Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA JMOSI….WAFAHAMU AL MERRIKH…KOCHA WAO NI BALAA…WANAKABA SIO POA…

KUELEKEA MECHI YA JMOSI….WAFAHAMU AL MERRIKH…KOCHA WAO NI BALAA…WANAKABA SIO POA…

Habari za Yanga

Mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania (NBPL), Klabu ya Yanga wanatarajia kucheza mchezo wao wa kwanza wa hatua ya pili ya mtoano Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh ya Sudan nchini Rwanda, Septemba 16, 2023.

Mchezo huo unatarajiwa kufanyika katika Dimba la Pele, nchini ya Rwanda ni jirani na Tanzania pia Wananchi Wana mashabiki wengi hiyo ni faida kwao maana watapata sapoti ya kutokasha.

Yanga wamefuzu kuingia hatua hiyo baada ya kuifunga ASAS FC ya Djibouti jumla ya bao 7-1 katika michezo miwili wakati AL Merrikh ikivuka kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya sare ya bao 1-1 ugenini na sare ya bila kufungana wakiwa nyumbani.

Al-Merrikh SC ni Klabu kongwe nchini Sudan na ni miongoni mwa klabu mbili zenye upinzani wa jadi nchini humo, ambapo mpinzani wao ni Al-Hilal Omdurman kama ilivyo Simba SC na Yanga SC kwa hapa Tanzania.

Wakati Ligi ya Sudan inasimama sababu ya mchafuko nchini humo, Merrikh tayari alikuwa amecheza mechi 19 kati ya mechi 34 wakiwa na alama 48, mabao ya kufunga 33 na kuruhusu mabao 8, na wao ndio walikuwa na ukuta mgumu kwenye ligi, huku wakiwa nafasi ya pili ya Ligi nyuma ya Hilal wenye alama 53.

Mwalimu wao Osama Nabih Mahmoud Mohamed Elghamrawy ni mshambuliaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Misri na vilabu mbalimbali ikiwemo Zamalek na vilabu vingine, amewahi kutwaa ubingwa wa CAFCL akiwa na Zamalek, ametwaa timu hiyo hivi karibuni na kufanikiwa kutinga Makundi ya CAFCL baada ya kuitoa Otoho ya Congo Brazaville.

Merrikh ni wazoefu kwenye hatua ya makundi ya CAFCL kwani msimu uliopita tu waliingia makundi lakini wakamaliza mkiani kwa kuwa walikutana na kundi gumu la Zamalek na CR Belouzidad. Mwaka 2021 pia walikuwa kundi moja na Simba SC ya Tanzania.

Yanga msimu uliopita wameweka rekodi yao wenyewe ya kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika tangu lianzishwe mwaka 2004 yalipounganishwa makombe mawili, wakashindwa kwa bao la ugenini, kabla ya hapo hakuna klabu ya Tanzania iliyokuwa imefikia hatua hiyo.

Merrikh wameshatwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho mwaka 2007, wamewahi kuchukua ubingwa wa Kombe la Washindi, kwa hiyo ni wazoefu kwenye michuano ya CAF wakati Yanga mara ya mwisho kufika makundi ya CAFCL ni mwaka 1998.

Al Merrikh si miongoni mwa vilabu 20 bora sana Afrika, Yanga ni miongoni mwa vilabu bora Afrika na kwa mujibu wa CAF Yanga iko nafasi ya 16.

MFUMO Merrikh chini ya Osama ni wazuri sana kwenye kuzuia, wanazuia zaidi na kushambulia kwa kushitukiza lakini Yanga chini ya Gamondi wao wanashambulia sana.

Osama ameifanya Merrikh kufika hapa walipo kwa kuzuia zaidi kisha wanashambulia kwa kushitukiza, walitoa sare ya bao 1-1 ugenini, nyumbani wakatoa sare ya bila kufungana hivyo wakapita kwa faida ya bao la ugenini.

Mfumo wanaotumia Merrikh na 5-4-1, (kipa, walinzi watano, voungo wanne na mshambuliaji mmoja). Maana yake ni kwamba, kwenye walinzi watano walinzi watatu ni wa kati na wawili ni wa pembeni ambao kuna wakati wanacheza kama washambuliaji wa pembeni.

Viungo wanne ambao mmoja ni kiungo mkabaji, mmoja wa kushambulia na wawili wanakuwa viungo wa kati na msingi wake ni kuleta hali ngumu kwa wapinzani kufikia lango lao na mshambuliaji wa mwisho yeye anasubiri hiyo mipira ya counter attack ili kukimbia na kujaribu kuwadhuru wapinzani. Merrikh wanajilinda zaidi na wanakuacha ucheze mpira lakini wakipata mpira wanakimbia sana kufanya counter.

Gamondi mfumo wake ni 4-2-3-1, mabeki wanne, viungo wa kati wawili na viungo washambuliaji watatu. Kwa mfumo huu, anamiliki sana mpira, anashambulia muda wote na ana kasi sana lakini Merrikh wao ni kufyonza yale mashambulizi ya mpinzani, kuwashawishi waje kwao mpaka mabeki, halafu wao wawapige counter.

Yanga wanapomiliki mpira na njia zao hazifunguki hawachoki, ni wavumilivu, watauhamisha mpira kulia, kushoto, kati, nyuma, mbele halafu mpinzani anahangaika kuutafuta, mwisho wa siku mpinzani anachoka au analazimika kufanya makosa na baadae wanamuadhibu.

YANGA WAFANYE NINI? Gamondi ajiandae na uvumilivu kwa sababu wanakutana na timua ambayo sio tu inapaki basi, inapaki treni kabisa, pili waongeze kasi na pasi nyingi lakini wakienda kushambulia, wasiache mlango wazi.

Mabeki wahakikishe kwenye lango lao kuna usalama wasimwache kipa Djigui Diarra peke yake maana hawa jamaa ni wazee wa mbinu.

SOMA NA HII  ADAMA SALAMBA APATA SHAVU JS SOURA YA ALGERIA...MASHABIKI WA TIMU WAMPOKEA KWA MANENO MAZITO