Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA KESHO….CADENA AWASHIKA PABAYA WAIVORY… MO DEWJI KUMALIZA KAZI LEO…

KUELEKEA MECHI YA KESHO….CADENA AWASHIKA PABAYA WAIVORY… MO DEWJI KUMALIZA KAZI LEO…

Habari za Simba

ASEC Mimosas ya Ivory Coast, tayari ipo nchini kuwahi pambano la kwanza la Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya Simba, lakini kabla ya kutinga jijini Dar es Salaam kocha wa wenyeji wao Simba, Dani Cadena amewafanyia kitu mbaya kwa kulinasa faili zima la kikosi hicho na kuanza kulifanyia kazi.

Simba itaikaribisha Asec kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya Kundi C, lakini tayari Cadena amefanikiwa kuwasoma Wa Ivory Coast mapema na kubaina uimara na udhaifu wao kitu alichodai kitamsaidia kwenye mechi ya kesho na tayari ameshaongeza na mastaa wake mapema.

Kikosi cha Simba kinaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo huo na Cadena amesema amelianda jeshi lake kupata ushindi mzuri baada ya kuwasoma vya kutosha wapinzani hao kwa kujua nje ndani na amewapa maagizo wachezaji wa kikosi hicho namna ya kushughulika nao Kwa Mkapa hiyo kesho.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Cadena alisema kiu kubwa ya mashabiki ni kuona timu hiyo inaanza vyema hivyo wao kama benchi la ufundi wamejiandaa kimbinu, kiakili na kisaikolojia kwa wachezaji ili waweze kutimiza malengo waliyojiwekea.

“Tunaenda kwenye mchezo mgumu na mzuri lakini malengo yetu ni kuona tunaanza vyema kundi letu, kikubwa ambacho nawaomba mashabiki zetu waje uwanjani kutuunga mkono kwani hiyo ni silaha ya kuwapa nguvu wachezaji kupambana zaidi,” alisema Cadena na kuongeza amebaini Asec wapo vizuri katika ufungaji mabao.

“Ni timu yenye balansi nzuri kuanzia eneo la kujilinda na ushambuliaji, hivyo ni lazima kuandaa namna bora ya kukabiliana nao ipasavyo, tunahitaji mchezo huo kwa lengo la kurejesha heshima kwa mashabiki zetu walioanza kukata tamaa,” alisema Cadena aliyefichua amekuwa akitumia muda mwingi mazoezini kuzungumza na wachezaji na kuwapa mbinu kulingana na wapinzani wao walivyo.

Cadena alisema ameifuatilia timu hiyo na kubaini katika Ligi Kuu ya Ivory Coast ‘Ligue 1’, imecheza mechi 11 ambapo kati ya hiyo imeshinda saba, sare mmoja na kupoteza mitatu ikiwa nafasi ya pili na pointi 22, lakini safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 18 na beki yake kuruhusu saba tu.

Alisema hiyo imempa picha anakutana na timu ya aina gani na kukiri kwa sasa Asec haina staa wa kushughulika naye kwa vile inacheza kitimu zaidi, kitu ambacho wachezaji wa Simba wanapaswa kushuka uwanjani ikiwa makini ili ianze vyema mechi hizo kabla ya kukabiliana na wapinzani wengine wa kundi hilo.

Simba ipo Kundi B pamoja na Wydad Casablanca ya Morocco watakaocheza ugenini mechi itakayofuata na Jwaneng Galaxy ya Botswana, kitu kizuri ni kwamba timu hizo zote imeshawahi kukutana nazo kwenye michuano ya CAF kwa vipindi tofauti.

ASEC iliyotua nchini jana ina kumbukumbu ya kupoteza mabao 3-1 kwa Simba Uwanja wa Mkapa Februari 13, mwaka jana hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika, japo nayo ililipa kisasi kwa kuinyoa Simba 3-0 Machi 20, 2022. ziliporudiana nyumbani kwao.

Katika hatua nyingine mastaa wa Simba jana ama leo wanatarajiwa kupokea ugeni mzito kambini kwa bilionea wa klabu hiyo Mohammed Dewji ‘Mo’ kupanga kukutana nao ili kujadiliana mambo mbalimbali sambamba na kuwekeana ahadi ya mkwanja ili mambo yawe mepesi kwenye mchezo wa kesho na mingine.

Simba inanolewa na Cadena akiwa kaimu kocha mkuu, akisaidiwa na Seleman Matola baada ya mabosi wa timu hiyo kumtema Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na wasaidizi wawili, Oumane Sallemi na Cornelly Hategekimana baada ya kipigo cha 5-1 kutoka kwa Yanga.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA JUMANNE