Home Habari za michezo PAMOJA NA MATARAJIO MAKUBWA…CHILUNDA APEWA ‘MAKAVU LIVE’ SIMBA….

PAMOJA NA MATARAJIO MAKUBWA…CHILUNDA APEWA ‘MAKAVU LIVE’ SIMBA….

Mshambuliaji wa Simba, Shaaban Chilunda ana kazi ya kujitetea mwenyewe uwanjani, ili kuwaonyesha viongozi wa klabu hiyo hawakukosea kumsajili, kwani usajili wake uliwashitua mashabiki wengi.

Tangu aiunge na Simba amecheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons dakika moja na Namungo dakika 31, akiingia kuchukua nafasi ya Clatous Chama na kwenye mchezo huo alicheza kama winga.

Akimzungumia nyota huyo, staa wa zamani wa Simba, Mohamed Banka alisema mchezaji kusajiliwa na timu ni ishu moja na kucheza ni jambo ambalo mhusika anapaswa kulitetea mwenyewe uwanjani.

“Hakuna jambo rahisi kwenye kusaka maisha. Kitu ambacho anapaswa kukifanya Chilunda ni kujituma kwa bidii na kunoa kiwango chake. Mfano mzuri wakati anasajiliwa Meddie Kagere na Joash Onyango walisema ni wazee ila walijitetea wenyewe uwanjani,” alisema.

“Kuna ishu ya Moses Phiri mashabiki wanamtetea kwa sababu awali alionyesha kiwango kikubwa na akipewa nafasi anafanya kitu. Narudia mchezaji kusajiliwa ni jambo moja na kuzaa matunda ya kazi ni bidii yake mwenyewe.”

Aliyekuwa kipa wa Yanga, Benjamin Haule alisema kitendo cha kupata nafasi katika klabu kubwa za Simba na Yanga, mchezaji anapaswa kuangalia kwa jicho la kubadilisha maisha na kukua kiakili.

“Kwa hapa Tanzania, ni Simba, Yanga na Azam FC zinaweza zikabadili maisha ya mchezaji kiuchumi. Sasa ni akili ya mchezaji mwenyewe kujituma na kufanya bidii hata mazoezi binafsi.

“Hakuna kocha atakayemkataa mchezaji anayeweza kumpa matokeo mazuri, ndio maana unaona mashabiki wa Simba walikuwa wanapiga kelele apangwe Phiri, wanajua uwezo wake,” alisema.

SOMA NA HII  NABI ATEMA CHECHE HIZI YANGA..."SIO RAHISI KUPATA USHINDI