Home Habari za michezo SIMBA, YANGA WAPEWA MBINU HIZI CAFCL

SIMBA, YANGA WAPEWA MBINU HIZI CAFCL

Habari za michezo

Simba na Yanga zimepangwa na vigogo kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini nyota wa zamani wa timu hizo wamezipa ujanja ili zitoboe na kuvuka pamoja kwenda robo fainali.

Simba imepangwa Kundi B na mabingwa wa zamani Wydad Casablanca, Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy wakati Yanga imepewa watetezi wa sasa wa taji la michuano hiyo Al Ahly, CR Belouizdad na Medeama na kuonekana kuwa na mlima mzito kupenya hatua inayofuata.

Hata hivyo, wakongwe wa soka wamesema kama zitatumia vyema viwanja vya nyumbani ni rahisi kutoboa kuungana na vigogo walivyonavyo kundini, kwani soka la kisasa limebadilika na Tanzania imeonekana kuwa tishio hata kwa wapinzani tofauti na ilivyokuwa zamani ilipoonekana kuwa kibonde.

Dua Said, nyota wa zamani wa Simba, alisema Yanga ina nafasi ya kufanya vizuri kwani itarahisishiwa kazi kwa Al Ahly itakayokuja nchini mapema kucheza na Simba kwenye mechi za michuano ya African Football League (Super League).

Dua alisema ni muhimu timu zote zifanye maandalizi ya kutosha na kuutumia vyema uwanja wa nyumbani kukusanya pointi za kutosha, huku zikienda kukomaa ugenini japo ziambulie sare.

“Mashabiki wengi wanaona Simba ina afadhali kuliko Yanga, lakini wanasahau msimu uliopita vijana wa Jangwani walifika fainali za Kombe la Shirikisho hivyo wana uzoefu wa kutosha wa mechi ngumu,” alisema Dua aliyewahi kuwika pia na Mtibwa Sugar na Small Simba ya Zanzibar.

Nahodha wa zamani wa Yanga, Kenneth Mkapa alisema kuondoka kwa wachezaji ambao walifanya vizuri msimu uliopita Yanga hakuipunguzii chochote, kwani ina uwezo wa kufanya makubwa. “Lolote linaweza kutokea kinachotakiwa ni kumsoma mpinzani na kujiandaa kupambania timu kwani hiyo ni nafasi ya kujiuza kimataifa hizo ni mechi zinazotazamwa sana,” alisema Mkapa.

Kiungo wa kimataifa wa zamani wa Yanga, Pan Africans na Taifa Stars, Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema: “Zikicheza kwa utulivu na umakini hakuna timu ngumu kama wapinzani wakiingia katika mfumo tunaweza kuandika rekodi kubwa zaidi kuliko zilizowahi kuwekwa.”

SOMA NA HII  AHMED ALLY AWEKA WAZI ISHU YA KIMATIFA