Home Habari za michezo SIMBA SC KUSHUSHA WACHEZAJI HAWA SITA NA KUKAMILISHA USAJILI WAKE MSIMU HUU

SIMBA SC KUSHUSHA WACHEZAJI HAWA SITA NA KUKAMILISHA USAJILI WAKE MSIMU HUU

Habari za Simba SC

Simba imepanga kukamilisha zoezi lake la usajili kwa kunasa na kutambulisha nyota sita ambao wataungana na wengine siku chache zijazo huko Uturuki walikoweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya.

Wachezaji hao sita wapya pamoja na wengine wanne ambao bado hawajaungana na timu kwa sababu binafsi sambamba na kipa Aishi Manula ambaye anauguza majeraha yake.

Katika kundi la wachezaji hao sita wapya, Simba imepanga kusajili nyota wa kigeni watatu ambao kati yao, mmoja ni wa nafasi ya kiungo wa ulinzi, kipa pamoja na kiungo mshambuliaji huku pia wengine watatu wakiwa wazawa ambao mmojawapo atakuwa beki wa kati.

Hata hivyo, maingizo ya wachezaji wawili wa kigeni yatategemea kufanikiwa kwa mpango wa timu hiyo kuachana na winga Peter Banda ambaye inataka kumtoa kwa mkopo pamoja na kukamilika kwa Pape Osmane Sakho ambaye anawaniwa na klabu kadhaa barani Ulaya.

“Tutasajili wazawa kama watatu na wageni watatu lakini kwa upande wa wageni ni hadi pale suala la Sakho na Banda litakapomalizwa kwa vile kanuni inatubana kuwa na wachezaji wengi zaidi wa kigeni,” kilisema chanzo kutoka ndani ya timu hiyo.

Ikumbukwe kuwa hadi sasa Simba ina wachezaji 11 wa kigeni na imebakiwa na nafasi moja tu ya kusajili nyota kutoka nje ya nchi ambapo wageni ilionao ni Aubin Kramo, Sakho, Banda, Sadio Kanoute, Saido Ntibazonkiza, Willy Onana,Jean Baleke, Clatous Chama, Enock Inonga, Che Fondoh na Moses Phiri.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kuwa bado hawajamaliza utambulisho wa wachezaji na hivi karibuni wataweka hadharani wengine.

“Tumefanya usajili mzuri na bado kuna vifaa vingine vitatambulishwa hivi karibuni. Kuna mchezaji mkubwa tuliyemsajili kutoka timu kubwa Afrika naye atakuwa miongoni mwao.

“Safari hii tunajipanga vilivyo na lengo letu ni kufanya vizuri katika mashindano yaliyo mbele yetu,” alisema Try Again.

Meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa kazi ya kusuka kikosi chao bado inaendelea.

“Wachezaji waliopo Uturuki ni 17 lakini wengine wataungana nao wakiwemo nyota wetu wapya ambao wataungana na timu hukohuko,” alisema Ally.

SOMA NA HII  UNAAMBIWA MASTAA HAWA WATATU TU NDIO WAMEMKOSHA BENCHIKHA