Home Habari za michezo HUU NDIO UBAYA WA JEZI NO 20 YA CHA MALONE…MASTAA SIMBA WAKAE...

HUU NDIO UBAYA WA JEZI NO 20 YA CHA MALONE…MASTAA SIMBA WAKAE CHONJO…..

Habari za Simba

LILIKUWA soka zuri lililopigwa siku ya sherehe ya kukamilisha kilele cha wiki nzima za shughuli mbalimbali za kijamii zilizofanywa na Wana Simba .

Soka lililoambatana na ufundi mkubwa kutoka kwa wachezaji wa pande zote mbili kwa maana ya wenyeji Simba na wageni wao, Power Dynamos kutoka Zambia.

Makocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wa Simba na mwenzake Masautso Tembo wa Power Dynamo hawakutaka kuficha silaha zao kwa kuwa huu ulikuwa mpambano tofauti wenye malengo tofauti, hivyo waliliacha soka lichezwe.

Simba ilikuwa na malengo mawili , moja kuwaonyesha wapenzi wake sura halisi ya usajili wao na pili kuonyesha nini wamekiandaa kuelekea msimu huu unaoanza ambapo wachezaji wake watashiriki michuano mingi.

Hebu tuwatazame wababe wetu waliotupa ladha ya soka zuri siku ya kilele cha sherehe za siku ya Simba na alama walizopata kwenye mabano.

GOLINI SIMBA WALIANZA NA ALLY SALIM

Hakupata majaribio mengi ambayo yangeweza labda kumsumbua, hata hivyo, kulikuwa na nafasi kadhaa ambazo Ally Salim alicheza kwa ufasaha.

Krosi tatu kipindi cha pili na kona moja ambayo alisafiri kwenda kuichezea na kuidaka kwa utulivu ile aliyoona haipo karibu kuicheza alipangua kwa ustadi mkubwa.

Kwenye soka la kisasa ambapo makipa wamekuwa ni waanzishaji wa mashambulizi kwa kutengeneza ‘Vii Shepu’ alijaribu kuanza kucheza kwa kuanzisha mchezo hata hivyo, bado hajakuwa mwepesi sana, leo anapata alama 8/10

SHOMARI KAPOMBE

Ilikuwa ni kitu cha mwendelezo kwake kufanya safari za kwenda juu na kurudi huku bado akiendeleza utulivu kwenye kuanzisha mashambulizi na kusaidia kukaba. Shomari kama ilivyokuwa kwa mabeki wengine hakupata kazi kubwa kwenye kuzuia, aliendelea kufurahia soka la kasi na pasi nyingi licha ya kuwa hakuwa mwenye kutoa mchango mkubwa hasa kupiga krosi !

Kwa nini Shomari Kapombe hakupanda kila mara kuelekea golini kwa Power Dynamo ni kwa sababu upande aliotakiwa kupita kila mara wachezaji wengi wa mbele walitumika kufungua uwanja ili kuwatoa mabeki wa Power Dynamos katikati ya goli lao 7/10

MOHAMED HUSSEIN

Kiongozi mkubwa ndani ya uwanja akicheza dakika zote 90 huku akifanya mikimbio kwenda mbele au kukokota mipira mara tatu kwa ukamilifu uliompa nafasi ya kupiga krosi au pasi za mwisho.

Alikuwa mwepesi sana kwenye kurudi kuzuia pale alipopoteza mpira ama kwa pasi yake kutofika kwa usahihi au kuzuiwa na wapinzani, Mohamed Hussein hakutengeneza nafasi nyingi kama ilivyo kawaida yake zaidi alikuwa makini kuzuia 7/10

CHE MALONE FONDOH

Ukiiangalia jezi aliyovaa ambayo ilikuwa inatumika na mtangulizi wake ambaye hata hivyo hakuwa akicheza kwenye nafasi moja inayofanana, kinachowafananisha wavaa jezi hii namba 20 ni utulivu ndani ya dimba .

Che Malone alileta utulivu mkubwa kwenye ulinzi, alikuwa mtulivu mno pale anapofanyiwa ‘pressing’ akifanikiwa kupiga pasi zaidi ya 50, anachukua mpira bila kukufanyia madhambi licha ya kufanya hivyo mara moja, akienda hewani kupiga vichwa sahihi mara 4 na kukosa mara moja, ni mapema sana kumpa sifa nyingi labda kutokana na wapinzani Power Dynamo kutofika golini kwa Simba mara nyingi, huyu ndiye staa wao. 9/10

HENOCK INONGA

Beki mzoefu ambaye ndani ya dakika zaidi ya 60 alizocheza alikuwa akicheza kwa furaha na kufanya marembo na mbwembwe nyingi, Inonga alipiga pasi 35 zilizokamilika huku akinyang’anya mipira mara tatu na kukokota mipira mara mbili na akihusika kwenye kupiga shuti nje ya goli.

Ni mchezaji aliyekamilika hasa inapokuja suala la kukaba mchezaji anayemkusudia au kumpania, alipiga mipira mirefu inayohamishika mara nne .

Kwenye kikosi cha wachezaji wa Simba ambao unaona kambi ya nje imewasaidia, yeye ni mmoja wao. 8/10.

MZAMIRU YASSIN

Yupo kwenye orodha ya wachezaji wanaoisaidia timu inapokuwa haina mpira na ikiwa na mpira yeye pamoja na Kibu Dennis na Mohamed Hussein .

Mzamiru anaonekana kutopungua pale alipoishia msimu uliopita na sasa anaanza kuendelea , alifanikiwa kunyang”anya mipira mara tatu huku akikokota mipira mara tatu bila kupoteza ingawa kwenye safari ya kukokota mpira alifikiwa na kunyang’anywa mara mbili hali iliyomlazimu kufanya faulo 6/10

KIBU DENNIS

Ni mzuri kwenye kusaidia kutafuta mipira iliyopotea na kupandisha mashambulizi kwa nguvu alizonazo, bado Kibu hana ule mwendekezo wa kucheza kwa usahihi kila mchezo .

Kibu alikokota mipira mara nne na kupiga pasi sahihi 18 huku akipoteza mara nne.

Kibu ana kosa matumizi ya akili ndani ya uwanja na muda mwingine anakosa umiliki wa mpira pale anapopigiwa pasi huku akiwa katikati ya mabeki. Si rahisi Mungu kukupa nguvu ndani ya uwanja na kukupa utulivu wa akili ya mpira bado Kibu ni msaada sana kwa kocha wake Oliveira 6/10

SAIDO KANOUTE

Nilikuwa namtazama bwana harusi na kumuona kama sasa kakua ndani ya uwanja kwa kucheza kikubwa, kucheza bila faulo za makusudi ni kama kweli kazaliwa upya .

Kanoute alicheza faulo mara tatu huku akionyesha utulivu katikati ya uwanja, alisaidia sana kuipoteza idara ya viungo wa Dynamo na kuifanya Simba kufika mara nyingi golini kwa wageni.

Licha ya Kanoute na Mzamiru kucheza katikati pamoja kwa muda sasa bado Kanoute hajacheza kama Kiungo Bora wa juu kwa kupiga pasi nyingi za mwisho, Kanoute hubaki sana katikati na kupanda mara chache mbele kusaidia kutengeneza mashambulizi ya kila mara. 7/10

WILLY OSAMBA ONANA

Mfungaji wa bao bora la kwanza kwenye mchezo huo , kasi aliyokimbia na mpira kutoka pembeni kuja katikati huku akikata eneo la mbele kwa kasi na jinsi alivyouzungusha mpira ilikuwa moja kati ya nyendo nzuri kwa mchezaji wa aina yake .

Kama ilivyokuwa kawaida macho mengi ya watazamaji yalikuwa kwa Onana MVP wa Ligi ya Rwanda na mfungaji wao bora, Onana hakuwa akicheza katikati ya goli licha ya kuonekana yeye ndiye aliyepangwa kusimama kama mtu wa mwisho .

Ulikuwa ukimuona jinsi anavyohaha kuutafuta mpira kila eneo , kuna kipindi alionekana akitokea kulia, mara kushoto na hakuwa kila mara katikati.

Alipiga shuti matatu golini akipiga pasi nyingi zisopungua 30 huku akipoteza mipira mara tano na kukosa utulivu mara mbili.

Ni usajili unaonekana utalipa kwa kiasi kikubwa kwa aina ya mchezaji kama Onana. 8/10

SAIDO NTIBAZONKIZA

Alianza mchezo kwa kasi nzuri huku akiwa na kiu ya kufunga, Saido mara nyinyi hufungulia kushoto huku akimuacha Chama aingie ndani ya uwanja ili apate nafasi ya kuingia ndani kwa kasi .

Ukimuona Onana amefungulia kulia kuomba mpira na Kibu akiwa kulia bila shaka tulimtegemea Saido kuingia kati na kusimama lakini kutokana na yeye kutopenda kutulia basi haikuwa rahisi kupata mipira sahihi kwenye eneo sahihi.

Bado Saido anatakiwa kuongeza bidii ili afike pale alipoanzia msimu uliopita, hata hivyo Saido hajakuwa bora inapokuja kucheza kwenye michezo ya kimataifa na gonjwa hilo bado juzi kutwa halikumuacha salama, alipoteza mipira mara tatu huku baadhi ya mipira ilipokwa miguuni mwake 6/10

CLATOUS CHAMA

Labda kuchelewa kwake kuingia kambini kule Uturuki na ule mvutano fulani wa mkataba wake na klabu umemfanya awe nyuma.

Chama alipoteza mipira mara nne mara mbili mguuni kwake na mingine ikipotea njiani. Alicheza pembeni zaidi huku akishuka kila mara kuchukua mipira chini.

Pamoja na upungufu aliyonayo ya kutokuwa safi kwenye utimamu wa mwili bado Chama atabaki kuwa Chama sababu ya levo aliyoifikia au aliyoiweka .6/10

FABRICE NGOMA

Mmoja kati ya wachezaji ambao wana Simba wengi walikuwa na hamu ya kumtazama kutokana na usajili wake na heshima aliyonayo kwenye soka la Afrika .

Ngoma alicheza ndani ya dakika 27 na kupiga pasi 30 zilizokamilika, huku akipoteza mipira mara mbili akifanya faulo mbili .

Ngoma bado hana kasi na ndio aina ya soka lake lakini ni mahili sana kwenye kupiga pasi za mwisho zinazofika kwa usahihi. Kwa jinsi mabadiliko yalivyofanywa na uwepo wa Fabrice ndani ya uwanja ina maana yeye si kiungo mzuiaji bali mshambuliaji 7/10.

LUIS MIQUISSONE

Mchezaji aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu na Wana Simba kutokana na kile alichowahi kukifanya huko nyuma na kumfanya kuwa mchezaji aliyeuzwa kwa bei kubwa miaka kadhaa iliyopita.

Luis amerejea na kishindo nje ya uwanja lakini bado Luis hajawa yule Luis, kasi yake siyo ile, wepesi umepotea na mwili umeongezeka.

Alipiga mipira nje ya goli miwili huku akipoteza mipira mara nne na kuchukua mpira mara moja 5/10.

Wengine walioingia wapya ni panoja na Aubin Kramo aliyecheza kwa dakika chache na kuonyesha kuwa angalau mguuni kuna kitu. Abdalah Hamis na Hussein Kazi hawa ni wazawa wanahitaji muda wa kucheza ili waweze kuzungumzwa.

MWANDISHI WA MAKALA HII MAALUMU NI JOSEPH KANAKAMFUMU AMBAYE KITAALUMA NI KOCHA MZOEFU WA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI NA WAARABU...CAF WAZUIA 'JANJA JANJA' YA SIMBA...MSIMAMO WAO HUU HAPA..