Home Habari za michezo SAMATAA KUVUNA MSHAHARA WA MABILIONI HAYA KWENYE KLABU YAKE MPYA YA UGIRIKI…

SAMATAA KUVUNA MSHAHARA WA MABILIONI HAYA KWENYE KLABU YAKE MPYA YA UGIRIKI…

Habari za Michezo

Wakati nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akitarajia kupokea zaidi ya Sh2.7 bilioni kwa mwaka kutoka PAOK FC ya Ugiriki aliyojiunga nayo juzi, mshambuliaji huyo atacheza sambamba na wachezaji mbalimbali waliowahi kutamba katika klabu na timu tofauti za taifa za soka duniani kwa nyakati tofauti.

Samatta alijiunga na PAOK juzi akiwa mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba na Fenerbahce ya Uturuki aliyoitumikia kwa miaka mitatu baada ya kumsajili akitokea Aston Villa ya England.

Kwa mujibu wa mtandao wa Hellas Postsen wa Ugiriki, Samatta mwenye umri wa miaka 30, atapokea kitita cha Euro 1 milioni (Sh2.75 bilioni) kwa mwaka ndani ya PAOK ambayo amejiunga nayo kwa mkataba wa miaka miwili kukiwa na fursa ya kuongeza mwaka mwingine hivyo kuwa mitatu.

“Taarifa kutoka Uturuki zinasema Samatta atakuwa na mshahara wa Euro milioni moja sawa na ule wa Nelson Oliveira,” ulifafanua mtandao huo.

Kikosi cha PAOK ambacho kinanolewa na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Romania na klabu za Al Hilal na Rapid Bucurest, Răzvan Lucescu kinaundwa na baadhi ya nyota waliowahi kutamba Ulaya hasa katika ligi kubwa.

Nyota wa zamani wa Shakhtar Donetsk na timu ya taifa ya Brazil, Taison atakuwa ni miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo ambao Samatta atacheza nao mwingine akiwa ni beki wa Nigeria, William Paul Troost-Ekong aliyewahi kuzichezea Gent, Udinese na Watford.

Nahodha wa PAOK ni Vieirinha aliyewahi kuzichezea Porto, Wolsfburg na timu ya taifa ya Ureno lakini pia yupo winga wa zamani wa Serbia na Benfica, Andrija Živković. Mastaa wengine waliopo kwenye timu hiyo ni Abdulrahama Baba, Lucas Taylor, Tomasz Kędziora na Rafa Soares.

Msimu ujao, PAOK itashiriki katika mashindano ya Uefa Conference League, baada ya kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Ugiriki msimu uliopita ambao AEK Athens ilitwaa ubingwa.

Ni timu inayoshika nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya mashabiki nyuma ya Olympiacos na Panathinaikos na inatumia Uwanja wa Toumba unaoingiza mashabiki 28,703. PAOK inakuwa timu ya tano kwa Samatta kuichezea Ulaya ambapo amezitumikia pia Fenerbahce, Genk, Royal Antwerp na Aston Villa.

SOMA NA HII  BAADA YA KUWAONYESHA KAZI AL AHLY JANA...MASHABIKI SIMBA WAMPIGIA MAGOTI KIBU D...