Home Habari za michezo KISA AL AHLY….SIMBA NA YANGA KUUNGANA KWA MUDA…CAF WATOA BARAKA ZAO…

KISA AL AHLY….SIMBA NA YANGA KUUNGANA KWA MUDA…CAF WATOA BARAKA ZAO…

Yanga SC na Simba SC

Hii inaweza kuwa mara ya kwanza kushuhudiwa miamba ya soka la Bara, Simba na Yanga ikiungana kwenye oparesheni mbili tofauti dhidi ya mpinzani mmoja ambaye Mnyama atakutana naye kwenye michuano mipya ya African Football League, huku upande wa Wananchi ikiwa ni kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa miaka mingi Simba na Yanga zimekuwa zikiombeana njaa kwenye michuano mbalimbali ya kimataifa, lakini safari hii ni wazi kuwa zitaungana ili kuwa na namna bora ya kukabiliana na Al Ahly ambayo itakuja nchini mara mbili tofauti kucheza dhidi ya watani hao wa jadi.

Safari ya kwanza ya Al Ahly ambayo inashikilia rekodi ya kutwaa Ligi ya Mabingwa Afrika mara nyingi zaidi (11), itakuwa Oktoba 20 ambapo itacheza dhidi ya Simba kwenye michuani hiyo mipya ambayo itafanyika kwa mara ya kwanza huku mchezo huo ukiwa wa ufunguzi.

Wakati Simba ikiwa kwenye hesabu za kuendeleza rekodi nzuri iliyonayo ikiwa nyumbani dhidi ya vigogo hao, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi na benchi lake la ufundi watakuwa bize wakitazama ubora na udhaifu Al Ahly ili kuwa nyenzo muhimu kwao wakati wa kujiandaa kukabiliana nao kwenye Ligi ya Mabingwa.

Kutoka Oktoba 20 hadi kati ya Desemba Mosi na 2, ambapo Yanga itatupa karata yake ya pili kwenye Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Ahly, Gamondi atakuwa na mwezi mmoja na siku 13 kujiandaa na mchezo huo.

Tayari Simba ambayo inanolewa na Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ imepanga programu zake kabambe katika wiki hizi mbili za mapumziko ya michezo ya kimataifa ili kuhakikisha inafanya vizuri.

“Tumekuwa tukiweka nguvu kwenye mchezo mmoja baada ya mwingine. Tutaendelea na maandalizi huku tukisubiri wachezaji wetu wengine warejee kutokana katika majukumu ya timu za taifa,” alisema Robertinho ambaye ameiongoza Simba kwenye michezo 16 ya ligi bila kupoteza tangu alipotua nchini.

Akizungumzia ushiriki wao katika Ligi ya Mabingwa, Gamondi alisema: “Nimeona kundi (lao) lakini kabla ya kukutana na timu hizo tuna kibarua kigumu cha kutafuta pointi kwenye ligi ya nyumbani dhidi ya Azam FC. Kundi gumu ukiangalia timu zote ni bora kwa sababu ya kuzifahamu, kasoro Medeama sijaijua vizuri.”

Kabla ya kukutana na Al Ahly katika mchezo wa pili kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, Yanga itaanzia Algeria kucheza dhidi ya CR Belouizdad. Simba baada ya kumalizana na Al Ahly, kwenye Ligi ya Mabingwa wataanzia nyumbani kati ya Novemba 24 hadi 25 kucheza dhidi ya Asec Mimosas.

SOMA NA HII  HII INAITWA KIMYA KIMYA...TARATIIBUU...AZAM NAO WAJIINGIZA KWENYE MAISHA YA SIMBA NA YANGA...

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here