Home Habari za michezo ROBERTINHO AWEKA WAZI SILAHA DHIDI YA AL AHLY

ROBERTINHO AWEKA WAZI SILAHA DHIDI YA AL AHLY

Habari za Simba

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ametamba kuwa uzoefu na ubora wa beki wake wa kati, Che Fondoh Malone utakuwa silaha muhimu kwa safu yake ya ulinzi katika mchezo wa ufunguzi wa mashindano ya African Football League (AFL) dhidi ya Al Ahly, Oktoba 20 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Malone aliyesajiliwa na Simba akitokea Coton Sports ya Cameroon, amecheza mechi zote tisa za Simba katika mashindano tofauti msimu huu ambazo timu hiyo imeruhusu mabao saba huku ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja, ikishinda saba na kutoka sare mbili.

Robertinho alisema uwepo wa Malone una maana kubwa kwa safu yake ya ulinzi katika mechi hiyo dhidi ya Al Ahly ambayo wanajipanga kuhakikisha wanapata ushindi wa kishindo ili wajiweke katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya kwanza.

“Che Malone ni beki bora lakini ameshawahi kucheza na Al Ahly hivyo asilimia za kushinda na kuweka heshima katika mchezo huo muhimu ni kubwa akiunganika na Shomari Kapombe,Luis Miqusone,Hussein Shabalala na wengine.

“Safu ya ulinzi ni eneo ambalo kama halitakuwa sawa kuna uwezekano wa mchezo kuharibika ndio maana nguvu kubwa kwa sasa nimewekeza huko ili kumfanya mpinzani ashindwe kutumaliza,” alisema kocha Robertinho.

Kocha huyo alisema kuwa tofauti na mechi nyingi ambazo wameonekana kufanya makosa katika safu ya ulinzi ambayo yamewapa faida wapinzani wao kwa kupata mabao, anaamini mechi dhidi ya Ahly itaonyesha uimara mkubwa katika ukuta wake kutokana na maandalizi wanayoendelea kuyafanya.

Huu ni mchezo wa kuonyesha uimara wetu na hilo sina shaka nalo kutokana na maandalizi ambayo tunayafanya katika uwanja wa mazoezi. Al Ahly ni timu bora na ngumu hivyo na sisi tunatakiwa kuwa imara katika kila eneo na hilo nawaahidi mashabiki wetu.

“Hii ni mechi kubwa na ya kihistoria ambayo kama tukipata ushindi, itakuwa na maana kubwa kwa timu na kila mmoja wetu,” alisema Robertinho.

Katika hatua nyingine, Robertinho ameonyesha kufurahishwa na urejeo wa nyota wake wawili, Enock Inonga na Aishi Manula ambao walikuwa majeruhi, akidai wataongeza kitu katika kikosi chake kutokana na ubora wao.

Manula alikaa nje kwa muda mrefu akiuguza maumivu ya nyama za paja wakati Inonga alikosa mechi tatu zilizopita za Simba kutokana na majeraha ya ugoko.

SOMA NA HII  KAMA WEWE NI BODABODA...HILI JIPYA KUTOKA MERIDIANBET LINAKUHUSU...