Home Habari za michezo UJIO WA MANULA WAMPA WASIWASI MWARABU WA SIMBA

UJIO WA MANULA WAMPA WASIWASI MWARABU WA SIMBA

Tetesi za Usajili Simba

Mashabiki wa Simba kwa sasa angalau wana furaha baada ya kusikia kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula amerejea uwanjani na juzi kucheza kwa dakika 40 wakati ilipoifumua Dar City kwa mabao 5-1 kwenye mechi ya kirafiki, lakini ujio huo umekula kichwa cha kipa raia wa Morocco, Ayoub Lakred.

Kipa huyo aliyesajiliwa kutoka FAR Rabat akitoka kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Morocco (Botola Pro), ili kuziba nafasi ya Manula aliyekuwa majeruhi tangu Aprili mwaka huu, akichukua nafasi ya kipa Mbrazili, Jefferson Luis aliyesajiliwa na kuachwa na timu hiyo ilipokuwa kambini kwa pre season huko Uturuki.

Simba ililazimika kumlipa Mbrazili huyo Sh400 milioni kwa kuvunja mkataba huo, akiwa hata hajaanza kuitumikia timu hiyo.

Hata hivyo, Ayoub tangu atue kikosini, amecheza mechi tatu tu zikiwamo mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia zilizoishia kwa sare ya 2-2 ugenini Ndola na ile ya 1-1 waliporudiana Dar es Salaam na nyingine moja ya Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union, kabla ya kuwekwa benchi kumpisha Ally Salim.

Lakini ghafla baada ya Manula kurejea kikosini, taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema kipa wa Morocco ni kati ya wachezaji waliowekewa wino mwekundu wa kupigwa panga kwenye dirisha dogo litakalofunguliwa Desemba 16 hadi Januari 15 mwakani na tayari mwenyewe ameshajulishwa na mabosi wa klabu hiyo.

Inaelezwa mabosi wa Simba wamepanga kumfyeka Ayoub kwa kushindwa kuonyesha ubora licha ya kusajili kwa gharama kubwa akiwa pia ni kipa wa kigeni.

Ikumbukwe hadi sasa Simba ina makipa wanne ukiachana na Manula na Ayoub, pia kuna Ally Salim aliyedaka mechi nne za Ligi na Ngao ya Jamii pamoja na Hussein Abel ambaye hajadaka mechi hata moja tangu asajiliwe dakika za mwishoni kutoka KMC.

Habari za kuaminika kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Simba waliopo ndani ya Bodi ya Wakurugenzi, zinasema kuna mabadiliko yatafanyika katika kikosi hicho wakati wa dirisha dogo ingawa hayatakuwa makubwa sana.

“Ni jambo ambalo linajadiliwa hadi sasa ni Ayoub, lakini kwa asilimia kubwa ataondoka maana Manula amerudi, sio kipa mbaya sana, ila itakuwa vigumu kipa wa kigeni kukaa benchi halafu mzawa acheze, hivyo tunaona ni vyema tumalizane naye wakati wa dirisha dogo, mkataba wake ni wa mwaka mmoja,” alisema kigogo huyo (jina tunalo) na kuongeza;

“Hata yeye hawezi kukubali akae benchi bila kucheza, maana unapokuwa mchezaji wa kigeni hasa nafasi hii ya kipa basi ni lazima ucheze yaani umzidi uliyemkuta.”

Habari zaidi zinasema tayari kipa huyo ameshajulishwa juu ya hatma yake kikosini kwa sasa na anasubiri kipyenga cha dirisha dogo lifunguliwe apewe chake kwa muda uliosalia na mkataba ili asepe zake.

Pia katika maboresho hayo, inadaiwa Simba ipo kwenye mpango wa kusajili beki wa kati nafasi ambayo inachezwa na Henock Inonga, Kennedy Juma na Che Fondoh Malone pamoja na beki wa kushoto ambako anacheza Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Akizungumzia ishu ya kipa Ayoub, nyota wa zamani aliyeidakia timu hiyo pamoja na Yanga na Taifa Stars, Ivo Mapunda alisema hakukuwa na sababu ya kumsajili kipa wa kigeni na kama imekuwa hivyo alipaswa kuwa bora zaidi ya Manula.

“Sikuona sababu ya Simba kumsajili kipa wa kigeni, ujio wa Ayoub ulipaswa angekuwa na ubora zaidi wa Manula ambaye ni kipa namba moja wa Simba na Stars,” alisema Ivo aliyewahi kuzidakia pia Moto United, Tanzania Prisons, St George ya Ethiopia, Gor Mahia Kenya na Azam FC.

Kauli hiyo iliungwa mkono na kipa na kocha wa makipa wa zamani wa Simba, Idd Pazi “Father’ aliyeshauri Simba kuvunja mkataba na kipa huyo.

“Mimi nimecheza nje, ukiwa kipa wa kigeni basi ni lazima ucheze na si vinginevyo, kama Manula amerudi kuna sababu gani ya Ayoub kuendelea kuwepo Simba,” alisema Pazi aliyewahi kuwika na Pilsner, Majimaji na kucheza soka Sudan na Indonesia.

SOMA NA HII  ODDS ZA KUMALIZIA WEEKEND HIZI HAPA...HAKIKISHA MKEKA WAKO WA MERIDIANBET UNATEMA LEO...