Mkurugenzi na Rais wa Kampuni GSM Group, Ghalib Said Mohamed ambae pia ni Muwekezaji mdhamini Mkuu wa Young Africans amezungumza kwa mara ya kwanza baada ya jana kumalizika kwa fainali ya Ngao ya Jamii 2023 kati Yanga SC dhidi ya Simba Sports Club katika uwanja wa Mkwakwani Mkoani Tanga.
Akizungumza na millardayo.com alisema; “Kipekee ningependa kabisa kuwashukuru Wanachama, Mashabiki na Wapenzi wa Young Africans SC kwa kujitokeza kwa wingi jana Mkwakwani katika mchezo wa fainali ya Yanga SC dhidi ya Simba.
“Mchezo umemaliza dakika tisini kisha dakika tatu za nyongeza Wachezaji wetu wamecheza kiume haswa, tusikate tamaa wanayanga tuendelee kuwapa moyo wachezaji wetu safari bado ni ndefu, Yanga Daima mbele nyuma mwiko.
“Tuna wachezaji wazuri kikosi kipo imara mpira wa jana wameupiga mwingi uwanjani na kila kheri kwenye michuano inayofuata Yanga Bingwa,” amesema Mkurugenzi na Rais wa Kampuni GSM Group, Ghalib Said Mohamed.
Haya yote yameibuka baada ya Simba SC kufanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii mbele ya Yanga kwa ushindi wa penati 3-1 baada ya dakika 90 kumalizika 0-0 katika mchezo uliochezwa jana Agosti 13, 2023 kwenye Uwanja wa Mkwakwani Mkoani Tanga.
Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Simba na Yanga kucheza fainali ya Ngao ya Jamii, mbili zilizopita zote alichukua Yanga SC kwa kuifunga Simba SC.