Home Habari za michezo ISHU YA SIMBA KUACHANA NA ROBERTINHO, UONGOZI WAFUNGUKA HAYA

ISHU YA SIMBA KUACHANA NA ROBERTINHO, UONGOZI WAFUNGUKA HAYA

Habari za Simba

Klabu ya Simba imesema kuwa haijafikiria kuachana na kocha wake mkuu, Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo, ‘Robertinho’ raia wa Brazil kwani amefanya kazi nzuri na timu haijatoka kwenye malengo yake.

Taarifa zilianza kusambaa jana kuwa Kocha huyo amepewa mechi moja ya marudiano dhidi ya Power Dynamos na endapo atashindwa kupata matokeo chanya basi atapewa mkonio wa kwa heri.

Hii inakuja baada ya ya kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia na kutoa sare ya bao 2-2 huku baadhi ya mashabiki wakidai kuwa kiwango kinachooneshwa na kikosi cha Simba sio bora hivyo huenda kocha amekosa mbinu za kukifanya kikosi chake kuwa tishio.

“Tunaridhishwa zaidi na matokeo ambayo tunayapata kwa sababu tunashinda, na kama sio kushinda basi ni sare kama tulivyopata na Power Dynamos. Tangu msimu huu umeanza hatujapoteza mchezo hata mmoja, tumeshinda michezo yote na kuvuna alama tatu ama kusonga mbele.

“Kiujumla mpaka sasa tuko sehemu salama ya kufurahishwa na matokeo huku taratibu Kocha Robertinho akiendelea kuitengeneza timu ambayo itatupa kitu ambacho roho yetu Wanasimba inataka.

“Kile kitu ambacho wanasimba wanakitaka bado hatujapata, ile biriani haijafikia, bado tupo kwenye pilau tunaelekea kwenye nchi ya ahadi. Lakini kwenye upande wa matokeo tunamshukur Mungu tunapata matokeo mazuri na tunalipongeza bencho la ufundi, tunawapa muda waendelee kuitengeneza Simba tishio zaidi.

“Mpaka sasa tupo sehemu salama sana, kama una kocha anakuhakikishia kushinda mchezo wowote unaocheza, maana yake ni kocha wa kumshika, anafanya kazi nzuri. “Mpaka sasa bado hatujapoteza njia, lengo lilikuwa ni kuchukua Ngao ya jamii tumechukua, lengo ni kushinda kila mchezo tumeshinda, lengo ni kwenda Makundi Afrika tumetanguliza mguu mmoja ndani, mpaka sasa tupo kwenye malengo yetu,” amesema Ahmed Ally.

SOMA NA HII  CHILUNDA APEWA MTIHANI HUU NA UONGOZI WA SIMBA