Home Habari za michezo ISHU YA MAXI KUTAKIWA SIMBA UKWELI HUU HAPA…TIMU YAKE YA CONGO WAANIKA...

ISHU YA MAXI KUTAKIWA SIMBA UKWELI HUU HAPA…TIMU YAKE YA CONGO WAANIKA KILA KITU…

Habari za Simba

YANGA wako Algeria na kesho watapambana na CR Belouizdad ya huko kwenye mechi ya kwanza ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini huku nyuma watani wao, Simba kuna eneo wanataka kuwagusa ambako kama wakifanikiwa kutakucha.

Simba wamefanya jaribio zito la kutaka kumng’oa juu kwa juu kiungo wao Mkongomani, Maxi Nzengeli ambaye alipiga mabao mawili dhidi ya Simba kwenye ushindi wa mabao 5-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara hivi karibuni.

Simba wamepiga simu kwa klabu ya zamani ya Nzengeli ya Union Maniema ya DR Congo na kumwaga ofa nzito wakijua kwamba huenda kiungo huyo yuko jangwani kwa mkopo kama ilivyowahi kuzushwa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya wachambuzi.

Hata hivyo,  Simba wamejibiwa kwamba Nzengeli ni mali halali ya Yanga na kwamba kama kuna hatua za kumuuza licha ya Maniema watapata mgao wao lakini watu wa kwanza watakaosimamia biashara hiyo ni watani Jangwani.

Simba hawakuridhika wakaingia mfukoni na kutoa ahadi nzito kwamba mabosi hao wa Maniema basi walinzishe kwa kutaka kumchomoa kisha wao watamwaga fedha za kufuru mara mbili ya zile ambazo Yanga walilipa.

Pia, Nzengeli mwenyewe atakunja mkwanja mrefu huku wakitaka kumlipa kitajiri mara mbili na nusu ya mshahara ambao analipwa na Yanga ahadi ambayo mabosi wa Maniema baadhi yao akili ikawaruka wakacheki na watu wa Yanga kuwajulisha hali hiyo.

Baada ya jaribio hilo bosi wa juu wa Maniema amegoma kukubali mtego huo wa Simba akitaka kwanza kuzungumza na mabosi wenzake wa Yanga na hata mchezaji kwanza.

Simba iliwahi kumtaka Nzengeli wakati Yanga inataka kumchukua lakini ghafla mabingwa hao wakashtuka kisha rais wao injinia Hersi Said akamaliza biashara haraka na kumshusha nchini ili asiendelee kusumbuliwa akiwa huko kwao.

Mratibu wa Maniema, Guy Kapia ingawa hakutaka kuliongelea hilo kwa undani alikiri kuwa Simba bado wanamtaka Nzengeli lakini wazungumze kwanza na watani wao Yanga ambao pia alishawaambia kuhusiana na simu za Msimbazi.

“Simba wanamtaka Maxi muda mrefu hata wakati Yanga wanamchukua walikuwa bado na wao wanamtaka, walikuja lakini tumewaambia wawatafute Yanga waongee nao wakisema watamuuza sisi tutazungumza na Yanga kujua tutapa kipi ila yupo pale kwas mkataba wa Yanga wa miaka miwili,”alisema Kapia.

“Mimi sijajua kama Yanga wataweza kuwauzia kama sisi tulivyowauzia, hayo ni mambo yao sisi tunafurahia kuona Maxi sasa anaendelea kufanya mambo makubwa kule Tanzania,” alisema.

Ndani ya msimu wake wa kwanza akiwa na Yanga msimu huu Maxi amekuwa kwenye kiwango bora sambamba na kuingia haraka ndani ya kikosi cha kwanza, tayari ameshaifungia timu hiyo mabao 7 akiwa mmoja wa vinara wa ufungaji kwenye ligi sambamba na Stephanie Aziz KI na Jean Baleke wa Simba ambao wote wana idadi kama hiyo ya mabao.

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  MUKOKO ATINGISHA KIBERITI YANGA...ATOA SHARTI LA MKATABA MPYA..AGUSIA ISHU YA KUJIUNGA SIMBA...