Home Habari za michezo DAWA YA KIBU KUCHEZA KIKOSI CHA KWANZA SIMBA HII HAPA

DAWA YA KIBU KUCHEZA KIKOSI CHA KWANZA SIMBA HII HAPA

Habari za Simba

Nilikuwa nasoma mahala Himid Mao akimzungumzia mchezaji wa Simba, Kibu Denis. Kwamba walinzi wengi watachukia kumkaba mchezaji wa aina yake. Ni msumbufu. Ni kweli ana matumizi mengi ya nguvu uwanjani.

Wakati mwingine akili yake inakwama uwanjani lakini ukweli ni kwamba akipatia huwa anapatia haswa. Na zaidi ya hayo mashabiki wa Simba wanashangaa kwanini kocha wa Simba, Robertinho anapendelea kumpanga Kibu.

Kabla yake, tangu atue Simba Kibu hajawahi kuwa mchezaji wa benchi. Anaweza kuanza mechi au kuingia baadaye. Hajawahi kusugua benchi mechi tatu mfululizo akiwa fiti. Kuna mashabiki wamegawanyika mtazamo kuhusu uwezo wake.

Tumeingia katika msimu mwingine wa soka na tumetoka katika dirisha la uhamisho wa wachezaji. Ambacho mashabiki wengi wa Simba wanatarajia ni kuona umuhimu wa mchezaji kama Kibu unapungua uwanjani huku wachezaji wapya wakishika hatamu.

Ukweli ni kwamba kuna uwezekano umuhimu wa Kibu ukaendelea kikosini. Wakati Simba ikiwa Uturuki tulisikia tu kwamba Kibu amefunga katika mechi mbili. Simba imerudi hapa nchini na Kibu ameendelea kucheza kama kawaida.

Kama Simba ikiendelea kuwa na wachezaji laini kikosini umuhimu wa Kibu utaendelea tu. Makocha wanapendelea aina ya mchezaji kama Kibu hasa katika dunia ya kisasa ya soka. Katika dunia hii mpya kumekuwa na umuhimu mkubwa wa wachezaji kuwa wazuri pale wanapokuwa hawana mpira.

Bahati mbaya sisi tumeendelea kuwa makini zaidi na dunia ya zamani ambapo tulikuwa tunaitazama timu wakati ikiwa na mpira zaidi. Kibu anakupa kitu wakati timu haina mpira. Haishangazi kuona wachezaji wasio na vipaji vikubwa wamekuwa na umuhimu mkubwa kikosini kama wale wenye vipaji.

Ukitaka kuwa nyota zaidi katika soka basi changanya vitu vyote. Unaweza kuwa na kipaji kikubwa ukiwa na mpira lakini ukawa na mchango mkubwa wakati timu haina mpira. Siku hizi mpira unakabwa katika maeneo yote ya uwanja.

Mawinga wanalazimika kushuka na kukaba kama mabeki pindi wakati timu haina mpira. Washambuliaji wanapaswa kuanza kukabia juu wakati timu haina mpira. Mambo ya kusubiri mpira ukabwe na kiungo mkabaji au walinzi yamepitwa na wakati.

Kuna wachezaji ambao walinufaika na zama. Hawa ndio akina Zinedine Zidane, Ronaldinho, Andrea Pirlo na wengineo. Zamani zao kuna kitu kilikuwa kinaitwa ‘free role’. Yaani nyie wengine mnacheza kwa ajili ya kuwakabia halafu mnawapasia kwa ajili ya kufanya mipango.

Leo maisha yamekuwa tofauti. Kuna wachezaji wanaoshindwa kucheza kwa sababu ya kukosa ubora wakati hawana mpira. Mchezaji kama Mesut Ozil alijiondoa katika soka la ushindani baada ya Mikel Arteta kutua Arsenal. Mahitaji ya kocha kwake yakawa mengi.

Leo Kevin de Bruyne mchunguze tu wakati Manchester City haina mpira. Anacheza kama Punda. Tatizo watu wengi wanamuangalia akiwa na mpira. Hawa akina Sadio Mane, Roberto Firmino na Mohamed Salah licha ya kuwa bora wakati na mpira pale Liverpool lakini walikuwa punda wakati timu haina mpira kwa ajili ya kuurudisha mpira katika himaya.

Hii kitu inaitwa pressing. Kwa mara ya kwanza niliiona pale Barcelona ya Pep Guardiola. wakipoteza mpira basi huko huko juu Lionel Messi pamoja na ustaa wake anakaba, hapo hapo Xavi Hernandez anasogea, kushoto Andres Iniesta anakuja.

Mchezaji wa kisasa inabidi uwe fiti. Kwa kuanzia tu hapa Tanzania kuna wazawa wengi bado wameendelea kujivunia uwezo wao wakiwa na mpira. Wakiwa hawana mpira hakuna kitu. kwa staili hii Kibu lazima acheze tu.

Fei Toto ni miongoni mwa wachezaji ambao akiwa na mpira ana ubora, asipokuwa na mpira bado ana ubora. Aziz Ki ni mchezaji ambaye alikuwa akisumbuana na Professa Nabi kwa sababu alikuwa hana ubora wowote wakati timu haina mpira.

Njia pekee ya kuwaondoa wachezaji kama Kibu uwanjani ni wachezaji wenye vipaji kujirekebisha na kuwa wapambanaji uwanjani. Sio yeye tu, hata mashabiki wa Simba walikuwa hawamuelewi mchezaji anayeitwa Mzamiru Yassin.

Walichelewa kumuelewa kwa sababu muda mwingi walikuwa wanajaribu kuangalia ubora wake wakati akiwa na mpira. Walichelewa kujua kwamba alikuwa na umuhimu mkubwa wakati timu haina mpira kuliko Clatous Chotta Chama.

Zamani wachezaji wengi wasiokuwa na vipaji ilikuwa inawawia vigumu kucheza. Siku hizi hata wao wanaweza kucheza kwa sababu mchezo wenyewe umekuwa wa kitimu zaidi. Mchezo wenyewe umekuwa na mambo mengi zaidi nje ya kipaji cha mchezaji.

Lakini zamani pia Kibu asingeweza kucheza kwa sababu hata wachezaji wenye vipaji walikuwa wapambanaji wakubwa uwanjani. Mfano ni mchezaji kama Athuman China. Alikuwa na kipaji kikubwa uwanjani lakini alikuwa faru wakati hana mpira. Ni kwa sababu alikuwa fiti.

Leo tuna wachezaji ambao wanakaa maskani na kudanganyana kwamba ‘mpira ni kama Baiskeli, ukijua umejua’. Kocha wa kigeni anapokuja hatazami sana majina. Anaangalia ni wachezaji gani watamsaidia kazi yake. kazi yenyewe imekuwa ngumu kila mahala kwa sababu upinzani katika soka umeongezeka.

Hakuna kocha wa kisasa ambaye atamchukia Kibu. Na kama Simba imechukua wachezaji wapya wenye vipaji lakini legelege basi bado Kibu atacheza tu. Ni kama ambavyo Mzamiru ameendelea kuwa lulu katika kikosi cha Simba na timu ya taifa licha ya makocha kubadilika.

Tuanze kuwatengeneza vijana wetu kuhusu jambo hili. Tusiwasifie ubora wa miguu yao tu. Mpira sio kazi rahisi hasa huu wa kisasa. Ndio maana siku hizi mpira wa takwimu umekuwa mwingi zaidi kwa sababu tunahitaji utimamu wa kimwili wa mchezaji.

SOMA NA HII  YANGA LEO WASIPOKUWA MAKINI HILI NDIO LITAWAKUTA