Home Habari za michezo GAMONDI : MECHI HII NI NGUMU ILA ITAFAHAMIKA HUKO HUKO

GAMONDI : MECHI HII NI NGUMU ILA ITAFAHAMIKA HUKO HUKO

Habari za Yanga leo

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amekiri mechi ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh ya Sudan ni ngumu, lakini amesema watajuana huko huko kwani ana matumaini makubwa ya matokeo mazuri kutokana na maandalizi waliyofanya hadi sasa na bahati nzuri hana majeruhi kikosini.

Gamondi amefunguka hayo baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Kiluvya FC katika mechi ya kirafiki iliyopigwa juzi, akisema kuna mwanga amezidi kuupata kabla ya kuifuata Al Merrikh.

Alisema baada ya mechi mbili za ligi na kupata mapumziko kupisha mechi za timu za taifa kuwania fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 alitenga mazoezi ya aina tatu yaliyokamilika na kubaini kikosi chake kuwa na utayari wa mechi ya kimataifa kwa sasa.

“Maandalizi tuliyagawa katika sehemu kuu tatu, ya kwanza ni utimamu wa miili ya wachezaji, pili ni kumjua mpinzani na tatu ni mbinu gani za kutumia kumkabili,” alisema kocha huyo raia wa Argentina.

Alisema walianza mazoezi ya mchangani, gym wakafanya mazoezi ya kuchezea mpira uwanjani na kucheza mechi ya kirafiki na kupitia programu hizi amebaini utayari wa wachezaji wake huku akithibitisha kuwa hadi sasa hana majeruhi hata mmoja.

Alisema anajivunia kuwa na wachezaji ambao wanahitaji mchezo akiweka wazi kila mmoja amekuwa akitamani kucheza ndani ya kikosi hicho, hivyo anaamini kazi iliyobaki kwake ni kuwajenga kisaikolojia kuwa wanatakiwa kuuchukulia mchezo huo ni muhimu.

“Nina bahati kuwa na wachezaji ambao mbali na ubora walionao pia ni wazoefu wa michuano ya CAF, hilo halina shaka kubwa ni namna wanavyoutamani mchezo wa Al Merrikh. Tayari nimetoa maelekezo kwa wachezaji wote kuhusu mambo ya kufanya ndani ya uwanja, hivyo kazi imebaki kwao kwenda kupambana ili washinde ugenini,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Al Merrikh sio wepesi na hatujaichukulia kwa udogo tunajua tunaenda kushindana na timu ambayo pia inahitaji nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo, nasi pia tunaenda kushindana ili kuweza kufikia lengo, ndio maana nasema tutajuana huko huko kabla ya kurudiana hapa nyumbani.”

Yanga itavaana na Al Merrikh Jumamosi hii Uwanja wa Kigali Pele (zamani Nyamirambo) ikiwa ni mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kurudiana wiki ijayo jijini Dar es Salaam na mshindi wa jumla atatinga makundi, hatua ambayo Yanga ilishiriki mara ya mwisho 1998.

SOMA NA HII  MSHAMBULIAJI WA YANGA ATUA AL NASSAR YA RONALDO