Home Habari za michezo ONANA, MIQUISSONE WAPEWA MTIHANI HUU

ONANA, MIQUISSONE WAPEWA MTIHANI HUU

Tetesi za usajili Simba

Baada ya kurejea kambini nchini Uturuki, Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira Robertinho ameanza na mastaa wapya akiwemo Luis Miquissone na Willy Onana.

Robertinho hakuwa kambini kwa siku saba zilizopita programu zote alimuachia Kocha msaidizi Mtunisia Sellami Ouannane aliyesimamia timu katika kipindi chote hicho.

Akizungumza baada ya kurejea kambini hapo, Robertinho amesema kazi ya kwanza ni kutengeneza muunganiko wa timu haswa eneo la Ushambuliaji.

Kocha huyo amesema atahakikisha mastaa wapya wote walioingia kwenye dirisha hili wanatengeneza uwiano sawa kati ya wale watakaoanza kwenye kikosi cha kwanza na wale watakaoanzia benchi.

“Nataka kila mchezaji wakiwemo Miquissone na Onana wajitume kwa asilimia zote ili kupata nafasi.

Tumesajili wachezaji wazuri sasa kinachofuata ni kutengeneza timu yenye muunganiko imara

kwa ajili ya michuano mbalimbali ambayo tunayo msimu huu,” amesema Robertinho na kuongeza;

“Naamini muda tulionao tutalifanikisha hilo kwa umoja na msimu ujao utakuwa bora zaidi kwetu.”

Simba SC tayari imefunga usajili kwa kushusha jumla ya majembe 10 mapya ambapo kati yao wazawa ni wanne mabeki, David Kameta ‘Duchu’ na Hussein Bakari ‘Kazi’, kiungo mkabaji Abdallah Hamis na mshambuliaji Shaaban Chilunda.

Wachezaji wa kigeni waliotua Simba SC katika dirisha kubwa hili ni sita, Kipa Mbrazil Jefferson Luis, beki Mcameroon Che Malone Fondoh, kiungo Mkongomani, Fabrice Ngoma na washambuliaji, Mcameroon Onana, Muivory Coast, Kramo Aubin na Miquissone raia wa Msumbiji aliyerejea Simba SC baada ya kuuzwa Al Ahly miaka miwili nyuma.

Idadi hiyo ya wachezaji imefanya Simba SC kutimiza wachezaji 12 wa kigeni katika kikosi chao kama inavyotakiwa na kanuni na taratibu za ligi, kwani tayari imemuuza Msenegal Pape Sakho kwenda Quevilly Rouen Metropole ya Ufaransa na kuachana na Mmalawi, Peter Banda.

SOMA NA HII  MCHEZAJI STARS AKUMBWA NA MAJANGA HAYA UBELGIJI...ISHU NZIMA HII HAPA