Home Habari za michezo FT: TABORA UTD 0-4 SIMBA…..JOBE FREDDY WAANZA KUUWASHA MOTO NBC…CHAMA MHHH…

FT: TABORA UTD 0-4 SIMBA…..JOBE FREDDY WAANZA KUUWASHA MOTO NBC…CHAMA MHHH…

Habari ya Simba leo

Mastaa wapya wa Simba, Omary Jobe na Freddy Kouablan wameanza vyema safari yao ya matumaini ndani ya kikosi hicho baada ya kusajiliwa wakati wa dirisha dogo la usajili lililopita, wakifunga bao moja kila mmoja katika ushindi wa timu yao wa mabao 4-0 dhidi ya Tabora United katika Ligi Kuu Bara.

Wachezaji hao ambao wamesajiliwa Msimbazi kuziba nafasi zilizoachwa na washambuliaji waliotupiwa virago kina Moses Phiri na Jean Baleke, wamefunga mabao hayo katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi dhidi ya Tabora United.

Huo ni mchezo wa pili wa Simba wa kiporo kushinda baada ya uleo uliochezwa Kigoma mwishoni mwa wiki ambao Wekundu wa Msimbazi waliondoka na alama zote tatu dhidi ya Mashujaa FC kwa kuifumua bao 1-0

Jobe licha ya kuifungia Simba katika mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Tembo FC hakufunga katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa FC, Jumamosi iliyopita kama ilivyokuwa kwa Kouablan ambaye yeye hakuwa amefunga bao lolote.

Simba wametumia dakika 19 kupata bao la kuongoza kupitia kwa Jobe ambaye amefunga kwa kichwa akiunganisha kwa ustadi mpira wa faulo uliopigwa na Clatous Chama.

Mwamuzi Ally Mnyupe kutoka Morogoro ameipa Simba faulo hiyo baada ya Andy Bikoko wa Tabora United kumfanyia faulo, Jobe.

Kuingia kwa bao hilo ni kama kumewaongeza Simba morali zaidi ya kusaka mabao mengine ambapo wameendelea kulishambulia lango la Tabora United kama nyuki kupitia nafasi za mara kwa mara walizotengeneza huku wakionekana kumiliki mchezo kwa kiasi kikubwa kwa kupiga pasi nyingi zilizowafikia walengwa kwa usahihi na kuwalazimisha wapinzani wao kujilinda kwa namba kubwa ya wachezaji.

Beki na nahodha wa Tabora United, Said Mbatty amefanya kazi ya ziada katika dakika ya 29 ya mchezo kuzuia mpira uliokuwa unaelekea wavuni ambao ulipigwa na Chama ambaye kabla hajafanya hivyo, ameiwatoka kwa ustadi walinzi wawili wa Tabora United na kupiga mpira huo kwa staili ya kuuzungusha lakini Mbatty akaondosha hatari hiyo.

Mwendelezo huo wa Simba kutawala mchezo ulizaa matunda katika dakika ya 36 ilipofanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa Sadio Kanoute ambaye amefunga akiunganisha kwa kichwa krosi ya Shomary Kapombe.

Mabao hayo mawili yamedumu hadi mwamuzi Mnyupe alipopuliza filimbi ya kuashiria kumalizika kwa kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili kimeanza kwa Tabora United kufanya mabadiliko matatu ya wachezaji ambapo imewatoa Said Mbatty, Eric Okutu na Jackson Mbombo ambao nafasi zao zimechukuliwa na Lambere Jarome, Athuman Abas na Abdallah Madirisha.

Licha ya mabadiliko hayo kuonekana kuichangamsha kidogo Tabora United, Simba wameendelea kuwa tishio kwao na haikushangaza kuona wakipata bao la tatu katika dakika ya 59 ya mechi baada ya kuunganisha pasi ya Chama, bao ambalo lilikuwa la kwanza kwake kuifungia Simba tangu alipojiunga nayo.

Simba imeshindilia msumari wa mwisho katika dakika ya 86 kupitia kwa Kouablan ambaye ameingia katika dakika ya 86 ya mchezo kuchukua nafasi ya Jobe.

Baada ya kuingia kwa bao hilo, timu hizo zimeendelea kushambuliana kwa zamu, lakini Simba imesimama imara kulinda ushindi na kuvuna pointi tatu muhimu katika mechi hiyo.

Katika kipindi hicho cha pili, Tabora United imemtoa pia John Nakibinge na kumuingiza Yohana Nkomola wakati huo Simba iliwatoa pia Ntibazonkiza Saido, Babacar Sarr, Kibu Denis na Kanoute ambao nafasi zao zimechukuliwa na Mzamiru Yassin, David Kameta, Edwin Balua na Luis Miquissone.

Refa Mnyupe kwenye mechi hiyo amewaonyesha kadi za njano Kanoute wa Simba na Heritier Lulihoshi kutokana na faulo walizocheza kwa nyakati tofauti.

Hadi filimbi ya kumaliza mchezo ilipopulizwa, Simba wametoka kifua mbele na ushindi huo ambao umewafanya wafikishe pointi 29 na kuzidi kujichimbia katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi huku Tabora United ikibakia katika nafasi ya 12 na pointi zake 15.

Kikosi cha Tabora United kilichoanza katika mchezo huo kimeundwa na John Noble, Shaffih Maulid, Said Mbatty, Lulihoshi Heritier, Andy Bikoko, Daudi Milandu, Jackson Mbombo, Najim Ibrahim, Eric Okutu, Emotan Cletus na John Ben.

Kwa upande wa Simba, kikosi cha kwanza kilikuwa na Ayoub Lakred, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein, Che Fondoh Malone, Kennedy Juma, Babacar Sarr, Sadio Kanoute, Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza, Kibu Denis na Omary Jobe.

SOMA NA HII  KMC YATANGAZA VITA...MASHABIKI MGUU PANDE MGUU SAWA...TUNAZIDI KUWA IMARA