Home Habari za michezo WACHEZAJI HAWA WALIOACHWA NA SIMBA, YANGA WAPATA MAJANGA KATIKA USAJILI

WACHEZAJI HAWA WALIOACHWA NA SIMBA, YANGA WAPATA MAJANGA KATIKA USAJILI

Habari za Yanga

KUNA wachezaji waliochwa Simba na Yanga kutokana na kile walichopanda msimu uliopita, lakini mavuno yao yanaweza kuwa kiduchu au kuvunja benki kulingana na thamani zao.

Mfano mzuri ni straika Fiston Mayele ambaye Yanga imekuwa ikipambana kumbakiza baada ya kujitokeza klabu za nje zinazomtaka, kiwango chake ndicho kilicholeta ushindani sokoni kwani ndani ya misimu miwili kwenye Ligi Kuu Bara amefunga mabao 33 nje na pia katika mashindano mengine.

Wakati huohuo wapo wale ambao hawakufanya vizuri msimu uliopita, biashara zinakuwa ngumu sokoni ingawa baadhi wameshapata timu za kuzitumikia msimu ujao, lakini timu zilizowapata hazikuwagombea na usajili wao haukuwa wa kushitua.

Mwanaspoti limekukusanyia wachezaji ambao sokoni bei zao hazitishi kulingana na thamani zao kushuka na kama watapata timu watakuwa na kazi ya kufanya kupandisha thamani misimu ijayo kulingana na mikataba watakayoingia na waajiri wapya:

GADIEL MICHAEL
Tangu beki wa pembeni Gadiel Michael alijiunga na Simba msimu wa 2019-2023 hakuwahi kutamba mbele ya mshindani wake wa namba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, kiwango chake kilishuka na kusahaulika kwenye anga za ushindani, jambo litakalofanya biashara yake iwe ngumu sokoni.

ABDALLAH SHAIBU ‘NINJA’
Beki wa kati, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ sokoni bei yake itakuwa ya kawaida, kutokana na msimu ulioisha hakuwa na namba Yanga, alijaribu kutoka kwa mkopo kwenda Dodoma Jiji angalau alipata mechi za kucheza, aliporejea aliendelea kukaa benchi.

BERNARD MORRISON
Hakuwa asiyefahamu kipaji cha winga, Bernard Morrison aliyefanikiwa kuzichezea Simba na Yanga ambayo imempa thank you, kutokana na msimu ulioisha kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosi cha kwanza chini ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi, bei yake sokoni haitasumbua.
Ikumbukwe Morrison wakati anajiunga Simba 2020-2022 mashabiki wa Yanga waliumizwa na uhamisho wake, kwani alikuwa ni mchezaji wa kiwango cha juu, pia wakati anahama Msimbazi anarejea Jangwani bado wafuasi wake waliumia kuikosa huduma yake, tofauti na sasa wanaona kawaida tu.

DAVID BRYSON
Ilikuwa ngumu kwa beki wa pembeni, David Bryson kupata nafasi mbele ya Joyce Lomalisa na Shomari Kibwana ambao walikuwa kwenye kiwango cha juu, licha ya kutajwa kasaini Singida Fountain Gate, lakini bei ya sokoni isingezitesa timu kuvunja benk kumsajili.

DICKSON AMBUNDO
Winga aliyeachwa na Yanga na inaelezwa kasaini Singida Fountain Gate, pamoja na hilo hakuwa mchezaji tishio wa kuzifanya timu zishindane kutoa pesa ndefu kupata saini yake.
Wengineo ni Erick Johora(Yanga), Victor Akpan, Nelson Okwa, Augustine Okra, Mohammed Ouattara (Simba).

MSIKIE MALIMA
Staa wa zamani wa Yanga, Bakari Malima anasema wachezaji walioachwa na klabu kongwe, wakipata timu nyingine wana nafasi ya kupambana na huenda wakarejea kuzitumikia tena.
“Yanga na Simba zinashiriki michuano ya CAF lazima ziwe na wachezaji ambao wana utayari wa kuzisaidia, naamini kama watasajiliwa timu nyingine ni juu yao kupambana, viwango vyao vikiwa juu na bei zao sokoni zitapanda na wanaweza wakarejea tena kwenye klabu hizo,” anasema.

SOMA NA HII  YANGA WAIPIGA KIJEMBE SIMBA KISA VIKAO VYA USIKU.... KAMWE AFUNGUKA HAYA