Home Habari za michezo KWA USALAMA WAKO…IKIFIKA DK YA 80 UKICHEZA NA YANGA HII YA GAMONDI...

KWA USALAMA WAKO…IKIFIKA DK YA 80 UKICHEZA NA YANGA HII YA GAMONDI AMUA KUPAKI BASI TU..

Habari za Yanga SC

HAKUNA utata kwamba kila mmoja kwa sasa anasifia soka la kikosi cha Yanga kinachonolewa na kocha Miguel Gamondi baada ya kucheza mechi sita za mashindano.

Katika mechi hizo sita za mashindano Yanga imecheza michezo miwili ya Ngao ya Jamii, miwili ya Ligi Kuu Bara na miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kati ya yote hiyo, timu hiyo haijapoteza mchezo wowote ndani ya dakika tisini, ukiacha ule dhidi ya Simba ambao walipoteza kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya dakika tisini kumalizika kwa 0-0, wakiwa wamefungwa bao moja tu.

Katika mechi hizo, Yanga imefunga mabao 19, lakini mbinu za Gamondi zikionekana kuwa matata sana kipindi cha pili ambacho imefunga mabao 15, huku manne tu ikifunga kipindi cha kwanza, lakini ni dhahiri kusema ukifika dakika 80 toa timu uwanjani, kwani kuanzia dakika hiyo hadi ya 90, Yanga imefunga mabao matano.

Yanga iliifunga Azam 2-0 katika Ngao ya Jamii ikipata mabao yake katika dakika ya 84 (Aziz Ki) na dk88 (Clement Mzize), na ikaifunga KMC 5-0 huku bao moja likifungwa dakika ya 81, kisha ikaipasua ASAS 5-1 huku bao moja likifungwa dakika ya 90 na kuichakaza JKT 5-0, bao mojawapo likifungwa dakika ya JKT dakika ya 88.

Kwenye Ligi, Yanga ilifungua pazia dhidi ya KMC na bao la kwanza lilifungwa dk17 na beki Dickson Job.

Mabao mengine yote yalifungwa kipindi cha pili, Aziz Ki dk59, Konkoni dk70, Mudathir Yahya dk76 na Pacome dk81.

Mchezo wa marudiano wa kimataifa dhidi ya ASAS, Yanga ilishida 5-1, bao la kwanza likifungwa dakika ya nane na Maxi Nzengeli huku mabao mengine yakifungwa na Konkoni dk45, Pacome dk55, Mzize dk69 na Maxi tena dk90+.

Katika ushindi wa 5-0 dhidi ya JKT, bao la kwanza lilifungwa na Aziz Ki dk45+ (50), huku mabao mengine yakifungwa na Musonda dk55, Yao Attohoula dk64, Maxi dk79 na 88.

Hii inaonyesha kuwa Gamondi mbinu zake amezificha kipindi cha pili, kwani timu yake kila inapotoka mapumziko huja na kasi ya hali ya juu, lakini jambo jingine la kustua ni kwamba kwenye michezo yote ambayo Yanga imeshinda, imepata bao kipindi cha kwanza.

Hali hii inaonekana kufanana kidogo na mfumo wa kocha aliyepita, Nassredine Nabi ambaye yeye timu yake ilikuwa inaamka na kupata mabao mengi baada ya kufanya mabadiliko ya wachezaji wanapotoka mapumziko.

Yanga imeanza vyema kwani wachezaji wake wengi waliosajiliwa msimu huu kutoka wameshafunga mabao, isipokuwa Fred ambaye hajapata nafasi ya kucheza na Skudu Makudubela ambaye alipata majeraha mwanzoni mwa msimu.

WENYEWE WAFUNGUKA

Katika mahojiano baada ya mchezo dhidi ya JKT Tanzania, Gamondi alikaririwa na gazeti hili akisema anataka kikosi chake kicheze kwa spidi na kufunga mabao mengi inavyowezekana.

“Nataka wachezaji wangu waweze kucheza kwa dakika zote uwanjani na kuwalazimisha wapinzani kwa spidi ili tupate mabao, bado naendelea kukitengeneza kikosi changu,” alisema Gamondi.

Kauli hiyo ni kama iliungwa mkono na kiungo Khalid Aucho ambaye alizungumza baada ya mchezo huo kumalizika akiweka wazi kocha wao amewapa uhuru wa kucheza.

“Kocha ametupa uhuru wa kucheza na pia kuutembeza mpira kwa kasi ambayo itawachosha wapinzani wetu na sisi ndio tutafanya vizuri,” alisema kiungo huyo raia wa Uganda.

SOMA NA HII  MPANGO WA SIMBA KUWASHUSHA AL AHLY BONGO UKO NAMNA HII...MANGUNGU AFUNGUKA A-Z