Home Habari za michezo KAULI YA MPIRA PESA YAZUA KIZAZAA SIMBA, YANGA, ISHU IKO HIVI

KAULI YA MPIRA PESA YAZUA KIZAZAA SIMBA, YANGA, ISHU IKO HIVI

KAULI ya Mpira ni Pesa ndio unaweza kuitumia kuelezea namna Simba na Yanga zinavyoonyesha dalili ya kutamba tena msimu ujao wa 2023/2024 kutokana na jeuri ya fedha ambayo zimevuna katika miezi ya hivi karibuni na hivyo kuzifanya ziwe na uhakika wa kumudu bila tabu gharama zote za mashindano ambayo kila moja itashiriki msimu ujao.

Kwa pamoja, timu hizo zitashiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi lakini kwa Simba wao watakuwa na shindano lingine watakalocheza msimu ujao ambalo ni lile African Super League.

Changamoto kubwa huwa ni mechi za kimataifa hasa zile za ugenini ambazo huzigharimu kiasi kikubwa cha fedha timu hizo katika kugharamia huduma za malazi, usafiri na posho kwa wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi lakini kwa fedha ambazo timu hizo mbili zimekusanya na zinaendelea kukusanya, hapana shaka mipango itaziendea vizuri katika shughuli za utawala na usimamizi na hivyo jukumu kubakia kwa wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi kufanya vizuri ndani ya uwanja ili kuzipa mafanikio.

MZIGO WA CAF

Fedha hizo kutoka Caf zimegawanyika katika makundi mawili ambayo kundi la kwanza ni zile za zawadi kutokana na nafasi ambazo timu hizo kila moja ilifikia kwenye mashindano ya klabu Afrika msimu uliomalizika na kundi la pili ni zile za maandalizi kwa mashindano ya African Super League yatakayoanza Oktoba.

Yanga imepata Dola 1 milioni (Sh 2.4 bilioni) kutoka Caf ambacho ni sawa na 11.82% ya bajeti ya Yanga msimu ujao ambayo itakuwa ni Sh 20.3 bilioni.

Simba yenyewe ilifikia hatua ya robo fainali na kupata mgawo wa Dola 900,000 (Sh 2.1 bilioni) kutoka Caf ambao ni sawa na 9.13% ya bajeti yote ya Simba msimu wa 2023/2024 ambayo ni Sh 23 bilioni.

Kwa kushiriki mashindano ya African Super League msimu ujao, Simba pia imeuna kiasi cha Sh 5 bilioni za maandalizi kutoka Caf ambazo ni sawa na 21.74% ya bajeti yake katika msimu huo.

Kiujumla, kutoka Caf, Simba imepata kiasi cha Sh 7.1 bilioni ambacho ni sawa na 30.87% ya bajeti yake ya msimu ujao.

MAYELE, SAKHO

Inaripotiwa kuwa Mayele ameuzwa Dola 1 milioni (Sh 2.4 bilioni) kwa Pyramids Fc ya Misri, fedha ambazo ni sawa na asilimia 11.82 ya bajeti ya Yanga katika msimu wa 2023/2024.

Simba nayo imelazimika kumuuza winga wake Pape Osmane Sakho kwenda timu ya Quevilly Rouen Metropole inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza huko Ufaransa.

Kiasi cha zaidi ya Dola 850,000 (Sh 2 bilioni) ambacho ni sawa na asilimia 8.7 ya bajeti yote ya Simba msimu ujao kimeingia Msimbazi.

MATAMASHA YAO

Wiki ya Wananchi kwa upande wa Yanga na lile kongwe la Simba Day kwa upande wa Simba yamekuwa miongoni mwa vyanzo vikubwa vya mapato vya timu hizo mbili.

Fedha hizo zinapatikana kupitia kiingilio cha mashabiki katika mechi zinazochezwa siku ya kilele cha matamasha hayo na pia nyingine zinavunwa kupitia mikataba ya udhamini wa matamasha hayo.

Na hicho ndicho kinachotegemewa hivi sasa kwa Yanga ambayo tayari imeshafanya kilele cha tamasha lake, Julai 22 na Simba ambayo imepanga kufanya kilele cha tamasha lake, Agosti 6.

Kupitia tamasha la Wiki ya Mwananchi, Yanga inaripotiwa kuingiza kiasi kisichopungua Sh 600 milioni kutokana na viingilio na mikataba ya udhamini wa tamasha hilo iliyoingia na kampuni na taasisi mbalimbali.

Ni matarajio ya Simba pia kuvuna kiasi kikubwa cha fedha kwenye tamasha lake ambalo siku ya kilele chake, wameshatangaza beki ya viingilio, ambapo kile cha chini kitakuwa ni Sh 5,000.

FEDHA ZA LIGI

Yanga ilipata zaidi ya Sh 100 milioni kama fedha za zawadi kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita kutoka Mdhamini Mkuu, Benki ya NBC wakati Simba iliyomaliza katika nafasi ya pili ilipata zaidi ya Sh 50 milioni.

Kiasi cha Sh 500 milioni kilikwenda kwa Yanga kutoka Azam TV kama bonasi ya kumaliza ikiwa bingwa na Simba iliyomaliza katika nafasi ya pili ikavuna kiasi cha Sh 250 milioni.

Kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la ASFC, Yanga ilijihakikishia pia kiasi cha Sh 50 milioni ambacho mshindi wa mashindano hayo anakipata kila msimu.

WADHAMINI BINAFSI

Kwa kufika hatua ya fainali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na ASFC yanga ilipata zaidi ya Sh 1 bilioni kutoka kwa wadhamini wake binafsi kama fedha za bonasi kwa kufikia makubaliano hayo ikiwa ni utekelezaji wa mikataba iliyopo baina yao.

Simba nayo imevuna zaidi ya Sh 300 milioni kwa kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kumaliza ya pili kwenye Ligi Kuu ya NBC.

SOMA NA HII  WAKATI CHAMA NA PHIRI WAKIPEWA SIFA...MGUNDA AIBUKA NA KUANIKA HILI KUHUSU KUIFUNGA COASTAL JUZI....