Home Habari za michezo AUCHO APIGIWA SALUTI NA MWAMBA HUYU

AUCHO APIGIWA SALUTI NA MWAMBA HUYU

Habari za Yanga

Tanzania imebarikiwa kuwa na wachezaji wengi bora katika eneo la kiungo sio bara tu hadi visiwani Zanzibar ambako kwa hakika kumekuwa kukitoa wakali wengi wa eneo hilo wakiwamo kina Abdi Kassim ‘Babi’, Feisal Salum, Mudathir Yahaya na wengineo.

Licha ya ubora mkubwa wa mastaa wazawa kwenye nafasi ya kiungo bado kumekuwa na maingizo mengi ya wachezaji wa kigeni ambao wamekuja kuwaongezea ubora wazawa.

Yanga wana Khalid Aucho, Stephane Aziz Ki, Simba kuna Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute, Clatous Chama pale Azam FC wapo James Akaminko, Yanick Bangala wakati Singida Big Stars kuna Bruno Gomes, Marouf Tchakei na kadhalika. Hawa ni baadhi ya wachezaji wa kigeni wanaocheza eneo hilo na tayari wameonyesha ubora wao.

Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza na mzawa anayekipiga katika nafasi ya kiungo mkabaji wa Singida Big Stars, Aziz Andambwile akifunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumtaja Khalid Aucho kuwa ni kiungo anayerahisisha mambo uwanjani.

AUCHO KWELI DOKTA

Ni kiungo wa Yanga ambaye anaitumikia timu hiyo ya Jangawani kwa msimu wa tatu sasa baada miwili ya mwanzo kumalizika na kucheza kwa mafanikio makubwa akiiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo, Ngao ya Jamii mara mbili, Kombe la ASFC mara mbili na medali ya ushindi wa pili baada ya kucheza fainali Kombe la Shirikisho Afrika.

“Nimewaona viungo wengi wa kigeni na kupata nafasi ya kucheza nao timu moja na wengine kucheza dhidi yao, kati ya hao wote navutiwa na Aucho ni mchezaji mzuri anaufanya mpira uonekane rahisi uwanjani;

“Kiungo huyo ni mtu sana, anarahisisha sana mpira, anafanya majukumu yake kwa ufasaha uwanjani, nimekuwa nikimtazama na kujifunza mengi kwake, apewe tu maua yake,” anasema Andambwile ambaye amethibitisha kuvutiwa na Yaya Toure, kiungo wa zamani wa Man City na Barcelona ambaye kwa sasa ni kocha wa timu za vijana za Tottenham.

AITAJA YANGA

Wachezaji wana historia mbaya na nzuri uwanjani na kila mmoja anayo moja ya kumbukumbu ya furaha huku wengine ni za huzuni kama anavyothibitisha Andambwile.

“Katika maisha yangu ya soka nimecheza mechi nyingi ngumu na nzuri kutokana na aina ya matokeo tunayoyapata, lakini siwezi kusahau mechi dhidi ya Yanga msimu wa 2021/22 nikiwa Mbeya City;

“Tulicheza mechi ya ligi kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam ambao uliisha kwa suluhu, ulikuwa mchezo mgumu na mzuri, napenda kukiri kuwa ndio mchezo ambao ulinipa jina na kunifanya nizungumziwe sana,” anasema kiungo huyo ambaye pia aliutaja msimu huo huo wa 2021 alikaa nje ya uwanja kwa miezi sita bila kucheza.

MUDATHIR, KAGOMA

Soka lina aina nyingi ya kujifunza na kujitofautisha na wengine, kuna ambao hawawezi kumwaga sifa kwa wachezaji wenzao kutokana na kucheza nafasi moja na wengine wana moyo wa kuweka ukweli wazi kama ilivyo kwa Andambwile.

“Mudathir Yahya na Yusuph Kagoma ni wachezaji wazuri wote wana umuhimu wao kwenye kikosi kwa nyakati tofauti na wanaweza kucheza pamoja kutokana na kuwa bora kwa kushambulia na kukaba wana jicho la kuona pasi inatakiwa kwenda wapi;

“Kwenye kutofautisha siwezi kwasababu naona wote uchezaji wao upo sawa na wana ubora sawa ni miongoni mwa viungo wazawa ambao nawakubali na nimekuwa nikiwatazama,” anasema.

KUNA BRUNO HALAFU TCHAKEI

Msimu uliopita jina kubwa kwenye nafasi ya kiungo lilikuwa ni Mbrazil, Bruno Gomes na sasa Singida wameshusha kiungo mwingine fundi ambaye ameanza kuibua wadau kuweza kumzungumzia si mwingine ni Tchakei.

“Ujio wa Tchakei ndani ya Singida Big Stars umeongeza nguvu eneo la usambuliaji, ni mchezaji ambaye anatumia akili na nguvu katika maeneo sahihi, nafurahi kucheza naye timu moja;

“Lakini pia kuna Bruno huyu kila mmoja anafahamu ubora wake kwasababu kacheza msimu mmoja sasa ni msimu wa pili, kuhusu kuwatofautisha ni mapema sana, lakini ningekuwa kocha ningewatumia wote mmoja, atokee pembeni kama winga na mwingine apitie kati, timu lazima izalishe mabao mengi,” anasema Andambwile.

SINGIDA NI MAPEMA SANA

Andambwile msimu uliopita amekiri kucheza mechi 24 hivyo haoni sababu ya watu kuanza kumzungumzia kuwa hana namba ndani ya kikosi hicho ambacho hadi sasa kimecheza mechi tatu za ligi.

“Ni mapema sana kukubali kuwa kuna changamoto ya namba kikosi cha kwanza kwa mechi tatu tulizocheza ambazo zote sijapata nafasi, hilo halinipi shida naamini bado nina nafasi nitacheza;

“Msimu uliopita nimecheza mechi 24 kwanini nijikatie tamaa mapema yote hii, nitacheza, naamini kocha atanipa nafasi, hii ni kutokana na namna ambavyo najipambania kwenye uwanja wa mazoezi kuhakikisha napata nafasi ya kucheza,” anasema.

SIRI YA PENALTI

Sio wachezaji wote wana uwezo wa kupiga penalti, kuna wanaofunga kwa asilimia kubwa na wengine wamekuwa wakibahatisha lakini wanafunga, Andambwile ametaja sifa za kupiga penalti bora.

“Kwanza unahitajika kuwa na utulivu na kumsoma kipa wapi anakwenda kwasababu ukikaa kwa kutulia na kumuangalia unajua kabisa anakwenda wapi hiyo ndio siri ya ubora wa upigaji wa penalti,” anasema kiungo huyo ambaye amekiri kama sio soka ndoto yake ilikuwa ni kuwa daktari.

KIPA HADI KIUNGO

Sio kila mchezaji anaweza kucheza nafasi zote japo aina ya wachezaji kama hao wapo na kuna wengine mbali na kuwa mafundi kwenye nafasi wanazocheza wamebadilishwa namba na makocha.

“Nilikuwa golikipa na nilikuwa mzuri sana eneo hilo kutokana na urefu wangu, lakini nikabadilika;

“Naweza kucheza namba nane na mkabaji, ni nafasi ambazo nafurahia kucheza hakuna kocha aliyenibadili nafasi ni mimi mwenyewe nilikuwa nasogea nafasi na kujikuta nikicheza nafasi hii ninayocheza sasa,” anasema.

SOMA NA HII  NGAO YA JAMII KUONYESHA MBIVU NA MBICHI, SIO SIMBA SIO YANGA...... ISHU IKO HIVI