Home Habari za michezo SIMBA vs YANGA NI KISASI NA HESHIMA VYOTE KATIKATI YAKE

SIMBA vs YANGA NI KISASI NA HESHIMA VYOTE KATIKATI YAKE

Habari za michezo

Leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa patachimbika, hii ni siku ambayo itakuwa mwisho wa ubishi, nyodo na tambo wakati miamba miwili ya soka nchini, Simba na Yanga itakapokutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Simba inashuka kwenye mchezo huo ikitoka kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu wakati Yanga ikiwa imetoka kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida Big Stars.

Ushindi huo umeongeza ugumu kwenye mtanange huo mkubwa wenye upekee na hadhi kubwa zaidi katika mchezo wa soka nchini.

Huu unakuwa mchezo wa kwanza kuzikutanisha timu hizo tangu Uwanja wa Benjamin Mkapa ulipofanyiwa marekebisho na serikali ambapo ulizinduliwa katika michuano ya Ligi ya Soka ya Afrika (AFL).

Uwanja wa Benjamin Mkapa ni miongoni mwa viwanja ambavyo vimeandaa michezo ya watani wa jadi, viwanja vingine ambavyo vimewahi kupata bahati hiyo nje ya Dar es Salaam ni CCM Kirumba na Nyamagana (Mwanza), Sheikh Amri Abeid Kaluta (Arusha),Jamhuri (Morogoro) na Amaan (Zanzibar), Jamhuri Dodoma na Sokoine Mbeya.

Timu hizo zitakutana kwenye mchezo huu huku kila upande ukiwa na morali kubwa na nyota ambao wana uwezo mkubwa wa kuamua mchezo, chini ya makocha Roberto Oliveira

‘Robertinho’ wa Simba na Miguel Gamondi wa Yanga ambaye moto wake umeanza kuonekana tangu alipotua hapa nchini.

Mechi hiyo inakuja ikiwa Simba na Yanga zote ziko juu ya msimamo wa Ligi Kuu Bara zikiwa na pointi 18 zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa. Miamba hii inakutana ikiwa ni kama miezi mitatu imepita tangu ikutane kwenye fainali ya Ngao ya Jamii Agosti 13, mwaka huu, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 3-1.

NI MECHI YA KISASI NAHESHIMA

Pamoja na heshima ya kutwaa taji, mechi hiyo ni fursa nzuri na muhimu kwa kila timu kulipa kisasi cha matokeo ya nyuma baina yao pindi walipokutana katika mashindano tofauti.

Yanga bila shaka watakuwa na kiu ya kulipa kisasi cha kufungwa kwa mikwaju ya penalti 3-1 na Simba kwenye Ngao ya Jamii mwaka huu baada ya timu hizo kutoka suluhu katika muda wa kawaida wa mchezo.

Lakini pia wana kisasi cha kufungwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili katika msimu wa 2022/23. Simba wenyewe kwa upande wao watakuwa na hamu ya kuendeleza rekodi yao ya ushindi kwa Yanga ambao katika michezo mitatu ya karibuni hawajapata ushindi dhidi yao.

MZANI UMEBALANSI

Takwimu za mechi sita zilizopita zinatoa taswira ya ugumu wa mechi hiyo ya kutafuta kinara wa Ligi Kuu Bara mtanange ambao utazikutanisha timu hizo mbili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Timu hizo zote kila moja imejikusanyia pointi 18 lakini Yanga ikiwa kinara wa Ligi Kuu kutokana na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa. Lakini pia Simba ina faida ya kuwa nyuma mchezo mmoja hivyo iwapo itashinda itaongeza wigo wa pointi zaidi mbele ya Yanga.

Simba imeshinda mechi zake sita zilizopita za Ligi Kuu Bara, dhidi ya Mtibwa Sugar, Singida Big Stars, Tanzania Prisons, Coastal Union, Dodoma Jiji na Ihefu.

Kwa upande wa Yanga ambao wamecheza mechi saba wakishinda sita na kupoteza mmoja,wameibuka na ushindi mbele ya Namungo, JKT Tanzania, KMC, Geita Gold, Azam FC, na Singida Big Stars huku ikipoteza mbele ya Ihefu.

NI MECHI YA GAMONDI NA OLIVEIRA

Huu unakuwa mchezo wa pili kwa makocha hawa kukutana, walianza kukutana kwenye Ngao ya Jamii ambapo Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 3-1.

Lakini hii inakuwa mara ya tatu kwa Oliveira kukutana na Yanga akiwa kwenye ardhi ya Tanzania ambapo ameshinda kwenye michezo yote miwili akishinda 2-0 kwenye Ligi Kuu Bara na Ngao ya Jamii.

Huu unakuwa mchezo wa kocha Gamondi, kujiuliza alipotezaje mchezo wa Ngao wa Jamii ambao ulikuwa wa kwanza kumtambulisha kwenye Ligi Kuu Bara lakini akaanza kinyonge sasa ni wakati wa kwenda kusawazisha makosa.

Ubora wa vikosi vyao unaenda kuongeza hamasa ya mchezo huu ambapo Yanga uwepo wa Stefane Aziz Ki mwenye mabao sita, Maxi Nzengeli mwenye mabao matano na Pacome Zouzoua aliyeingia wavuni mara tatu wanampa jeuri kocha Gamondi.

Wakati kwenye kikosi cha Simba uwepo wa Jean Baleke mwenye mabao sita, Moses Phiri aliyepachika wavuni mabao matatu ni miongoni mwa watu waawake naotarajia kuongoza mashambulizi ya wekundu wa Msimbazi kwenye dimba la Benjamin Mkapa.

NI VITA YA WAPIGA PASI ZA MWISHO

Vinara wa pasi za mabao wanaenda kuthibitisha ubora wao kwenye mchezo huu mkubwa ambao utaenda kutoa taswira nani anapaswa kuwa kileleni mwa msimamo.

Yao Kouassi ndio kinara wa kupiga pasi za mwisho kwenye Ligi Kuu Bara hadi sasa akiwa amepiga pasi nne kwenye mechi dhidi ya Singida Big Stars, Geita Gold, Namungo na JKT Tanzania.

Anayefuata kwa kutoa pasi nyingi za mabao ni Luis Miquissone ambaye licha ya kutopata nafasi ya kuanza mara nyingi lakini amekuwa na mwendelezo mzuri.

Miquissone, ametoa pasi zake kwenye michezo muhimu dhidi ya Ihefu na Singida Big Stars ambapo ameendelea kuwa imara kila siku anapopata nafasi.

SOMA NA HII  KIWANGOO! YANGA WAANDIKA REKODI....MUSONDA,MZIZE WAIUA AL MAREIKH