Home Habari za michezo HII NDIO AVIC TOWN….SEHEMU WALIPOJIFICHA YANGA …KIBONGO BONGO UNAWEZA KUDHANI NI ULAYA...

HII NDIO AVIC TOWN….SEHEMU WALIPOJIFICHA YANGA …KIBONGO BONGO UNAWEZA KUDHANI NI ULAYA AISEE…


Kikosi cha Yanga kiko Avic Town Kigamboni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ikijinoa huku kambi yao ikiwa na mambo mengi rafiki kwa maandalizi ya msimu mpya, lakini kocha wao Nasreddine Nabi amesisitiza kikosi chake kipo freshi na nyota wote amewaelewa vizuri uwanjani.

Awali Yanga ilipanga kwenda Marekani kwa ajili ya kambi, lakini ikaghairi na kuchagua Uturuki, ila nako dakika za mwisho kutokana na itifaki mbalimbali sambamba na muda mfupi ikaamua kuchomoa na kubaki Avic.

Tathmini iliyofanywa  kwenye kambi hiyo, limebaini ina mambo mengi ya kisasa na rafiki kwa maandalizi ya wachezaji ya msimu mpya ambayo hayapatikani sehemu nyingine Dar es Salaam.

Avic ni kambi ambayo kwa mwezi kila chumba anacholala mchezaji kinalipiwa zaidi ya Sh850,000, huku kukiwa na miundombinu ya kisasa, viwanja vya mazoezi, gym, utulivu wa hali ya juu na mabwawa ya kuogelea.

Miundombinu kama hiyo ndiyo inayopatikana kwenye kambi nyingi za Ulaya na Uarabuni ambako timu nyingi hukimbilia kujificha.

ULINZI NA UWANJA

Kwenye eneo hilo ambako kuna nyumba nyingi zilizopangishwa au kukodishwa kwa muda na wageni asilimia kubwa wakiwa raia wa kigeni ni ngumu mtu wa kawaida kuingia.

Ulinzi ni wa hali ya juu na wala sio mazingira ambayo shabiki anaweza kuruka ukuta, kwani lazima aonekane kutokana na miundombinu ilivyo na ulinzi kwenye uzio huo mkubwa.

Kitu ambacho kocha Nabi ameonekana kufurahishwa nacho ni uwepo wa uwanja wa nyasi za kawaida unaotumika kufanyia mazoezi ambayo hata msimu uliopita yaliwapa mataji matatu.

Katika uwanja huo ukiacha magoli mawili makubwa, pia makocha wa Yanga hata kama watahitaji magoli mengine yanayohamishika na vile vigoli vidogo vya kuwanolea washambuliaji vipo vya kutosha, huku nyasi hizo zikiwa zimekatwa vizuri.

CHAKULA NA MIKUTANO

Wakati wa chakula ipo sehemu maalumu yenye bwalo la kutosha ambalo timu nzima inakaa na kupata chakula kwa utulivu.

Hapa kuna sharti moja aliloweka Nabi. Hairuhusiwi kuingizwa kamera wala simu muda wote wawapo hapo. Hapo ni sehemu ya kula tu na kila mtu ahusike kikamilifu kwenye kula tena kwa muda na hii ni kwa makocha, wachezaji au viongozi.

SOMA NA HII  BAADA YA KUISAIDIA DTB KUPANDA LIGI KUU KISHA IKABADILISHWA JINA...TAMBWE KAIBUKA NA HAYA YA KWAKE...

Kuna jengo lingine kubwa maalumu la mikutano. Hapa ni kama darasani. Yanga wakitaka kujadili mambo yao kwa kina au kufundishana kwa kuandika ama kuchora ubaoni wanakutana hapa.

Pana utulivu mkubwa. Kuna ubao wa karatasi na kalamu yenye wino mzito, ‘projekta’ na televisheni kubwa ambayo hutumiwa kuangalia mikanda ya timu pinzani. Vilevile tathmini ya mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, Agosti 13 itafanyika hapa baada ya kutoka mazoezini.

WAWILI NYUMBA MOJA

Yanga kama ingetoka nje ya nchi ingetumia hoteli ambayo kila chumba hukaa wachezaji wawili, lakini Avic maisha ni tofauti wachezaji wawili wanakaa nyumba moja na kila nyumba ina vyumba viwili vikubwa kila chumba kikiwa na choo cha kisasa, sebule kubwa yenye samani na televisheni.

Eneo hilo lina nyumba nyingi ambazo zingine wamepangishwa raia wa kigeni na vigogo kutokana na gharama kubwa wanazolipa, huku zikiwa zimejengwa kisasa kukiwa hakuna mwingiliano na watu wengine. Nyumba za wachezaji zimejitenga peke yao hakuna mwingiliano wowote na wageni wengine.

APENDACHO AUCHO

Kuna bwawa la kisasa la kuogelea ambalo hutumiwa na wachezaji katika kupunguza mchoko na kujiweka fiti.

Juzi lilishuhudiwa likibadilishwa maji huku mtu maalumu ambaye analihudumia akidai staa ambaye hulitumia zaidi ni kiungo Khalid Aucho ambaye hupenda kufanya mazoezi ya pumzi akiwa majini muda mwingi.

Kambini hapo pia kuna gym ya kisasa iliyoongezewa vitu zaidi kuifanya kuwa ya kisasa zaidi tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.

NABI, MECHI

Kocha Nabi amesema kwamba ameridhishwa na maboresho kwenye kambi hiyo na kwamba hata wachezaji wapya wamefurahia mazingira rafiki kujiandaa na msimu na wanampa imani kuwa mambo yatakwenda vizuri.

“Ukiangalia tangu tumeanza maandalizi kila mchezaji yuko makini na wanafanya mazoezi kwa ushindani mkubwa. Kama tukiendelea na morali hii tunaweza kuwa na maandalizi mazuri wakati tunawasubiri wengine nao kujiunga na sisi,” alisema kocha huyo akiwazungumzia wachezaji ambao wako timu ya taifa.

“Ni bora kuwa hapa (Avic) kuliko kwenda sehemu nyingine ambayo hamjaijua. Tukiwa hapa tunakuwa tuko nyumbani. Tumeanza maandalizi kila mchezaji yuko makini.”