Home Habari za michezo GAMONDI AWATAJA MASTAA WAWILI YANGA

GAMONDI AWATAJA MASTAA WAWILI YANGA

Habari za Yanga

Nyota wa Yanga, Jesus Moloko na Clement Mzize wamemkosha kocha wao, Miguel Gamondi kwa kile walichokifanya kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, wakati Yanga ikishinda 1-0.

Moloko na Mzize ambao waliingia kipindi cha pili ndio walioifanya Yanga kushinda mchezo wa tano mfululizo na kuendelea kujikita kwenye kilele cha msimamo wa ligi huku wakiwa na pointi 24.

Gamondi ambaye mwezi ujao, Desemba Mosi atatimiza miaka 60 tangu azaliwe, alisema wachezaji hao walienda kufanya kile ambacho aliamini wanaweza kukifanya kiasi cha kuwapa nafasi baada ya kuwasoma wapinzani wao na anatumia nafasi hii kuwapongeza kwa kufuata maelekezo yake.

“Hizi ni pointi muhimu sana kwetu, tuliona namna ambavyo Coastal ilikuwa ikicheza na kuamua kufanya mabadiliko ambayo yamekuwa na matokeo chanya, ilibidi kuwaingiza Moloko na Mzize ili wakabadilishe hali ya mchezo,” alisema kocha huyo na kufafanua;

“Nadhani wote mmeona kile walichokifanya, nina furaha sana na uwajibikaji wa kila mchezaji kwenye kikosi changu, mechi ilikuwa ngumu hasa katika kuwafungua wapinzani wetu lakini jambo muhimu ni kwamba tumefanikisha kile ambacho tulikuwa tumekilenga na nichukue nafasi hii kuwapongeza wachezaji wote lakini hawa wawili walifanikisha kile ambacho niliwatuma uwanjani.”

Mabadiliko ya wachezaji hao ambao waliingia kuchukua nafasi ya Kennedy Musonda na Mudathir Yahya yaliibeba Yanga kwani Moloko ndiye aliyetoa pasi ya bao kwa Mzize katika dakika ya 71 zikiwa ni dakika chache tangu waingie uwanjani.

Kwa matokeo hayo, Yanga inafukuzia kile ilichofanya Simba kwenye michezo yake sita ya mwanzo kwa kushinda mfululizo kabla ya kupototeza kwenye dabi wikiendi iliyopita.

Mnyama alifanya hivyo kwa kuzifunga, Mtibwa Sugar (4-2), Dodoma Jiji (2-0), Coastal Union (3-0), Tanzania Prisons (3-1),Singida Big Stars (2-1) na Ihefu (2-1).

Baada ya kipigo dhidi ya Ihefu, Yanga imeshinda mechi tano mfululizo ambazo ni dhidi ya Geita Gold (3-0), Azam FC (3-2), Singida Big Stars (2-0), Simba (5-1) na Coastal Union kwa bao 1-0.

Mchezo ujao kwa Yanga kwenye ligi ni dhidi ya Mtibwa Sugar ambao utachezwa Desemba 16 akiwa nyumbani baada ya kucheza michezo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

AIVULIA KOFIA COASTAL

Katika hatua nyingine Kocha Gamondi ameukubali mziki kwa Coastal kwenye kujilinda huku akiwapongeza walikuwa bora kiasi cha kumfanya atumie njia mbadala ili kupata matokeo kwenye mchezo huo ambao ulitawaliwa na kadi za njano nane.

“Walikuwa makini katika kulinda, walitupa wakati mgumu hasa katika kipindi cha kwanza, ikatubidi kutafuta suluhu kipindi cha pili, Coastal wana timu nzuri,”alisema kocha huyo raia wa Argentina.

SOMA NA HII  HAWA HAPA WAKALI WATATU WAMEMTUNGUA MANULA NJE YA 18