu kama ataonyesha uwezo mazoezini kwa sababu timu ina benchi jipya la ufundi.

Mshambuliaji wa zamani Yanga, Hery Morris alisema Gift anaweza kupata nafasi kama tu ataamua kujituma na kumuonyesha kocha kwamba anahitaji kuanza.

“Siwezi kusema atachukua namba ya nani, ujue kocha ni mpya na akikutana na wachezaji anaweza kubadili kikosi, lakini kubwa ni wafanye vizuri wanaopewa nafasi.

“Mashabiki hata kama kukiwa na mabadiliko lakini timu ikawa inapata matokeo basi ni ngumu kuhoji kwanini fulani hachezi,” alisema Morris.

Nyota wa zamani Simba na Yanga, Zamoyoni Mogela alisema imani yake inamwambia kuwa usajili wa Gift unakwenda kuongeza kitu kwenye kikosi cha Yanga.

Mogela alisema Yanga ilikuwa imara kwenye idara zote msimu uliopita, lakini hadi kufika hatua ya beki huyo kusajiliwa maana yake kuna kitu kimewasukuma.

“Suala la kucheza ni uamuzi wa kocha ambaye ni mpya, ataangalia wachezaji mazoezini na ataangalia yupi anaweza kumtumia na baada ya hapo atampa nafasi aliyefanya vizuri. Hilo lipo wazi,” alisema Mogela.

Kipa wa zamani wa Yanga, Benjamin Haule alisema usajili ni kama bahati, mchezaji anaweza kufika na kufiti au isiwe hivyo, lakini mazoezini ndiyo kila kitu. Kocha atakuwa na machaguo sahihi kutokana na atakachokiona.

“Bahati nzuri Gift amekuja wakati kocha ni mpya, wote wengine atakuwa amewaona kwenye video za mechi zilizopita, kama atajituma atakuwa na nafasi ya mtu,” alisema kipa huyo.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Gift, mabingwa hao wa soka nchini wamemshusha winga, Max Mpia kutoka DR COngo, ambaye anakuja kuziba nafasi iliyoachwa na mwenzake, Tuisila Kisinda.

Max alionekana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, jana, akiwa anatoka nchini kwao alikokuwa akiitumikia Maniema ya DR Congo.

SOMA NA HII  SARPONG APEWA 'LAST CHANCE' YANGA