Home Habari za michezo YANGA YAANZA NA HESABU HIZI KALI CAF

YANGA YAANZA NA HESABU HIZI KALI CAF

Yanga vs Namungo

Kikosi cha Young Africans kimerudi uwanjani kujifua baada ya kutoka kucheza mchezo mgumu wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo iliyoamua kucheza nusu uwanja ili kuzuia isipigwe tano kama zilivyopigwa timu za KMC na JKT Tanzania, huku kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi akibadili gia.

Young Africans ilipata ushindi wa tatu mfululizo wa Ligi Kuu, katika mchezo ambao ilishindwa kuonyesha makali yake yaliyozoeleka kutokana na mbinu waliyoingia nayo Namungo ya kupaki basi na kuchomoka kimkakati, japo ilikubali bao 1-0 la usiku sana.

Kutokana na hali hiyo, kocha Gamondi amefanya kikao na wachezaji na kuwapa akili mpya yenye lengo la kuchanga karata zao vizuri kabla ya mechi ya kimataifa ya marudiano dhidi ya Al Merrikh ya Sudan.

Amewaambia mastaa wake kwamba wanapaswa kufanya kazi kubwa kuanzia sasa mpaka wikiendi ijayo ili kulinda heshima yao na klabu.

Young Africans inasaka kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 25 kupita.

Young Africans iichapa Al Merrikh kwa mabao 2-0 katika pambano la kwanza la Raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika lililopigwa kwenye Uwanja wa Kigali Pele uliopo Nyamirambo, Rwanda na sasa inahitaji kuepuka kipigo kisichozidi bao 1-0 ili kutinga makundi, ikiwa imetoka kucheza mechi ngumu na Namungo.

Gamondi amesema ameona ni muhimu kukaa na wachezaji kuwaambia wasahau kila kitu juu ya mechi iliyopita na kuweka akili zao kimataifa na hata ikitokea kaja mwingine wa kupaki basi wajue jinsi ya kumkabili.

“Tumefanya mazoezi ya gym kuweka mili kwenye utimamu baada ya mechi mbili ngumu jana tumerudi uwanjani kwa ajili ya mazoezi mepesi ya kujiweka timamu tayari kwa mapambano,” amesema Gamondi na kuongeza;

Timu ipo kwenye hali nzuri nimekaa na wachezaji kuongea nao mambo mengi ya msingi haswa kuhusiana na umuhimu wa mchezo huo wa kimataifa ili tuweze kutinga makundi kwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani,” amesema na kuongeza kuwa anahitaji kuona kila mchezaji anawajibika kuhakikisha anafanya majukumu yake kujenga heshima.

“Ni miaka mingi imepita timu hii haijapata nafasi ya kutinga hatua ya makundi kufanya vizuri itakuwa ni heshima kubwa kwa timu, Viongozi, wachezaji na benchi la ufundi kwa ujumla.

Pamoja na kupata matokeo tunahitaji kuwekeza juhudi zaidi huko kwani matokeo tuliyoyapata ugenini na wapinzani wetu wanaweza kuyapata wakija hapa hivyo umakini unahitajika.” amesema

SOMA NA HII  MO DEWJI AMTAKA MAYELE SIMBA...GSM ATOA KAULI YA KUTISHA AFRIKA