Home Habari za michezo KISA SARE NA AL AHLY JUZI….KIGOGO YANGA ‘KANG’ATA ULIMI’ KISHA AKASEMA HAYA...

KISA SARE NA AL AHLY JUZI….KIGOGO YANGA ‘KANG’ATA ULIMI’ KISHA AKASEMA HAYA MAPYA…

Habari za Yanga

Sare ya 1-1 iliyopata Yanga nyumbani mbele ya Al Ahly ya Misri kwenye mechi ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika, haijawashtua mabosi wa klabu hiyo, kwani wamesema kwa hesabu walizonazo kwa sasa ni kwamba wakikaza wanavuna pointi tisa kupitia mechi nne zilizosalia kwenye hatua hiyo ya makundi.

Yanga ilipata sare hiyo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikichomoa bao kupitia Pacome Zouzoua katika dakika za lala salama baada ya Al Ahly kutangulia kupata bao dakika ya 87 kupitia Percy Tau, ikiwa ni wiki moja tangu ilipocharazwa mabao 3-0 na CR Belouizdad ya Algeria zilipovaana ugenini.

Matokeo ya mechi hizo mbili yameifanya Yanga kushika mkia wa kundi hilo kama ilivyokuwa mwaka 1998 ilipocheza makundi ya Ligi ya Mabingwa mara ya kwanza, ikivuna pointi moja tu, huku watetezi Al Ahly wakiongoza kundi ikiwa na pointi nne ikifuatiwa na Belouizdad na Medeama zenye pointi tatu kila moja.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo amesema kuwa, licha ya sare hiyo ya Ahly bado hawajapoteza malengo kwani hatma yao ya kuvuka kwenda robo ipo kwenye michezo minne iliyonayo kwa sasa akiamini wana uwezo wa kuvuna pointi tisa kati ya 12.

Gumbo alisema kwa sasa wakishirikiana na makocha wanapiga hesabu kuanza kubeba pointi kwenye mechi ijayo ugenini dhidi ya Medeama ya Ghana iliyotoka kuiduwaza CR Belouizdad kwa kuichapa bao 1-0, kabla ya kurejea nyumbani wiki ijayo kurudiana nao kisha kuwasubiri Waalgeria Februari mwakani.

Kigogo huyo wa Yanga, alisema nguvu ya kushinda mechi hizo wanazo kwa kiwango kilichoonyeshwa na timu hiyo katika mechi mbili zilizopita za kundi hilo na tayari wameshamtanguliza mtu wao mapema Ghana kuweka mambo sawa kabla ya timu kufuata kuanzia leo kuwahi mchezo huo wa Ijumaa.

“Imetuumiza sana, kushindwa kupata ushindi dhidi ya Al Ahly tunajua kilichotukwamisha tutarekebisha lakini hesabu zetu mpya sasa zipo kwenye mechi tatu kati ya nne zilizosalia kundini,” alisema Gumbo na kuongeza;

“Ili tuweze kufuzu robo fainali tunahitaji kushinda mechi tatu, tumeshazungumza na wachezaji. Kundi letu bado linatupa nafasi ya kufanikiwa malengo yetu sasa tutanakiwa kushinda mechi zetu tatu zijazo.”

SOMA NA HII  ISHU YA BALEKE KUTUA RAJA CASABLANCA YA MOROCCO....UKWELI WOTE HUU HAPA...