Home Habari za michezo SIMBA YAANGUKIA KWENYE MTEGO HUU WA FIFA

SIMBA YAANGUKIA KWENYE MTEGO HUU WA FIFA

FT: TZ PRISONS 1-3 SIMBA SC

Wakati Simba ikiendelea kujiandaa na mechi ya ufunguzi wa michuano mipya ya African Football League (AFL) dhidi ya Al Alhy ya Misri, ghafla imejikuta ikianguka kwenye mtego kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kutokana na ratiba ya mechi za timu za taifa ilivyo.

Hivi sasa ligi nyingi ikiwemo ya Tanzania zimesimama huku mastaa wengi wakiitwa kuzitumikia timu zao za taifa katika mechi za kirafiki na zile za kuwania kufuzu michuano mbalimbali ambazo zipo kwenye kalenda ya FIFA jambo lililotikisa kidogo kikosi cha Simba inayojiandaa kuivaa Al Ahly Oktoba 20, mwaka huu uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya AFL.

Hadi sasa mastaa wa Simba watano kutoka kikosi cha kwanza, hawapo kambini Msimbazi wakiwa kwenye timu zao za taifa ambapo beki Henock Inonga, yupo nchini New Zealand na kikosi cha DR Congo, kiungo Clatous Chama yupo Misri na Zambia na Kibu Denis, Mzamiru Yassin na Ally Salim walioitwa Taifa Stars watapaa kesho kwenda nchini Saudi Arabia.

Inonga amekuwa sehemu ya kikosi cha DR Congo mechi ya kirafiki na New Zealand ugenini lakini pia timu yake hiyo itakuwa na mchezo mwingine nchini Angola dhidi ya timu ya taifa hilo, Oktoba 17, siku tatu kabla ya Simba kuvaana na Ahly.

Hali iko hivyo hivyo kwa Chama aliye nchini Misri na timu yake ya taifa la Zambia baada ya mechi ya jana ya kirafiki, na timu hiyo itacheza tena nchini Zambia Oktoba 17, dhidi ya Uganda, siku tatu kabla ya Simba kuivaa Ahly.

Pia Kibu, Mzamiru na Ally walio taifa Stars, watacheza mechi ya kirafiki na Sudan mchezo utakaopigwa nchini Saudi Arabia Oktoba 15 na baada ya hapo timu hiyo itarejea nchini.

Kwa maana hiyo huenda mastaa hao watano ambao ni muhimili wa Simba wakaingia kambini kwa Wanamsimbazi hao, siku moja au mbili kabla ya mechi kutokana na safari za kutoka walipo kuja Dar es Salaam zitakavyokuwa.

Hata hivyo uongozi wa Simba umeyaomba mashirikisho ya soka nchini wanakotoka wachezaji hao, kuwaparuhusu kujiunga na klabu zao lakini bado hawajajibiwa.

“Tunamazungumzo na mashirikisho ambayo wachezaji wetu wameitwa kwenye timu zao za taifa. Tumeomba wawape muda waweze kurudi kambini mapema kujumuika na wenzao ili kujiandaa na mechi ya Ahly lakini hadi sasa, tulikuwa hatujapata jibu la jumla,” alisema Ahmed Ally, Ofisa Habari wa Simba.

Wakati huo huo, mpinzani wa Simba, Al Ahly aliomba na kuruhusiwa kubaki na wachezaji wake muhimu walioitwa kwenye timu zao za taifa ikiwemo kiungo Mmali, Aliou Dieng na mshambuliaji kutoka Afrika Kusini Percy Tau, na wote wapo kambini wajiweka tayari kuivaa Simba.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Mbrazili, Roberto Oliveira alisema alitamani kuwa na wachezaji wake wote kwenye maandalizi haya lakini kwakuwa kuna walioenda kwenye timu zao za taifa basi atatumia waliopo.

“Nilitaka tuwe wote na kufanya maandalizi ya pamoja, lakini ndio imekuwa hivyo. Bado naamini katika kikosi chetu, tutaendelea kujiandaa kupitia wachezaji tulionoa kambini,” alisema Robertinho ambaye msimu huu ameiongoza Simba kwenye mechi tisa za mashindano, akishinda saba na kutoa sare mbili.

Ikumbukwe baada ya mechi ya kwa Mkapa kati ya Simba na Al Ahly, timu hizo zitarudiana tena Oktoba 24 jijini Cairo Misri, na mshindi wa jumla atasonga hatua ya nusu fainali huku atakayepoteza ataaga mashindano.

Huu ni msimu wa kwanza wa michuano hiyo na imehusisha timu nane tu ambazo ni Simba, Al Ahly, Petro de Luanda ya Angola, TP Mazembe (DR Congo), Enyimba (Nigeria), Wydad AC (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) na Esperande de Tunis ya Tunisia.

SOMA NA HII  KALENDA YA FIFA NA MABADILIKO YA MTIBWA SUGAR ...... KATWILA AAMUA KUFANYA KWELI