Home Habari za michezo SIMBA DAY YAWANG’ARISHA MASTAA HAWA

SIMBA DAY YAWANG’ARISHA MASTAA HAWA

Baada ya Yanga kuhitimisha ‘Kilele cha wiki ya Mwananchi’, sasa ni zamu ya wapinzani wao Simba nao pia kuja na tamasha la ‘Simba Wiki na kuhitimisha na ‘Simba Day’ Agosti 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Tamasha hilo ambalo limezoa umaarufu mkubwa nchini linatimiza miaka 15 tangu lilipoasisiwa rasmi mwaka 2009 chini ya aliyekuwa Mwenyekiti, Hassan Dalali na aliyekuwa katibu wake mkuu, Mwina Kaduguda.

Lengo kubwa ni kutambulisha wachezaji wapya watakaoichezea timu hiyo msimu ujao na kupitia makala hii, tunakuletea baadhi ya mastaa ambao walifanya vizuri kupitia tamasha hili.

SHIZA KICHUYA

Kichuya alijizoelea umaarufu kwenye tamasha hili kwa mara ya kwanza alipojiunga na Simba mwaka 2016 akitokea Mtibwa Sugar.

Winga huyo alifanya vizuri na alikaa Simba hadi mwaka 2019 akaanza kutolewa kwa mkopo kwenye Klabu za Pharco na Enppi SC za Misri na baada ya kurejea tu nchini mwaka 2020 alijiunga na Namungo anayoichezea hadi sasa.

MOSES PHIRI

Raia huyo wa Zambia alijiunga na Simba rasmi Juni 15, mwaka jana akitokea Zanaco FC, ya kwao na alimaliza nafasi ya pili kwa ufungaji na mabao 14 nyuma ya mfungaji bora Ricky Banda aliyemaliza na 16.

Katika tamasha la mwaka jana Phiri pia alifanya vizuri na hadi kwenye Ligi Kuu Bara na msimu ulioisha alifunga mabao 10 nyuma ya, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ na Fiston Mayele waliofunga 17.

MEDDIE KAGERE

Mshambuliaji huyu mzaliwa wa Uganda mwenye uraia wa Rwanda alijiunga na Simba mwaka 2018 akitokea Gor Mahia ya Kenya na msimu wake wa kwanza tu alianza kuuwasha moto na kuteka mashabiki wengi.

Katika msimu wake wa kwanza wa 2018/2019, Kagere alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 23 na kama haitoshi aliendelea kutawala tena kwani msimu wa 2019/2020 aliibuka kidedea baada ya kufunga mabao 22.

Baada ya kuichezea Simba misimu minne rasmi nyota huyo mwaka jana aliagwa kwa heshima katika tamasha hilo na kutimkia Singida Fountain Gate na msimu uliopita alifunga mabao manane ya Ligi Kuu Bara.

BERNARD MORRISON

Morrison asiyeishiwa vituko alitua nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2020 na kujiunga na Yanga akiwa mchezaji huru na licha ya kiwango chake kizuri ila aliondoka na kutimkia Simba kutokana na misuguano ya kimkataba.

Licha ya kutua Simba ila nyota huyo alidumu kwa msimu mmoja na nusu na alirejea tena Yanga kwa mara ya pili na msimu uliomalizika kwenye Ligi Kuu Bara alifunga mabao matano na baada ya hapo akapewa mkono wa kwaheri.

EMMANUEL OKWI

Mara ya kwanza kwa nyota huyo kutua nchini ilikuwa mwaka 2010 ambapo alijiunga na Simba akitokea SC Villa ya Uganda.

Okwi alijizoelea umaarufu mkubwa katika soka la Tanzania kwani amewahi kuzichezea timu zote kubwa nchini za Simba na Yanga huku akikumbukwa zaidi msimu wa 2017/18 alipokuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara na mabao 20.

Umahiri wake kwenye kufunga msimu huo uliiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza baada ya kutawaliwa na mahasimu wao Yanga waliotwaa mara tatu mfululizo kuanzia 2014/15, 2015/16 na 2016/17.

AUGUSTINE OKRAH

Wakati akiwa na Bachem United, Okrah alifunga mabao 14 na kutoa pasi mbili (assisti) katika michezo 32 ya Ligi Kuu Ghana na kuiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu nyuma ya Medeama na mabingwa, Asante Kotoko.

Kiwango kizuri alichokionyesha akiwa na timu hiyo ya kwao Ghana ndicho kilichowavutia mabosi wa Simba kumsajili winga huyo ila ushindani wa namba umemfanya kufunguliwa mlango wa kutokea ndani ya kikosi hicho. Okrah alitabiriwa makubwa hasa kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha dhidi ya Yanga Oktoba 23 mwaka jana.

Hadi Okrah anaondoka Simba msimu huu, licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara alikuwa amefunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara.

SOMA NA HII  BAADA YA KUONA SIMBA WAKO 'SIRIAZI SANA' ....NABI KAGUNA , KISHA AKAFUNGUKA HAYA MAPYA...KAANZA UWOGA...