Home Azam FC HIVI NDIVYO THANK YOU ZA SIMBA, YANGA ZILIVYOGEUKA NA KUWA WELCOME

HIVI NDIVYO THANK YOU ZA SIMBA, YANGA ZILIVYOGEUKA NA KUWA WELCOME

yanick bangala

Wakati tetesi za usajili zikiendelea kushika kasi nchini muda huo huo thank you nazo zikiendelea kutolewa kwa baadhi ya wachezaji na benchi la ufundi.

Hadi sasa Simba imewapa mkono wa kwaheri wachezaji 12 na ndio inaongoza kwa ‘Thank you’kwenye msimamo wa Ligi ya mitandaoni ikufumua kikosi kwaajili ya msimu ujao na kusajili wachezaji watano.

Azam nao walianza kufumua kikosi na benchi la ufundi mapema sana kabla ya timu yoyote Ligi Kuu Bara ambapo ilianza na kocha wa magoli kipa Daniel Cadena na kufikisha idadi ya watu 10 huku Coastal Union na Namungo ikiwapa mkono wa kwaheri wachezaji saba ambapo kwa Yanga tayari imepitisha panga kwa watu sita.

Thank you zinazotolewa na vilabu mbalimbali nchini zimegeuka welcome kwa baadhi ya timu na Mwanaspoti linakuletea thank you zilizogeuka welcome kwa timu nyingine.

MKUDE – YANGA

Baada ya kusota benchi ndani ya miaka miwili na mkataba wake kumalizika msimu uliopita, Kiungo wa Simba, Jonas Mkude alipewa mkono wa kwaheri kuendelea kuitumikia klabu hiyo.

Mkude ambaye aliichezea Simba kwa miaka 13 mfululizo alikula ‘Thank You’ wiki zilizopita na sababu kubwa ikielezwa kwamba ni kiwango kushuka.

Baada ya kupewa Thank You ndani ya viunga vya Msimbazi majirani zao Yanga wakampa Welcome kwa kumkabidhi mkataba wa mwaka mmoja kuwatumikia jangwani.

Yanga huenda wakapumua kama kiungo huyo ataweza kuwa kwenye ubora wake kwani Bangala tayari walishaanza kumtafutia mbadala kutokana na kiwango chake pamoja na mengine ya nje ya uwanja.

Hivyo wakati Simba wanajadili kuachana na Mkude kutokana na masuala ya kinidhamu Yanga kwao ilikua furaha kumkaribisha fundi huyo wa kabumbu.

ERICK JOHORA – GEITA GOLD

Thank you kutoka kwa kipa namba tatu wa Yanga, Erick Johora huenda ikawapa manufaa Geita Gold ambao tetesi zinasema kama mambo yakienda sawa atapewa mkataba.

Tangu Johora alipojiunga na Yanga 2021 hakuwa na nafasi, zaidi ya kucheza Kombe la Mapinduzi msimu uliopita, tofauti na makipa waliokuja nyuma yake kama Aboutwalib Mshery na Metacha Mnata ambao angalau wanapata nafasi mbele ya namba moja Djigui Diarra.

Johora aliitumikia Yanga kwa misimu miwili na kufanikiwa kuvaa medali ya CAF, Kombe la Shirikisho la Azam na Ligi Kuu Bara lakini hakuwa akipata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mbele ya Diarra, Mshery na Metacha ambao wamekuwa wakitumika kwa nyakati tofauti.

Kutofanya vizuri kutemwa na Mabibgwa hao lakini huenda ujio wake na ukawapa faida Geita ambao wanampa welcome.

ERASTO NYONI – NAMUNGO

Nyoni ni mmoja wa wachezaji waliopewa ‘Thank You’ na Simba wiki ziliyopita baada ya kuitumikia kwa misimu mitano tangu aliposajiliwa akitokea Azam FC.

Baada ya kutemwa na wekundu wa msimbazi saa chache Namungo kupitia peji yake ilimtangaza kama usajili wa kwanza kwao kwa ajili ya msimu ujao.

Lakini thank you ya Nyoni iligeuka welcome kwa Namungo kwani baada ya kumtambulisha tu alipokelewa kama mfalme na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wakitaja sifa zake mbalimbali ikiwemo nidhamu yake.

Alisajiliwa na Simba msimu wa 2017-2018 akitokea Azam akiwa sambamba na Aishi Manula, John Bocco na Shomary Kapombe na misimu minne kati ya mitano aliisaidia timu hiyo kubeba taji manne la Ligi Kuu Bara, mataji mawili ASFC na kuifanya Simba itishe.

JOASH ONYANGO – SINGIDA FG

Beki wa kati wa Simba, Joash Onyango ni kati ya wachezaji waliokuwa wakiomba kuondoka Msimbazi tangu dirisha dogo la msimu uliopita kabla ya kuongezwa mkataba wa mwaka mmoja.

Ilidai kuwa sababu ya Onyango kuandika barua ya kuondoka Msimbazi ni kutokuwa na furaha ndani ya kikosi hicho na pia kutotimiziwa baadhi ya matakwa yake.

Mkenya huyo baada ya kupewa thank you na Simba ilimleta Che Fondoh Malone ili kuja kuziba nafasi yake aungane na Kennedy Juma na Henock Inonga.

Hata hivyo inadaiwa Singida hawakucheza mbali kumvizia beki huyo na baada ya kupewa thank you huenda muda si mrefu akatambulishwa na walima alizeti.

BENO KAKOLANYA – SINGIDA FG

Kipa Beno Kakolanya amedumu katika kikosi cha Simba kwa misimu minne mfululizo baada ya kuwa mchezaji huru akitokea klabu ya Yanga 2019.

Kipa huyo inadaiwa ameshamalizana na mabosi wa Singida Fountain Gate kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kupewa thank you na Simba.

Kakolanya aliyewahi kuzichezea Tanzania Prisons na Yanga kama dili lake na Singida litatiki basi atakutana na mabeki Pascal Wawa na Onyango ambao alicheza nao wakati yupo Simba.

DICKSON AMBUNDO – DODOMA JIJI

Winga wa Yanga, Dickson Ambundo imeelezwa anaweza akarejea tena Dodoma Jiji kutokana na kukosa namba ndani ya kikosi hicho ambapo Jesus Moloko anaonekana kuwa kwenye kiwango cha juu.

Thank you ya Ambundo huenda ikawanufaisha Dodoma Jiji kwa kuwa tayari winga huyo anauzeofu na Ligi na mashindano mbalimbali yakiwemo ya Kombe la Azam.

Winga huyo ni miongoni mwa wachezaji wenye uwezo wa kucheza pande zote mbili kushoto na kulia uwanjani na kufanya umuhimu wao uonekane.

DAVID BRYSON – JKT TANZANIA

Beki wa kushoto, David Bryson ni miongoni mwa wachezaji waliopewa mkono wa kwaheri ndani ya kikosi hicho baada ya kushindwa kuonesha kiwango kizuri.

Nyota huyo alijiunga na Yanga Agosti 2021 akitokea KMC ambako alionyesha kiwango kizuri na kuzivutia timu nyingi ingawa tangu amejiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara mambo yalikuwa ni magumu.

Tangu ajiunge na Yanga alikosa nafasi ndani ya kikosi cha kwanza, uwepo wa Joyce Lomalisa na Kibwana Shomari ambao viwango vyao vipo juu na ndio wanaobadilishana kucheza, hivyo kuliwafanya viongozi wa timu hiyo kumpa thank you ambayo kwa JKT Tanzania huenda wakampa welcome.

YANNICK BANGALA – AZAM FC

Misimu miwili iliyopita alikuwa Mchezaji Bora wa msimu, lakini msimu uliopita haukuwa mzuri kwa kiungo huyo anayemudu kucheza pia kama beki wa kati na kusababishwa kutotambulishwa kwenye kikosi kipya cha Yanga siku ya kilele cha Wiki ya Mwananchi.

Wengi waliamini alikuwa akienda Singia Fountain Gate kwani ilikuwa ikimpigia hesabu hata kwa mkopo, lakini ghafla akaibukia Azam FC iliyomnunua wakati Yanga ikimpa ‘Thank You’ kushukuru kazi chafu aliyoifanya Jangwani.

Uwezo mkubwa alionayo katika kudhibiti washambuliaji na kuwatibulia viungo wenzake eneo la katikati ya uwanja imemrahisishia kazi kupewa Welcome viunga cha Chamazi anapokuwa sasa anapasha na wenzake kwenye Uwanja wa Azam Complex.

BERNARD MORRISON – SINGIDA FG

Huyu alikuwa mchezaji wa mwanzoni kabisa wa Yanga kupewa Thank You, kisha akasepa zake kwenda kwao Ghana kabla ya hivi karibuni kurejea na inaelezwa tayari amepewa ‘Welcome’ ndani ya Singida Fountain Gate ikihitaji huduma yake kwenye Ligi Kuu msimu ujao.

Morrison anatarajiwa kutambulishwa kesho kwenye Tamasha la klabu hiyo litakalohitimishwa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya AS Vita, moja ya klabu alizowahi kuzichezea katika maisha yake ya soka.

Kabla ya kuachwa Yanga, Morrison aliichezea pia Simba kwa misimu miwili, iliyomnyakua kutoka Jangwani, klabu iliyomleta nchini mwaka 2020 na kutua kwake Singida inaweza kuwa neema zaidi.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA CAF KESHO....MASTAA WAKUBWA YANGA KUKOSEKANA...NABI AANZA KULIA NA RATIBA KUBANA...