Home Habari za michezo SIMBA NA ADEBAYOR BILA KUCHOKA

SIMBA NA ADEBAYOR BILA KUCHOKA

Tetesi za Usajili Bongo

Kikosi cha Simba kinatarajia kushuka uwanjani jioni ya leo Ijumaa kuvaana na Kagera Sugar, huku mabosi wa klabu hiyo wakirudisha hesabu zao kwa nyota wa zamani wa US Gendermarie ya Niger, Victorien Adebayor.

Nyota huyo amekuwa akihusishwa na Simba tangu msimu uliopita, lakini dili lilikwama na sasa ikiwa chini ya Kocha Abdelhak Benchikha aliyewahi kufanya naye kazi RS Berkane ya Morocco imemuita mezani ili kufanya mipango ya kumsajili kupitia dirisha dogo linalofunguliwa kesho.

Simba inapiga hesabu za kumchukua Adebayor ikitaka kuimarisha eneo la winga ya kushoto ya timu hiyo ikiwa ni mipango ya kuitengeneza timu yenye ushindani. Benchikha aliwahi kumkuta Adebayor, RS Berkane ingawa hakumtumia sana lakini sasa ametaka kwanza kujiridhisha kama bado yuko kwenye ubora.

Wakati akiwa Berkane, Adebayor hakutumika sana akiwa anasota benchi mpaka alipotimka Afrika Kusini pale Amazulu.

Taarifa kutoka ndani ya Simba ni kwamba dili hilo limeanza upya, lakini linasubiri baraka ya kikao cha Benchikha na mabosi watakaoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ ambaye inaelezwa yuko nje ya nchi.

“Bado kuna mchakato wa kukamilika kwa usajili huo, huyu ni mchezaji ambaye kocha anamjua aliwahi kufanya naye kazi Morocco anataka kwanza kujiridhisha na tujiridhishe kama yuko kwenye kiwango cha kuja kufanya kikubwa hapa Simba,” alisema kigogo huyo wa ndani wa Simba (jina tunalo) na kuongeza;

“Maamuzi kamili yanaweza kufikiwa baadaye wikiendi hii tunasubiri mwenyekiti wa bodi arudi kuna kikao watafanya na kocha kufanya maamuzi haya yote.”

Nyota huyo mbali na kucheza kama winga wa kushoto, lakini anamudu ile ya kulia na kucheza kama mshambuliaji wa kati, kitu ambacho kimefanya mabosi wa Simba kumpigia hesabu zaidi, japo maamuzi ya mwisho yanaelezwa yatakuwa ni kwa Kocha Benchikha.

Mbali na Adebayor, Simba inahusishwa na usajili wa kiungo mkabaji, Eric Mbongossoum kutoka Chad na winga mzawa, Ladack Chasambi anayekipiga Mtibwa Sugar sambamba na beki wa kati Lameck Lawi aliyepo Coastal Union.

SOMA NA HII  WABUNGE PIA WAMEONYESHA UDHAIFU KUHUSIANA NA TAIFA STARS, HUU SI WAKATI WA MAKUNDI