Home Habari za michezo ROBERTINHO ANOGESHA USAJILI WA SIMBA AJA NA MDAKA RISASI KUTOKA BRAZILI…… HUKU...

ROBERTINHO ANOGESHA USAJILI WA SIMBA AJA NA MDAKA RISASI KUTOKA BRAZILI…… HUKU SABABU ZAKUWEKA KAMBI UTURUKI ZATAJWA

Tetesi za Usajili Simba

WAKATI Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho Oliveira, akiwasili nchini alifajiri ya jana pamoja na kipa mpya, Mbrazili Caique Luiz Santos da Purificacao, klabu hiyo imesema inaendelea kufanya usajili huku ikitoa sababu muhimu za kwenda kuweka kambi ya wiki tatu nchini Uturuki kujiandaa na msimu ujao.

Kwa mujibu wa chanzo chetu ndani ya klabu hiyo, kilieleza kuwa Robertinho ametua na kipa huyo ambaye ni mbadala wa Beno Kakolanya aliyemaliza mkataba na timu hiyo, lakini akitarajiwa kuanza kulinda lango la Simba kutokana na Aishi Manula kuwa nje kwa kipindi cha miezi minne akiuguza jeraha baada ya kufanyiwa upasuaji mwezi uliopita.

Kuhusu kwenda kuweka kambi Uturuki, akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema wameamua kwenda mji mkuu wa nchi hiyo, Ankara kwa ajili ya kuwapa utulivu wachezaji wao, kupata viwanja bora vya kufanyia mazoezi pamoja na vifaa vya kisasa, lakini kupata mechi kadhaa za kirafiki na timu nzuri, bora na zenye viwango vikubwa.

Ahmed alisema kikosi cha wachezaji wa Simba kitaondoka mapema wiki ijayo kikiwa na wachezaji wake wote mpaka wale wapya ambao wamesajiliwa msimu huu.

“Baada ya majadiliano ya viongozi na benchi la ufundi, hatimaye tumefikia mwafaka kwenda Uturuki kwenye jiji la Ankara ambako ndiko tunaenda kuweka kambi yetu na sababu ni kwamba tunataka kupata utulivu, kupata huduma zote , eneo tulivu, viwanja bora vya kufanyia mazoezi, tunataka kupata mechi nyingi nzuri za kirafiki dhidi ya timu bora zenye viwango vikubwa, ukijumlisha yote hayo, tumeona huko kunatufaa kufanya maandalizi mazuri ya ‘pre season’, hivyo rasmi tunatoa taarifa kuwa Mnyama Simba anakwenda zake Uturuki kwenda kujifua,” alisema.

Aliitaja sababu ya ziada kuwa huko ndiko kulikochezwa fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliomalizika kati ya Manchester City ya England dhidi ya Inter Milan ya Italia Juni 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ataturk Olympic jijini Istanbul, Man City ikishinda bao 1-0 na kutwaa ubingwa.

Ahmed alisema kwenda Uturuki pia ni mapendekezo ya Robertinho kupata muda wa wiki tatu hadi nne kwa ajili ya kukaa na wachezaji wake katika mazingira mazuri yenye utulivu ili kuandaa timu iliyo imara.

“Nadhani mmeona taarifa yetu kwamba tunaelekea nchini Uturuki kwa ajili ya kuweka kambi kuelekea msimu unaokuja, kila kitu kimewekwa vizuri na kocha Robertinho amewashawasili nchini akiwa na baadhi ya wasaidizi wake.

Kikosi kitaondoka nchini Julai 11, mwaka huu baada ya wachezaji wote kufika, waliokuwapo tangu awali na wapya watakuwa wamewasili kabla ya Julai 11, mwaka huu na kuwapo katika msafara huo,” alisema Ahmed.

Akizungumzia usajili, Ahmed alisema bado wao wanaendelea na usajili ingawa tayari wameshasajili baadhi ya wachezaji.

“Wachezaji tuliowasajili na tunaendelea kuwasajili wataonekana siku hiyo uwanja wa ndege siku ya safari, maana mipango yao yote itakuwa imeshakamilika, hiyo ina maana wiki hii tutawatangaza wachezaji wetu wote tuliowasajili na kwenye suala hili niwathibitishe mashabiki wa Simba kuwa mambo ni mazuri, tumedhamiria kufanya usajili babkubwa na sisi wachezaji wetu siyo wale waliopewa ‘thank you’ na klabu zingine.

“Sisi tunasajili wachezaji ambao tunanyang’anyana sokoni, yaani klabu yake inamtaka, zingine hadi za Afrika na Ulaya zinawataka, kwa hiyo aina hiyo ya usajili huwa inachukua muda kidogo, kama ingekuwa ni wale walioachwa au hawana timu, saa hizi tungekuwa tumeshamaliza siku nyingi.

Mmoja wa wachezaji ambao Simba inatarajiwa kumtangaza ni beki wa kati Che Fondoh Malone ambaye pia inadaiwa alikuwa akiwaniwa na FC Zurich ya Uswisi.

Simba inatarajia kuondoka nchini Julai 11, mwaka huu kuelekea Uturuki kabla ya kurejea baada ya wiki tatu kwa ajili ya Tamasha lao la Simba Day na baadaye kuanza mikikimikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara na CAF Super League.

Licha ya kutowaweka wazi wanawasili lini gazeti hili limepata taarifa kuwa tayari nyota hao wameanza kuwasili tangu usiku wa juzi.

Baadhi ya nyota wanaotajwa ni Willy Onana kutoka Klabu ya Rayon Sport ya Rwanda, Beki Mcameroon Che Fondoh Malone na Efoe Novon kutoka Klabu ya Asko Kara ya Togo.

SOMA NA HII  HII HAPA NDIO MITEGO MIWILI YA YANGA