Home Habari za michezo KWA HILI GAMONDI AMPE HEKO KAZE

KWA HILI GAMONDI AMPE HEKO KAZE

Ilikuwa mechi nzuri ya Ligi Kuu ya NBC, Yanga dhidi ya Namungo huku Yanga akishinda mchezo wa tatu mfululizo na kushinda mechi zote na kufikisha alama 9 na mabao 11. Hii wameonesha ufanisi wa asilimia 100.

Kitu kingine ambacho Yanga wamenufaika nacho dhidi ya Namungo ya Kocha Cedrick Kaze ni masuala ya kimbinu. Ni kujiandaa juu ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika endapo watafanikiwa kushinda tena mbele ya Al-Merrick na kutinga hatua ya makundi ambako Yanga wametanguliza mguu moja.

Mechi ya Namungo itakuwa imewaimarisha zaidi Yanga wakikutana na timu yenye staili ya uchezaji wa aina hii. Kwenye michauno ya CAF ngazi ya klabu, timu nyingi kubwa zinacheza kimbinu sana, wanakuachia mpira ucheze halafu wanakushtukiza na kukudhuru. Wanaweza kukudhuru hata kwa mipira ya kutenga.

Yanga wakitoboa Makundi na kukutana na timu kama ES Tunis, Wydad Casablanca, Al-Ahly au CR Belouzidad maana yake huenda wakakutana na staili kama ya Namungo chini ya Kaze anayeijua sana Yanga, timu ambayo inacheza mpira wa malengo (objective football) wa kupata matokeo wala sio wa kuvutia.

Namungo chini ya Kaze ni kama walipanga 5-5-0, (mabeki watano na viungo watano kiasili) kutokana na aina ya wachezaji waliopangwa ingawa wakati wanashambulia kule mbele walikuwa wanakwenda Pius Buswita na Jacob Masawe. Pembeni walitegemea mabeki wao Hashim Manyanya na Emmanuel Charles.

Muda mwingi walikuwa wakizuia kwa low block, wanawaacha Yanga waje na mashambulizi yao kisha wawazuie na kushambuia kwa kushtukiza. Ni mchezo wa kimbinu sana.

Kaze akiwa Yanga na Nabi walikuwa wakipanga 4-2-3-1, wakimiliki zaidi mpira na kupita kwenye njia. Yanga ikawa tishio. Gamondi hajabadili sana, ametumia mfumo huo huo akaongeza kasi na kukaba kwa haraka sana na kupora mpira.

Gamondi alipanga 4-2-3-1 akiweka watu wenye kwenye eneo la mwisho la ushambuliaji, Kaze walihakikisha wanameza hayo mashambulizi yasimfikie kipa wao Deo Munishi Dida. Yanga walisubiri mpaka dakika ya 88 kupata bao kupitia kwa Mudathir Yahya baada ya kazi nzuri ya kitimu.

Uchezaji huu wa Namungo, Yanga watakutana nao kwenye makundi ya CAFCL au hatua za mbele zaidi. Msimu uliopita Yanga alikuta na kitu kama hiki kwa US Monastri. Yanga akiwa ugenini alitawala mpira kipindi chote lakini akafungwa bao 2-0.

Aina ya uchezaji ule ndiyo imejaa kwenye CAFCL unapokutana na wakubwa wakubwa, labda ukutane na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, wao huwa wanacheza mpira mwingi, pasi nyingi, visigino. Lakini Ahly, Wydad na nyingine, si mar azote wanamiliki mpira, wanacheza kimbinu zaidi.

Msimu wa 2020/21, Simba walicheza robo fainali ya CAFCL dhidi ya kaizer Chiefs kule nchini Afrika Kusini, Simba walimiliki soka kwa asilimia 66, walipiga pasi 597 dhidi ya pasi 303 za wenyeji wao, lakini Simba wakafungwa bao 4-0. Mechi ya marudiano Simba walishinda 3-0, lakini haikusaidia kwa sababu Kaizer walikuwa mtaji wa mabao mengi waliofunga nyumbani kwao.

Kwa hiyo yanga wamepata kipimo sahihi pindi watakapotinga hatua ya makundi ya CAFCL. Wamshukuru Kaze katika hili, amewapa aina haswa ya uchezaji katika michuano hiyo ya CAF. Kaze amewapa zawadi, amewapa bonge la mechi la kimbinu mpaka wakasubiri mpango kazi wa sub za gamondi kufanya kazi.

SOMA NA HII  RAIS SAMIA ATIA NENO KIPIGO CHA SIMBA JANA....WENYEWE WAKIRI KUZIDIWA...