Home Habari za michezo WAKATI MASHABIKI WAKINGOJA ‘THANK YOU’ INGINE….MASTAA WOTE SIMBA WAITWA FASTA DAR…

WAKATI MASHABIKI WAKINGOJA ‘THANK YOU’ INGINE….MASTAA WOTE SIMBA WAITWA FASTA DAR…

Habari za Simba SC

SAIDO Ntibazonkiza, Clatous Chama na Shomary Kapombe walikuwa wakila bata makwao kipindi hiki cha mapumziko, lakini ghafla wakapigiwa simu na mabosi wao na kutakiwa kukatisha likizo hizo na fasta watue jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa michuano.

Sio Chama na Saido tu, bali hata wachezaji wengine 21 wa kikosi cha sasa cha timu hiyo wakiwamo kipa Aishi Manula anayejiuguza kwao mjini Morogoro naye ametakiwa kufika Dar kama ilivyo kwa Kibu Denis, Shomary Kapombe, Ismael Sawadogo, Habib Kyombo na John Bocco.

Nyota hao wa Simba wameitwa na mabosi hao kwa ajili ya vipimo vya afya watakavyochukuliwa kuanzia kesho kwa kundi la wachezaji wazawa kabla ya kuhamia kwa wageni, kisha kufuata nyota wale waliosajiliwa na kikosi hicho akiwamo Leandre Willy Onana Essomba aliyetoka Rayon Sports.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, mabosi wa Simba wameamua kuwaita wachezaji wote ili kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya safari ya nje ya nchi zikitajwa Afrika Kusini au Uturuki itakapowekwa kambi ya maandalizi ya msimu mpya kulingana na maelekezo ya Roberto Oliveira.

Kundi la kwanza la wazawa litakalopimwa kuanzia Jumatatu, linahusisha wachezaji 12 waliopo kikosi cha sasa akiwamo nahodha John Bocco, Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Kibu Denis, Ally Salim, Ahmed Feruzi Teru, Israel Mwenda, Mzamiru Yasin, Jimmyson Mwanuke, Nassor Kapama, Habib Kyombo na Mohamed Mussa.

Kundi la pili litakalojumuisha wachezaji 10 wageni na kipa Aishi Manula aliyetoka kufanyiwa upasuaji hivi karibuni Afrika Kusini, litafanyiwa vipimo Jumanne likiwa na Ismael Sawadogo, Moses Phiri, Joash Onyango, Sadio Kanoute, Jean Baleke, Saido, Chama, Henock Inonga, Peter Banda na Pape Ousmane Sakho.

“Haya ni maandalizi ya kuanza safari ya kwenda kwenye kambi ya maandalizi ya msimu mpya, kocha kataka wote wafanyiwe vipimo mapema kisha zianze taratibu za safari ya kwenda kuweka kambi ya msimu mpya, kisha naye atajumuika wiki chache zijazo sambamba na nyota wapya walisajiliwa na watakaosajiliwa,” alisema mmoja wa vigogo wa klabu hiyo aliyeomba kuhifadhiwa jina.

Kigogo huyo alisema wito huo unajumuisha wachezaji wote bila kujali kana kuna waliopo kwenye hesabu za kupewa ‘Thank You’, kwa vile hadi sasa hakuna maamuzi mengine yaliyofanyika baada ya kutemwa kwa nyota wanane Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Beno Kalolanya na Gadiel Michael.

Wageni waliopigwa chini hadi sasa ni Wanigeria Nelson Okwa na Victor Akpan, Mghana Augustine Okrah na Mohamed Ouattara kutoka Burkina Faso, na Ismael Sawadogo, huku Joash Onyango na Peter Banda wakitajwa wapo kwenye mazungumzo kutokana na kuwa na mikataba inayowabana.

Onyango inaelezwa ameomba kuondoka Msimbazi, huku Peter Banda akikomaa akitaka kuvunjiwa mikataba kama hayupo kwenye mipango ya kocha Robertinho na sio kupelekwa kwa mkopo katika klabu nyingine.

Kwa wazawa Kennedy Juma anatajwa kuwa nyota wa tisa kupewa ‘Thank You’ baada ya kugoma kuongeza mkataba kwa kilichoelezwa yupo mbioni kutua Singida BS ndio maana jina lake halikuwekwa kwenye orodha ya nyota hao waliokatiziwa likizo zao ili waje Dar.

SOMA NA HII  BAADA YA KUFUNGWA NA WAIVORY JUZI..SIMBA WAONA ISIWE TABU..WAANDIKA BARUA CAF...