Home Habari za michezo BENCHIKHA AFURAHIA JAMBO JIPYA SIMBA….

BENCHIKHA AFURAHIA JAMBO JIPYA SIMBA….

Habari za Simba

Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, amekiri kuwa kikosi chake kinazidi kuimarika ila kuna tatizo moja la ufungaji ambalo ameahidi kulifanyia kazi, akisifu kiwango cha wachezaji wake, lakini akilia na mwamuzi aliyechezesha mechi ya raundi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca Jumamosi iliyopita, akisema aliongeza dakika tatu zaidi kitu ambacho si cha kawaida.

Akizungumzia mechi waliyocheza dhidi ya Wydad, Benchikha alisema mechi ilikuwa nzuri ingawa ilikuwa na baadhi ya changamoto zilizosababisha wakose matokeo mazuri.

“Tulicheza vizuri, tuliwafanyia Wydad ‘pressing’ hadi dakika ya 90, tukafungwa goli dakika za mwisho ambalo ni kama tulikosa umakini hadi mwisho wa mchezo.

“Ninachofurahia kwenye timu yangu ni kuweza kuzuia na kushambulia kwa kasi, eneo la kuweka mpira nyavuni ndilo tumeshindwa kufanikisha, nadhani kuna haja ya kukaa na kulifanyia kazi, lakini nimeridhishwa na timu ilivyocheza,” alisema kocha huyo raia wa Algeria ambaye hana muda mrefu tangu aitwae timu hiyo kutoka kwa Mbrazili Robertinho Oliveira.

Alisema kwa sasa wamerejea nyumbani kujiandaa na mechi ya marudiano ambayo atataka kujipanga vizuri kuhakikisha Simba inaibuka na ushindi.

“Mechi ya marudiano tutajipanga vizuri na kuhakikisha tunakuwa sahihi zaidi ili nasi tushinde kwa kuwa tutakuwa nyumbani kama ilivyokuwa kwao,” ameongea kocha huyo.

Benchikha alilalamikia kitendo cha mwamuzi wa mechi hiyo kuongeza dakika tatu baada ya tatu za majeruhi kumalizika.

“Aliongeza dakika tatu tukacheza hadi dakika ya 96, si kitu cha kawaida sijui kwa nini alifanya hivyo, lakini ndio hivyo,” alilalamika Benchikha.

Naye Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, hakusita kumpa sifa kocha huyo akisema ni mwanamapinduzi aliyefanya mapinduzi makubwa ndani ya kikosi hicho kwa muda mfupi tu.

“Ndani ya muda mfupi amefanya mapinduzi makubwa ndani ya kikosi chetu, utimamu wa mwili kwa wachezaji umepanda maradufu, ukabaji wa hali ya juu, ufundi umeongezeka kwa baadhi ya wachezaji wetu, kiwango cha mchezaji mmoja mmoja kimepanda, hali ya kujiamini imeongezeka na morali iko juu,” alisema.

Simba imerejea nchini jana alfajiri na wachezaji kupewa mapumziko ya siku moja kabla ya leo kuanza mazoezi kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar na kisha Jumanne ijayo kuikaribisha Wydad katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

SOMA NA HII  BAADA YA KUONA 'MBUGI' LA SIMBA JUZI...NABI AINGIA UBARIDI...KUIBUKA NA MBINU MPYA KWA KMC..