Home Habari za michezo HIVI NDIVYO BAO 5 ZA YANGA ZINAVYOITESA SIMBA HADI LEO

HIVI NDIVYO BAO 5 ZA YANGA ZINAVYOITESA SIMBA HADI LEO

Habari za Michezo

Klabu ya Simba imewataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kutulia, ikisema huu si wakati wa kunyoosheana vidole kwa sababu Ligi Kuu bado mbichi na hata mechi za makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika bado hazijaanza, ambapo imeahidi kurekebisha kasoro zote zinazotajwa kuwapo.

Akizungumza nasi, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema wanachama na mashabiki wasicheze ngoma wasiyoijua badala yake kuwapa nafasi viongozi kurekebisha makosa.

Alisema kuwa klabu zote kubwa duniani zimepitia hatua hiyo wanayoipitia wao (Simba) saa hivi.

“Ningependa kuchukua nafasi hii kuongea na wanachama na mashabiki wa Simba kwa sababu wamehamaki na kukasirika kweli kweli… ni kweli kwa aina ya matokeo ambayo tumeyapata hakuna mtu wa Simba ambaye yanaweza kumfurahisha, kila mtu amechukia.

“Lakini waache vurugu, kejeli na matusi ambayo wanayatoa kwa viongozi wetu, si mienendo na tabia za Simba ni kweli tumevurugwa lakini ni lazima tuwe watulivu, ni vyema tuwe na subira ili viongozi wapate muda wa kufanya yaliyo sahihi kwa kuiboresha Simba yetu, tukianza leo huyu atoke huyu, ametuhujumu, huyu vile ina maana tunatengeneza mpasuko mkubwa,” alisema Ahmed.

Aidha, alisema bado hawajapotea kwenye ramani ya ubingwa kwa kuwa ligi bado mbichi hivyo wana muda wa kurekebisha mambo na kurejea kwenye mstari.

“Hatujapotea, ligi bado mbichi, Ligi ya Mabingwa ngazi ya makundi haijaanza kwa hiyo wanasimba tutulie, tutakaa sawa tu,” alisema Ahmed.

Wakati huo huo, Ahmed, alisema uongozi wa klabu hiyo unatarajia wakati wowote kuanzia kesho Jumatatu kumtangaza kocha wake mpya atakayechukua nafasi iliyoachwa wazi wa Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyeonyeshwa mlango wa kutokea, mara baada ya kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa watani zao wa jadi Yanga Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Alisema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho kumtangaza kocha huyo, ambapo tetesi zinasema kocha wa zamani wa timu hiyo, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck, kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi na Julien Chevalier ambaye ni kocha wa Asec Mimosas wote wanatajwa kuwania nafasi hiyo.

SOMA NA HII  ALLIANCE WAIVURUGA MWADUI FC, WALIPA KISASI CHA AZAM FC