Home Habari za michezo UNAAMBIWA HIVI NDIVYO SIMBA ILIVYOICHAPA MANCHESTER UNITED 5-1 MWAKA 1982

UNAAMBIWA HIVI NDIVYO SIMBA ILIVYOICHAPA MANCHESTER UNITED 5-1 MWAKA 1982

Tetesi za Usajili Simba

Manchester R United iko kwenye majanga makubwa zaidi msimu huu. Katika mechi sita imepasuka michezo minne na kushinda miwili. Imechapwa tatu za Ligi Kuu England (EPL) na moja ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Juzi Burnley ilikuwa inaikaribisha Manchester United, nadhani matokeo unayo.

Tukiachana na hayo, hapa kuna taarifa ambayo itapata upinzani mkali kutoka kwa mashabiki wa soka, hususani wale wa Yanga na Manchester United.

Simba ya Dar es Salaam Julai 24, 1982 iliwahi kuifunga Manchester AF iliyotoka Uingereza.

KWANI STORI IKOJE?

Ulikuwa ni mchezo wa kirafiki uliochezwa katika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) ambao Simba iliutawala mwanzo mwisho na kuibuka na ushindi wa mabao 5-1.

Pamoja na kupata ushindi huo wa mabao mengi, lakini Simba ingeweza kufunga mabao mengi zaidi ila iliangushwa na safu ya ushambuliaji kutokuwa makini, kwani walipiga mipira mingi nje na mingine kuokolewa na kipa wa Man AF, Tonny Farrow aliyekuwa nyota wa mchezo kwa upande wa timu yake.

KIWANGO KIBOVU

Hata hivyo, Manchester ilionesha kiwango kibovu sana na ilipeleka mashambulizi ya hatari mara mbili tu langoni kwa Mnyama na kuambulia kona moja tu katika dakika zote 90.

Shambulizi lingine liliisaidia timu hiyo kupata penalti.

KASI YA MCHEZO

Simba ilianza kwa kulishambulia lango la wapinzani wao na kuanzia kwenye beki hadi kiungo timu ilikuwa vizuri sana, shida ilikuwa ni umaliziaji.

Simba ilikosa bao la wazi kupitia kwa mshambuliaji, Innocent Haule aliyepiga kwa kichwa pasi iliyotoka kwa Sunday Juma ‘Pikipiki’.

Dakika nne baadaye, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ alikosa bao la wazi baada ya kubaki na kipa Tonny na kuubutua mpira juu ya lango la wapinzani.

Dakika 14 ya mchezo, Mogella alipokea pasi nzuri kutoka kwa Mohamed Kajole, alijaribu kutaka kumfunga kipa wa Manchester kwa ujanja, lakini alishindwa. Mshambuliaji huyo baada ya kuipita ngome ya wapinzani alijaribu kutaka kumpiga kanzu kipa wa Manchester aliyekuwa na mbwembwe nyingi na kipa huyo akaudaka mpira uliokuwa unaelekea wavuni.

HAT TRICK HII HAPA

Abuu Juma (kaka yake na Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ a.k.a Bonga Bonga aliyekuwa Yanga) katika dakika ya 28 aliyechukua nafasi ya Mohamed Bakari ‘Tall’ aliyeumia alifunga bao baada ya kupokea pasi ya Mogella.

Hata baada ya kufungwa bao hilo, Manchester haikufanya juhudi zozote kusawazisha. Wachezaji waliokuwa nyota wa Manchester, Tonny, Fredy Erye na Kevin Booth walionekana kukata tamaa.

UBAO WASHANGAZA

Kocha wa Simba, Mbrazil Edil Silva aliwashangaza baadhi ya watazamaji na mashabiki alipoingia uwanjani akiwa na ubao maalumu wa kutolea maelekezo kwa wachezaji. Kitendo hicho kilikuwa cha kwanza kufanywa na kocha nchini na kuwa kivutio cha aina yake.

Simba iliingia kipindi cha pili na moto wa aina yake na kufanikiwa kupata bao dakika ya nane tu lililofungwa tena na Abuu Juma.

Dakika ya 10, Abuu Juma tena alifunga bao lake la tatu na kukamilisha hat trick baada ya kona iliyochongwa na beki Thobias Nkoma.

MTEMI ALIKUWEPO

Simba ikiwa inatumia mitindo ya Mshazari (Diagonal) na Samba kutoka kwa kocha huyo Mbrazili ilipata mabao mengine kupitia kwa Robert Masanja katika dakika 72 na 82 akipokea pasi kutoka kwa Nico Njohole na Mussa Kihwelo.

Kiungo wa Simba, Mtemi Ramadhani alisababisha penalti baada ya kumkwatua Kevin Booth na kufungwa na Fredy Erye.

MANCHESTER YAPIGA MTU 8-0

Kabla ya kutua nchini, timu hiyo ya Manchester AF ilitokea Mombasa, Kenya ambako iliipata kibonde wake na kuichakaza mabao 8-0.

Simba iliikodia ndege timu hiyo na kutua nchini asubuhi ya siku ya mechi na baada ya hapo ilirudi Kenya ambako ilikuwa na ratiba ya kucheza na mabingwa wa wakati huo wa Afrika Mashariki na Kati, AFC Leopards jijini Nairobi.

SIMBA YAITWA ENGLAND

Mara baada ya mchezo huo wa hapa nchini, kiongozi wa Manchester AF, Chris Davies aliishukuru Simba kwa makaribisho mazuri ambayo iliipa timu hiyo ndani ya siku tatu.

Davies alisema Simba ilikodi ndege maalumu kutoka Kenya na kurudi na katika kulipa shukrani hizo aliialika Simba kwenda Uingereza.

Kiongozi huyo aliitaka Simba kujilipia nauli ya ndege ya kwenda na kurudi hadi London, England na wao wangeigharamikia kila kitu ikiwa huko. Hata hivyo, safari hiyo ya Simba iliota mbaya, haijawahi kuripotiwa popote pale.

MWISHO WA UBISHI

Kuna wachezaji ambao wametajwa katika timu hii ya Simba ambao bado wako hai, kina Innocent Haule, Abuu Juma, Zamoyon Mogella, Sunday Juma na hata Mtemi Ramadhani waulizwe ili kumaliza ubishi ambao najua nimeuanzisha kuanzia leo.

SOMA NA HII  MORRISON:- SIWANASEMA NINA 'BUSHA'...? WAJIANDAE KUKEREKA ZAIDI..!!