Home Habari za michezo KISA MABEKI WA SIMBA BENCHI LA UFUNDI LATOA TAMKO….. ROBERTINHO NAE AIBUKA

KISA MABEKI WA SIMBA BENCHI LA UFUNDI LATOA TAMKO….. ROBERTINHO NAE AIBUKA

Habari za Simba

Simba juzi Jumamosi ilishinda mechi ya sita mfululizo kwenye Ligi Kuu msimu huu na sasa imerudi chimbo kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya watani wa jadi Yanga utakaochezwa Novemba 5, mwaka huu, Uwanja wa Mkapa lakini benchi la ufundi la Wekundu wa Msimbazi hao limekiri kuwa na kazi ya ziada kurekebisha safu ya ulinzi.

Pamoja na kuwa Simba haijapoteza mechi zote 12 za mashindano msimu huu, lakini safu yake ya ulinzi imeonekana kuwa na makosa mengi ya kiufundi ikifungwa jumla ya mabao 11, ikiwa ni karibu wastani wa bao moja kwa kila mechi jambo ambalo sio salama kwao.

Katika Ligi Kuu, Simba imeruhusu mabao sita, matatu kwenye Ligi ya Mabingwa na matatu katika michuano mipya ya African Football League.

Katika mechi zote hizo, muda ambao timu inaruhusu mabao hayo ukuta wa Simba umekuwa ukiundwa na wachezaji saba ambao ni mabeki watano, Henock Inonga, Che Malone, Kennedy Juma, Mohamed Hussein, Shomari Kapombe na makipa Ally Salim na Ayoub Lakred.

Kocha mkuu wa Simba, Roberto Oliveira alikiri ni makosa yanayojirudia lakini anaendelea kuyafanyia kazi kwa kuongea na kuwaelekeza wachezaji wake namna ya kuyapunguza.

“Ni kweli tumekuwa tukiruhusu mabao, jambo ambalo hatulifurahii na siyo zuri kwetu.

Kila siku mazoezini tumekuwa tukilifanyia kazi lakini linajirudia. Kwa sasa tuna muda kidogo kabla ya mechi ijayo, tutajitahidi kulifanyia kazi eneo hilo ili kuhakikisha makosa hayo yanapungua,” alisema Robertinho na kuongeza;

“Ni makosa madogo madogo wanafanya machezaji ila pamoja na kukosea huko, wamekuwa wakifanya kazi kubwa kuhakikisha tunakuwa salama, nadhani ni sio wakati wa kuwabeza kwani wana mazuri mengi kuliko mabaya.”

Beki wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, alisema kila timu inafungwa na kila mchezaji anafanya makosa hivyo kinachotakiwa ni kuangalia namna ya kuyapunguza tu.

“Mabeki wa Simba wote kila mmoja anasifa zake kwa hiyo kinachotakiwa ni kuwafanya waelewane zaidi katika upungufu na uimara wao ili kupunguza makosa,” alisema Julio.

Simba na Yanga zitakutana zikiwa na alama sawa (18), huku Yanga ikiongoza kwa tofauti ya mabao 16 kwa 11 ya Simba.

SOMA NA HII  TUNAMTAKA CHAMA YANGA..SENZO AFUNGUKA KILA KITU..SIMBA WASHIKILIA MPINI...