Home Habari za michezo SAFARI YA UKAME WA MIAKA 25 KWA YANGA NDANI YA CAF KUVUNJWA...

SAFARI YA UKAME WA MIAKA 25 KWA YANGA NDANI YA CAF KUVUNJWA RASMI LEO….KAA MKAO WA KULA…

Habari za Yanga leo

SAA 4 usiku usiguse rimoti. Yanga itakuwa palepale iliposhinda siku ile dhidi ya USM Algers lakini wakakosa Kombe la Shirikisho Afrika sababu ya kikanuni tu.

Yanga ilicheza na USM Alger katika mechi ya pili ya fainali ya michuano ya msimu uliopita na kushinda bao 1-0 la mkwaju wa penalti ya Djuma Shaban.

Hata hivyo ushindi huo ulifanya matokeo ya jumla kuwa 2-2, kwani tayari ilishapasuka nyumbani kwa mabao 2-1 na Waalgeria wakabeba taji mbele ya Yanga.

Sasa leo usiku, kikosi cha Yanga imerudi tena jijini Algiers tayari kuvaana na wenyeji wao, CR Belouizdad katika mechi ya kwanza ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Kocha Miguel Gamondi amesisitiza kwamba Yanga iko tayari kukiwasha huku akionyesha kuwatisha wenyeji alipoweka wazi kwamba amefanya kazi yake ipasavyo kabla hawajakanyaga uwanjani usiku huu.

Ameweka wazi kwamba alikuwa na mtaalam maalumu aliyemfanyia kazi ya kuisoma kiundani CR Belouizdad ndani na nje ya uwanja na amejiridhisha kwamba nondo zote alizompa ni sahihi na ameshazifanya kazi.

Kwa mantiki hiyo,  hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya ulazima ataanza na Diarra, Yao, Lomalisa, Mwamnyeto, Bacca, Aucho, Mudathir, Pacome, Musonda, Maxi na Aziz KI.

Ndio maana anapata kiburi cha kuingia kwa kujiamini kwenye mchezo huo ambao Kocha wa CR Belouizdad, Mbrazili Marcos Paqueta akikiri kuhofia historia ya Yanga kwenye Uwanja wa Julai 5 1962 unaotumiwa kwa mchezo wa leo. Awali Yanga ilishinda bao 1-0 hapo dhidi ya USM Algiers kwenye fainali ya Shirikisho msimu uliopita.

Yanga itaanza mechi hizo za hatua ya makundi ikiwa na kumbukumbu kwamba mara ya mwisho kucheza hatua kama hii ilikuwa miaka 25 iliyopita. Yanga ilicheza makundi na kuweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza nchini mwaka 1998 baada ya CAF kurekebisha michuano hiyo kutoka Klabu Bingwa Afrika hadi kuwa Ligi ya Mabingwa mnamo 1997.

Na sasa timu hiyo inarudi ikiwa na kikosi imara ambacho msimu uliopita tu, kilishtua kwa kucheza fainali ya kwanza tangu klabu hiyo izaliwe 1935 katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ilibaki hatua moja tu Yanga kuchukua taji hilo lililochukuliwa na USM Alger kikanuni. Ilikuwa Juni 3, 2023 ambapo iliwashtua mashabiki wa USM Alger na kuwafanyia vurugu zilizowagharimu baadae.

Yanga haikuwahi kukutana na Belouizdad hapo kabla ambapo timu zote mbili zitakwenda kuandika historia ya kwanza kwenye mechi hiyo kabla ya kurudiana baadaye. Katikati refa leo atakuwepo raia wa Chad, Alhadji Allaou Mahamat.

Mabingwa hao wa Tanzania tayari wapoAlgeria kwa siku tatu kabla ya mchezo huo wakitua kwa mafungu matatu kutokana na wachezaji wengine kuwa timu za taifa.

HALI YA HEWA

Ni baridi kali kiasi lakini hali hiyo imeambatana na mvua za vipindi tofauti ambapo tayari kikosi hicho kimeonyesha kuanza kuzoea mazingira hayo tayari kwa mchezo huku kocha na viongozi wakisema si tatizo sana kwani wamejiandaa kisaikolojia.

Belouizdad hawako vizuri sana kwenye ligi kwani kwenye mechi zao tano zilizopita wameshinda tatu wakipoteza mbili lakini wakiwa na matokeo mazuri kwenye mechi zao mbili za Ligi ya Mabingwa walipowatupa nje BO Rangers ya Sierra Leone kwa jumla ya mabao 6-1.

TIZI LA JANA

Yanga ilianza kupiga tizi la uwanjani jana, kwani licha ya kufika juzi lakini vifaa vya mazoezi vilisahaulika jijini Dar es Salaam na vililazimika kuingia Algeria na kundi la wachezaji waliokuwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliyotoka kupasuka nyumbani mabao 2-0 mbele ya Morocco.

WAKUCHUNGWA LEO

Ni mshambuliaji, Leone Wamba raia wa Cameroon aliyefunga hat trick wakati wanatinga makundi, Kocha wake anahofia fitinesi yake, lakini amewaomba mashabiki waje kwa wingi uwanjani kuwapa nguvu wachezaji wa timu hiyo.

Mbali na Wamba anayeongoza kwa ufungaji ligi ya kwao sambamba na Boussouf Ishak wenye mabao mawili kwenye ligi, Yanga inatakiwa kuwa makini pia na Darfalou Oussama, kiungo Benguit Abdelraouf wenye bao moja kila mmoja.

Yanga itakutana na mshambuliaji Meziane Bentahar anayeivaa Yanga kwa mara ya tatu akihamia hapo akitokea USM Alger ambao walicheza na mabingwa hao wa Tanzania kwenye mechi mbili za fainali za Shirikisho Afrika msimu uliopita.

YANGA IKO VIZURI

Kwenye mechi zao tano zilizopita, Yanga haijaangusha alama yoyote kwenye ligi wakiringia safu yao ya kiungo iliyopewa jina la MAP (wakimaanisha Maxi Nzengeli, Aziz KI Stephanie na Pacome Zouzoua) ambao wako kwenye moto mkali msimu huu tangu uanze. Nyota hao watatu wamefunga jumla ya mabao 18 kati ya 26 katika Ligi, Aziz na Maxi wakiwa na saba kila moja na Pacome akitupia mawili.

Yanga itahitaji ushindi au sare katika mechi hiyo ili iwe kuongeza morali kabla ya kurudi nyumbani wiki ijayo kucheza na watetezi wa taji la michuano hiyo, Al Ahly ya Misri waliopo nao kundi moja.

SOMA NA HII  MASAU BWIRE NA RUVU YAKE WAIPELEKA YANGA KIGOMA...WADAI NI SUALA LA KIKANUNI....