Home Habari za michezo KIPA MBRAZILI KATEMA BUNGO BWANA, AMESHAPEWA MKONO WA KWAHERI, MWAMBA HUYU HAPA...

KIPA MBRAZILI KATEMA BUNGO BWANA, AMESHAPEWA MKONO WA KWAHERI, MWAMBA HUYU HAPA SASA KUTOKA AMERIKA ATUA MSIMBAZI

kipa wa simba

KIPA Mbrazili Jefferson Luis amechemka mazima na ameshapewa mkono wa kwaheri Msimbazi. Kama mambo yatakwenda kama yalivyosetiwa pale langoni kinatua tena chuma kutoka Bara la Amerika.

Yaani maana yake ni kwamba kwenye mechi za kwanza za Simba ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika pale kwenye milingoti kitakuwa kimesimama chuma cha El Salvado, Peru au Venezuela.

Simba rada yao iko kwenye makipa watatu kutoka kwenye nchi hizo ambazo wako kwenye timu kubwa ingawa bado imekuwa siri nzito.

Simba ilimsajili Jefferson kama mpinzani wa Aishi Manula ambaye ni majeruhi na atakaa jukwaa mpaka Novemba. Baada ya mazoezi ya siku mbili ndani ya jezi ya Mnyama, Mbrazili huyo alipata majeraha yatakayomuweka nje kwa muda mrefu lakini vilevile za ndaani kabisa zinadai hata baadhi ya wachezaji waandamizi waliubonyeza uongozi kwamba kipa huyo aliyeletwa na mmoja wa vigogo wa benchi la ufundi bado ubora wake hauendani na Simba wanayoitazamia msimu huu.

Ndio maana akachomolewa mapema hata kabla hajafika Tanzania.

Simba wamechungulia sokoni kwa makipa wa Afrika na kupata majina kadhaa lakini hawana mpango nao. Wanataka kipa kutoka Bara la Amerika ambaye atakuja na kitu kipya lakini asiyejua chochote kuhusiana na siasa na ‘shoti’ za soka la Afrika.

Sasa rasmi Simba imeanza kufanya mchujo wa makipa hao ikitafuta mmoja tu ambaye ataungana na Ally Salim na bwana mdogo Ahmed Feruz aliyepandishwa kutoka timu ya vijana kusimama katika milingoti mitatu ya wakali hao wa Msimbazi.

Hata hivyo, Simba italazimika kumlipa pesa Jefferson ili kuvunja mkataba wake alioingia wiki mbili zilizopita lakini pia itamlipa stahiki nyingine ambazo anastahili kutokana na mkataba wake ulivyo ingawa haziwezi kuwa kubwa za kuwaumiza vichwa na wameafikiana na Jefferson na muda wowote kuanzia leo atasepa zake.

Awali Simba ilikuwa na mpango wa kuwarudia makipa watatu iliokuwa imeanzisha mazungumzo nao kabla ya kumsajili Jefferson lakini imewapiga chini kwa madai kuwa inakwepa mitego kadhaa ikiwemo siasa za mipira ya Afrika na hujuma. Sasa akili yao inachakata majina hayo matatu ya kutoka El Salvador, Venezuela na Peru ambao hawafahamiki kabisa Afrika, lakini ikielezwa kuwa wanadaka timu zao za taifa japo si namba moja.

Makipa ambao awali Simba ilitaka kuwarudia ili wachukue mikoba ya Jefferson ni Mbrazili Caique Da Santos ambaye alishindwa kutua kutokana na kuhitaji pesa nyingi.

Mwingine ni yule Mcameroon Simon Omossola aliyewahi kuichezea AS Vita lakini kwa sasa anakipiga Saint Eloi Lupopo ya DR Congo sambamba na Muivory Coast Issa Fofana kutoka Al Hilal ya Sudan ambayo Simba imetajiwa pesa nyingi ili kumnunua jumla.

Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally alithibitisha; “Tunapambana kutafuta kipa mwingine baada ya kuachana na Mbrazili, tutatoa taarifa rasmi karibuni.”

SOMA NA HII  HUO MKWARA WA SIMBA KWA ASEC SIO POA