Home Habari za michezo SIMBA HII SASA HATARI KILA IDARA, ROBERTINHO AFUNGUKA MSIMAMO WAKE

SIMBA HII SASA HATARI KILA IDARA, ROBERTINHO AFUNGUKA MSIMAMO WAKE

Habari za Simba SC

NI sahihi kusema Simba pale mbele imeenea. Kocha wa Simba, Olivier Robert Robertinho amesisitiza kwamba msimu huu ni bandika bandua na mashabiki wataanza kujionea wikiendi hii kwenye Simba Day pale Kwa Mkapa.

Simba msimu uliopita ilikuwa na mapengo sehemu kadhaa kwenye kikosi, sehemu ya kiungo mkabaji na beki wa kati ni maeneo ambayo yaliwasumbua, lakini msimu huu kila kitu kimekuwa sawa baada ya timu hiyo kuwasajili, Che Malone anayecheza beki wa kati.

Lakini pale kwenye eneo la kiungo mkabaji ambalo lilikuwa na Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute, ameongezwa Fabrice Ngoma ambaye anatajwa kuwa moja kati ya mastaa kwenye timu hiyo.

Simba msimu uliopita ilifunga mabao 75 ikiwa ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu, wengi wakiamini hawawezi kusajili washambuliaji, lakini Kocha Robertinho amefunga busta mpya na kutangaza rasmi kwamba amemaliza tatizo la kipindi cha pili. Ameomba siku saba kupata kikosi cha pili matata zaidi kwani tayari cha kwanza anacho. Msimu huu pale mbele ameshusha Luis Miquissone, Willy Onana, Aubin Kramo kuhakikisha wanafunga mabao mengi zaidi msimu huu, kadirio la chini marambili ya yale ya msimu uliopita. Hali hiyo imewatisha mashabiki wa timu pinzani ambao wanaamini kuwa hakuna anayeweza kukizuia kikosi hicho kutwaa ubingwa msimu huu, lakini ni rahisi kwa namba hizi kuamini kuwa mtu akienda kichwakichwa atapigwa nyingi. Mchambuzi wa Mwanaspoti Oscar Oscar ‘Mzee wa Kaliua’ ameweka wazi kwamba karata yake ya ubingwa anaiweka Simba msimu ujao. Jiulize, kikosi cha Simba kiwe na Clatous Chama, Onana, Kramo na juu yao anakaa fundi Baleke.

MATAIFA MATANO

Kwanza itakuwa ni safu ya ushambuliaji yeye mastaa wa nchi tano tofauti, Chama kutoka Zambia, Luis Msumbiji, Onana Mcameroon, Kramo kutoka Ivory Coast na mshambuliaji wa mwisho ni Baleke raia wa Congo.

Kuonyesha kuwa wamepania, mataifa haya yote yana nguvu kubwa kwenye soka la Afrika na yamekuwa yakitoa mastaa wengi ambao wanacheza kwenye klabu kubwa za Ulaya.

WANA VITU

Msimu uliopita, Baleke mwenye miaka 22, alifunga mabao 14 akiwa alijiunga na timu hiyo Januari kwa mkopo kuonyesha kuwa ana uwezo mzuri zaidi wa kufunga mabao mengi zaidi msimu huu kwa kuwa atakuwa na muda mwingi zaidi wa kucheza.

Kwa upande wa Onana ambaye alikuwa anaitumikia Rayon Sports, inaelezwa ameshaonyesha mambo makubwa kwenye kambi ya Simba, akiwa na uwezo mkubwa wa kukimbia na mpira, kupiga mashuti na kutoa pasi safi za mabao.

“Naona kama kuna timu itakuja vibaya itachapwa mabao mengi , Onana anaonyesha vitu vya hatari uwanjani ana uwezo wa kufanya kila kitu ambacho mchezaji wa juu anatakiwa kufanya,” alisema Ahmed Ally, Msemaji wa Simba.

Pamoja na pasi alizotoa Onana, alifunga mabao 10 kwenye msimu wake wa mwisho nchini Rwanda akiwa ameshatajwa na Chama kuwa ni usajili bora kwa Simba msimu huu.

Kwa upande wa Kramo, ambaye mashabiki wamekuwa hawajamuelewa sana, huyu ni kati ya wachezaji wa juu ambao wanatajwa kuwa wanaweza kufanya mambo mazuri kwenye eneo hilo msimu huu.

“Tuna wachezaji wenye kiwango kizuri, vipaji vya hali ya juu, kama ukimtazama Kramo anavyocheza anakuonyesha kuwa anaweza kufanya jambo lolote uwanjani.

“Pasi zake ni nzuri, ushirikiano wake na wenzake uwanjani ni wa hali ya juu, lakini anajua kufunga kwani ameshatuonyesha hayo mazoezini,” alisema kocha wa Simba Robertinho.

Winga huyo wa kushoto aliifanya Asec Mimosas kuwika msimu uliopita huku akionyesha uwezo wa juu kwenye michezo yote ambayo alicheza, kasi yake, lakini krosi zenye macho zitaifanya Simba izalishe mabao mengi msimu ujao na kuwatisha wengine.

Pia faida nyingine kwa Simba ni kuwa na uwezo wa kucheza sehemu zote, kulia na kushoto, akiwa sasa ana umri wa miaka 27, umri ambao ni bora kwa washambuliaji. Kwa upande wa Luis mwenye miaka 28 umri mwingine safi kwa washambuliaji, mashabiki wamekuwa hawana wasiwasi naye kwa kuwa wanakumbuka kazi ambayo aliifanya hadi kusajiliwa na klabu bora Afrika, Al Ahly ambapo alicheza michezo 21 na kufunga mabao matano, kucheza tu pale kunaonyesha yeye ni bora.

Huyu ni kati ya wachezaji ambao wanamuunganiko mzuri na Chama ambaye walifanikiwa kuonyesha uwezo mkubwa wakiwa pamoja, yakiwa ni mafanikio ya Simba ya kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hivi karibuni yaliazia kwao.

Kufunga mabao 10 kwa msimu haliwezi kuwa jambo la ajabu kwake na kama mstari wa mbele wote unavyooneka utakuwa fiti, hakuna anayeweza kuwazuia kutwaa ubingwa.

“Mashabiki wasubiri kuona uwanjani, naamini bado ubora wangu ni wa juu na naweza kufanya zaidi ya pale kwa kuwa nimejifunza mengi zaidi, siyo kweli kwamba nimeongeza uzito, nipo kwenye kilo sahihi alisema Luis.

Chama pamoja na kufunga, lakini washambuliaji hao wakae mkao wa pasi za mabao kwani anatambulika kuwa ni fundi wa kazi hiyo akiwa msimu uliopita alitoa pasi 17 zilizozaa mabao.

MABAO 37 NJE?

Kama hawa hawataanza, siyo ajabu Simba ikawa na wachezaji wa akiba hatari zaidi, Moses Phiri ni kati ya wachezaji mahiri wanaokaa nje Simba lakini mashabiki wanaamini walitakiwa kuanza kutokana na ubora wake, msimu uliopita alifunga mabao 10 kwenye michezo michache.

Lakini usisahau kuwa kikosi cha juu hakina mfungaji bora wa msimu uliopita, Saido Ntibazonkiza aliyefunga mabao 17.

Lakini pia, John Bocco ni mshambuliaji hatari ambaye michezo michache tu alifunga mabao 11, tusubiri tuone. Ukijumlisha mabao hayo ya watatu utapata mabao 37 yamekaa nje.

SOMA NA HII  MENEJA WA YANGA NAE AJA NA HILI KWENYE MECHI YA SIMBA NA YANGA