Home Azam FC MBUNGI YA AZAM vs YANGA KUPIGWA SIKU HII WIKI IJAYO

MBUNGI YA AZAM vs YANGA KUPIGWA SIKU HII WIKI IJAYO

Tetesi za Usajili Yanga

Mechi inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini la Yanga dhidi ya Azam FC iliyokuwa limepangwa kupigwa Jumatano ya Oktoba 25, imewahishwa mapema na sasa itapigwa Oktoba 22, baada ya Bodi ya Ligi (TPLB) kufanya mabadiliko ya mechi za raundi zijazo za Ligi Kuu Bara.

Katika mechi tano zilizopita tangu Azam iliposhinda bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara Mnano Aprili 25, 2021, Yanga imeshinda mechi nne, ikiwamo moja ya Ngao ya Jamii na tatu za Ligi Kuu.

Timu hizo zinazoendelea kujifua kwa mchezo huo zinafukuzana katika msimamo, Azam ikiwa ya pili, huku Yanga ikifuatia nyuma baada ya kila moja kucheza mechi tano na kwa siku za karibuni zimekuwa na upinzani mkali.

Kwa msimu huu zilishakutana kwenye Ngao ya Jamii na Yanga kushinda mabao 2-0, wakati kwa msimu uliopita Yanga ilishinda mechi ya marudiano kwa 3-2 wakati ile ya kwanza iliisha kwa sare ya 2-2.

Rekodi zinaonyesha Azam ilipata ushindi mbele ya Yanga mara ya mwisho Aprili 25, 2021 kwa bao la Prince Dube na mechi tano zilizofuata imeambua sare moja tu na kupoteza nne ikiwamo ya Ngao ya Jamii iliyopigwa Agosti 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, hivyo mechi hiyo ya kwanza ya ligi kwa msimu huu itakuwa na kibarua cha kutaka kulipa kisasi.

Mabadiliko ya ratiba yaliyotangazwa jana na TPLB, imefafanua sababu ya kufanya hivyo ni kutolewa kwa timu za Azam Fc na Singida Big Stars kwenye michuano ya kimataifa ya CAF, lakini pia ushiriki wa Simba kwenye African Football League sambamba na kutokuwepo kwa mechi za mchujo za Chan 2024.

Badiliko hilo limeigusa ‘Tamtamu Derby’ ya Mtibwa Sugar na Kagera Sugar iliyokuwa ipigwe Oktoba 23 na sasa itawahi mapema kwa kupigwa Alhamisi ya Oktoba 19, huku ile ya Namungo na Singida BS ikipangwa Oktoba 21, sambamba na ile ya Ihefu na Coastal Union, pamoja na Geita Gold na Dodoma Jiji.

Pambano la Derby la Maafande wa Tanzania Prisons na JKT Tanzania limepangwa kupigwa siku moja na lile la Yanga, yaani Oktoba 22, awali nalo lilikuwa lipigwe Oktoba 25, jijini Mbeya.

Mabadiliko hayo yamegusa pia mechi za raundi nyingine za mbele hasa zile za raundi ya saba ilizokuwa zipigwe kuanzia Oktoba 28-29 kwa kupangwa sasa kupigwa kati ya Oktoba 25-27, huku mechi za Simba dhidi ya Mashujaa na ile ya Ihefu zikiwa hazijapangiwa kutokana na Wekundu hao kuwa na jukumu la mechi za CAF kupitia michuano mipya ya African Football League (AFL) inayozinduliwa Oktoba 20 hapa nchini.

Simba imepangwa kuvaana na Al Ahly mechi itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, kisha siku nne yaani Oktoba 24 kusafiri kwenda Cairo kurudiana na wababe hao wa soka la Afrika na mshindi wa jumla atakata tiketi ya kutinga nusu fainali.

Simba ndio vinara wa Ligi Kuu kwa sasa ikiongoza na pointi 15 na mabao 14 ya kufunga na kufungwa manne, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13 na mabao 10 na mabao mawili ya kufungwa, kisha watetezi, Yanga ikifuatia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 12 na mabao 15 ya kufungwa na kufungwa mawili, huku kila timu ikiwa imecheza mechi tano kwa sasa.

SOMA NA HII  FEISAL SALUM LEO MKWAWANI KUNACHIMBIKA , YANGA WAJIPANGE